SERIKALI YAAHIDI KUISUKA SEKTA YA ELIMU

 

NA FATMA HAMAD, PEMBA

SERIKALI YA MAPINDUZI Zanzibar imesema itaendelea kuboresha miundombinu ya Elimu ikiwemo Majengo, vifaa vya kisasa pamoja na maslahi kwa Walimu, ambavyo vitaibua vipaji na kuleta ufaulu mzuri kwa wanafunzi, wawe  na sifa za kuingia katika soko la ajira.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Utawala kutoka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Amos John Henok  kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo Khamis Abdulla Said, katika maadhimisho ya siku ya Walimu Duniani, huko Skuli ya Sekondari Uweleni Mkoani mkoa wa Kusini Pemba.

 Alisema lengo la serikali ya Mapinduzi ni kuona Zanzibar inakua na Wataalamu wengi  na ambao wamebobea katika fani mbalimbali kama vile Walimu, Madaktari, Mainjinia pamoja na wataalamu wa mitandao, hivyo itahakikisha inaboresha miundombinu ya kisasa, ili kufikia azma yake hiyo.

‘’Tutahakikisha tunaendelea kuweka mazingira rafiki katika sekta hii ya Elimu, ili vijana waweze kuuzika katika soko la ajira,’’ alieleza

Aidha aliwasisitiza walimu kuvitumia vifaa vilivyopo  maskulini katika ufundishaji wao, kama vile Komputa,  kila mtoto awe na uwezo wa kuvitumia, ili wajiajiri wenyewe pindi watakapomaliza masomo yao ya lazima.

Aidha Kwa upande mwengine alikipongeza Chama cha Walimu ZATU kutokana na mchango wake mkubwa katika kuimarisha sekta ya Elimu, hivyo aliwataka Walimu kujiunga na Chama hicho, ili kukiunga mkono kitoe matunda yatakayopeleka mbele wanafunzi na Taifa kiujumla.

‘’Kwakweli ZATU kinafanya kazi kubwa katika kuipeleka mbele sekta ya Elimu, na kwakweli tunatambua mchango na sisi kama serikali tutahakikisha tunaziunga mkono juhudi hizo mzidi kuendelea,’’alieleza.

Mapema Afisa Mdhamini wa wizara hiyo Mohamed Nassor Salim alisema ZATU ni miongoni mwa vyama vinavyopaswa kuigwa, kutokana na juhudi zake katika kuhakikisha sekta ya Elimu inapiga hatua Nchini.

‘’ZATU nyinyi ni mfano tosha mnapaswa kuigwa, hivyo endeleeni kutoa elimu muisadie wizara kupiga hatua kielimu,’’alisema.

Aidha aliwasisitiza Walimu kufuata Miko, maadili na sheria katika utekelezaji wa majuku yao,ili kuwa na imani thabiti jambo litalosaidia kuleta ufaulu mzuri kwa wanafunzi.

Kwa upande wake Rais wa Zatu Seif Mohamed Seif aliikumbusha serikali kuendelea kuboresha maslahi ya Walimu kuanzia ngazi ya Sekondari hadi maandalizi, ili wawe na ufanisi mzuri wa kufundishia, na kupelekea kuongezeka kwa ufaulu kwa wanafunzi.    

Nae Katibu mkuu ZATU Zanzibar Haji Juma Haji alisema licha mafanikio yaliopatikana bado sekta ya Elimu inakabiliwa na changamoto ya kushuka kwa hadhi, jambo litalopelekea Vijana wenye vipaji kutokua na hamasa ya kujiunga na taaaluma hiyo.

‘’ Tukiendelea kuidharau hadhi ya Mwalimu tutakuja kulipa gharama yake kesho, hivyo wakati wa kumthamini ni leo na sio kesho,’’ alifahamisha.


Maadhimisho hayo ya kitaifa ambayo kwa mwaka huu yalifanyika kisiwani Pemba, ikiwa kauli mbiyu ya mwaka huu ‘’hadhi ya Mwalimu ni msingi wa Elimu bora na Maendeleo Endalevu’’

MWISHO.





Comments

Popular posts from this blog

WANDISHI WA HABARI ANDIKENI HABARI ZA UCHAMBUZI

NAJIVUNIA KUONA WANANCHI WA MJINI KIUYU WAKIKANYAGA BARABARA YA LAMI

HOFU YA UDHALILISHAJI MTANDAONI INAVYOWANYAMAZISHA WANAWAKE