HOFU YA UDHALILISHAJI MTANDAONI INAVYOWANYAMAZISHA WANAWAKE

NA FATMA HAMAD, PEMBA

 Katika ulimwengu wa kidijitali, mitandao ya kijamii imekuwa sauti ya wengi, ni mahali ambapo watu hujadili siasa, biashara, elimu na masuala ya kijamii.

 Ingawa kwa wanawake wengi, majukwaa haya yamekuwa pia uwanja wa matusi, vitisho na udhalilishaji unaowafanya waogope kujieleza hadharani.

Mara nyingi mwanamke anapotoa maoni kuhusu suala la kijamii au kisiasa, hukumbana na mashambulizi yanayolenga jinsia yake badala ya hoja aliyoitoa.

Matokeo yake, baadhi yao huamua kunyamaza, kufunga akaunti au kujiondoa kabisa kwenye mijadala ya umma.

 Kwa sasa Tatizo hilo linaonekana kuwa changamoto kubwa ya haki za kidijitali na usawa wa kijinsia duniani.

 Utafiti wa kimataifa uliofanywa na UNESCO kwa kushirikiana na International Center for Journalists (ICFJ) mwaka 2021, uliowahusisha wanawake wanahabari 901 kutoka nchi 125, ulibaini kuwa asilimia 73 walikuwa wamewahi kukumbana na vurugu au udhalilishaji mtandaoni kutokana na kazi zao.

 Utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia 20 ya waliohojiwa walikumbana na mashambulizi ya ana kwa ana yaliyotokana na vitisho vilivyoanza mtandaoni.

 Ripoti hiyo ilionya kuwa udhalilishaji wa mtandaoni una athari kubwa kwa uhuru wa kujieleza kwa sababu wengi wa wanawake huanza kujidhibiti au kujiondoa katika mijadala ya umma kutokana na hofu ya kushambuliwa.

 Utafiti wa Amnesty International kuhusu matumizi ya Twitter (sasa X) uliochapishwa mwaka 2018 uligundua kuwa wanawake wanasiasa na wanahabari walipokea zaidi ya ujumbe milioni 1.1 wenye lugha ya matusi au udhalilishaji ndani ya mwaka mmoja pekee, hii ilikuwa sawa na ujumbe mmoja wa matusi kila sekunde 30.

 Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, makosa 1,281 yaliripotiwa ikilinganishwa na makosa 1,369 yaliyoripotiwa mwaka 2023. ikiwa ni upungufu wa makosa 88 sawa na asilimia 6.4, (Jedwali Na. 2.19).

 Chanzo: Jeshi la Polisi Tanzania

 WANAWAKE WAKIELEZA HOFU YAO JUU YA MITANDAO YA

 KIJAMII

 Batuli Mussa Sharif (46) mkaazi wa Kijichame Sizini anasema hanatabia ya kutumia mitandao ya kijamii kuweka mambo yake, kwani anahofu ya kufanyiwa udhalilishaji.

 ‘’Mwakajana  niligombea uwakilishi ingawa sikutumia  mitandao ya kijamii kujitangaza, nilihofia kuja kuchorwa vikatuni nikakashifiwa,’anasema.

 Maryam Juma Kombo (30) mkaazi wa Sizini anasema aliandamwa na kampeni za chuki mtandaoni baada ya kuripoti masuala ya kisiasa.

 Anasema mashambulizi hayo yalijumuisha matusi, vitisho na taarifa za uongo zilizolenga kumdhalilisha na kumtisha.

 "Nilianza Kuogopa Kufungua Simu, baada ya kuona matusi niliyokua nikitupiwa,"anasema.

 Maryam Nuhu Hamad (32) mkaazi wa Ole anasema

 mwaka jana alikua mgombea wa Udiwani na alijenga uthubutu wa kutumia mitandao kunadi sera zake, licha ya lugha chafu alizo akitupiwa.

 Katika mkusanyiko wa simulizi uliochapishwa na UNESCO kupitia kampeni ya #JournalistsToo, wanawake wanahabari kutoka nchi mbalimbali walieleza kuwa walipokea vitisho vya ubakaji, mauaji na mashambulizi dhidi ya familia zao,  Baadhi yao walikiri kuanza kujichunguza kabla ya kuchapisha habari au kutoa maoni kwa kuhofia mashambulizi mapya.

 JAMII

 Asha Khamis mkaazi wa Wesha (42) anasema licha ya mitandao ya kijamii kuwa ni fursa bado kumekua kukijitokeza wimbi la udhalilishaji, jambo linalowatia hofu wanawake kuitumia fursa hiyo kwa woga.

 ‘’Kumekua na watu kazi yao ni kutoa maneno  matusi kwa wenzao ambao hutoa mawazo yao, hali inayowatia hofu wanawake juu ya mitandao ya kijamiianasema.

 Mohamed Ali wa Wingwi anasema baadhi ya wanawake wanapunguza ushiriki wao mtandaoni kutokana na hofu ya kushambuliwa.

 ‘’Kunawanawa ke wanamambo muhimu ya kuvitanga vikaonekana na Kua mfano kwa wengine,  ila wanashindwa kuoneka kwa kuhofia kukashifiwa,’’anaeleza.

 WANAHARAKATI

 Saleh Hamad Juma Kaimu Mkurugenzi wa Jumuia ya Wasaidizi wa Sheria wilaya ya Micheweni  anasema Mitandao ya kijamii ilikusudiwa kuwa jukwaa la mawasiliano na ushirikishwaji wa watu wote, ingawa ongezeko la udhalilishaji wa wanawake mtandaoni linaendelea kuwatisha wengi na kuwafanya wajifiche kimya kimya.

 ‘’Ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa, hofu ya udhalilishaji itaendelea kuwanyima wanawake nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi,’’anaeleza.

 WATAALAMU WA MASUALA YA MTANDAO

 Mtaalamu wa masuala ya mtandao kisiwani Pemba Mustafa Mohamed Abdul Rabi  Moyo, anasema udhalilishaji ambao unatumika kwa sasa mitandaoni ni wa mashambulizi ya matusi, na huu unakuja pale mwanamke anapotuma  picha za maungo yake  akiwa utupu.

 ‘’Licha ya kua wanatangaza biashara zao ni vyema wavae nguo za stara,  zenye heshima, ili kuepuka udhalilisha ambao unaonekana kutokea siku hadi siku katika mitandao ya kijamii,’’anasema.

 Anasema Teknolojia mpya ya Akili bandia (AI)  inaweza ikatoa mwanya kwa wahalifu kupata fursa ya kuwadhalilisha wengine, hivyo wanawake wahakikishe wanatumia mitandao ya kijamii kwa uwangalifu ili kuepuka udhalilishaji.

Anasema asilimia 70 ya wananchi wa Pemba wanatumia mitandao ya kijamii kwa shughuli zao mbalimbali, hivyo mwanamke anaponyamazishwa kwa vitisho au matusi, jamii hupoteza mchango wake katika mjadala wa maendeleo,’’anasema.


SERIKALI

 Mrakibu wa Polisi Out Gromic Abock ambae ni mkuu wa Polisi jamii Kaskazini anasema ipo haja Jamii kuzingatia matumizi sahihi ya mtandao, kwa kuepuka kuangalia maudhui yaliokinyume na kanuni na Sheria za Nchi.

 CHANZO NIPASHE

 Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Tanzania, Rose Reuben, anasema bado kuna changamoto zinazoibuka zikichagizwa na sheria mbalimbali, ambazo zina mapengo na kukuza ukatili wa kijinsia kutokana na maendeleo ya teknolojia.

 “Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, yameathiri jamii hasa wanawake na wasichana ambao ndio mara nyingi wamekuwa walengwa wa picha zinazowadhalilisha,” ameeleza.

“Kuna ongezeko kubwa la unyanyasaji wa kijinsia, kwa njia ya mitandao ya kijamii. Tunaungana na Watanzania, kukemea vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na wasichana, hasa kupitia mitandao ya kijamii.


 Rose, anasema hayo, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, zinazolenga kuimbusha jamii kuachana na matendo ya ukatili, kama vile vipigo, ukeketaji, ubakaji, ulawiti, mimba za utotoni na rushwa ya ngono.

Kutokana na kuibuka kwa wimbi la udhalilishaji mtandaoni Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Tamwa Zanzibar  umekuja na mradi wa "Tunaweza Pamoja" unaotekelezwa ma UN Women kwa kushirikiana na TAMWA Zanzibar kwa ufadhili wa Serikali ya Norway chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa unaolenga kujenga jamii salama dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na wasichana.

NINI KIFANYIKE?

 Ili kudhibiti vitendo hivyo, ni vyema kuimarishwa  kwa sheria za kukabiliana na unyanyasaji mtandaoni, kuongeza elimu ya matumizi salama ya mitandao ya kijamii na kuwawajibisha wanaotumia haki za wanawake wanasema.

 MIKAKATI

 Tanzania inachukua udhalilishaji wa kijinsia mtandaoni kama tishio linalokiuka haki za wanawake, na mikakati yake mikuu inajumuisha Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya 2015, Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni ya 2020, na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKVWCU).

 Kifungu cha 23 cha Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya 2015: Kinapiga marufuku unyanyasaji mtandaoni na kinaeleza kuwa mtu yeyote atakayebainika kufanya hivyo atakabiliwa na kifungo cha miaka mitatu (3) jela, faini isiyopungua shilingi milioni tano, au vyote kwa pamoja.

 Sheria ya Maudhui ya Mtandaoni ya 2020: Inakataza kurusha picha, video za utupu, au kutumia lugha za matusi na kejeli zinazodhalilisha utu.

 MIKATABA

 Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha kinasema kila mtu yuko huru kutoa maoni yake.

Mikataba ya kimataifa na Haki za Kiraia na kisiasa (ICCPR) Kifungu cha 19(9) kinasema kila mtu anahaki ya uhuru wa kutoa maoni.

UZOEFU KATIKA NCHI NYENGINE

Kenya na Uganda zimefanikiwa kudhibiti udhalilishaji mtandaoni kupitia utungaji wa sheria kali, ushirikiano na taasisi za kiusalama, na kufuatilia wahalifu.

 Licha ya mafanikio haya, utekelezaji wake umekuwa na changamoto kubwa za kisheria na ukosoaji kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu.

 Kenya inatumia Computer Misuse and Cybercrimes Act No. 5 of 2018, iliyofanyiwa marekebisho ili kupambana na unyanyasaji wa mtandaoni, ulaghai, na uchochezi wa kujiua.

 Uganda inatumia Computer Misuse Act 2011, ambayo inashughulikia unyanyasaji wa mtandaoni (cyber harassment), udukuzi, na unyanyasaji wa watoto.Mwaka 2022, Uganda ilipitisha sheria kali zaidi inayokataza habari zenye nia mbaya, zenye kuleta uhasama wa kidini, kabila, na zinazoingilia faragha ya mtu. 

MWISHO.

 

 

Comments

Popular posts from this blog

WANDISHI WA HABARI ANDIKENI HABARI ZA UCHAMBUZI

UROHO WA MALI KWA WANAUME UNAVYONYIMA WANAWAKE ARDHI

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO