NA FATMA HAMAD, PEMBA
MTAALAMU wa masuala ya Utafit kutoka Taasisi
ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii Tanzania (Economic and Social Research Foundation)
Richard Ngilangwa amewataka waandishi wa
habari kuandika habari za uchunguzi na zenye ukweli ambazo zinazingatia takwimu
na tafiti, ili zilete tija kwa umma.
Mtaalamu huyo aliyasema
hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo ya habari za Utafiti
yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya ZRA Gombani Chakechake Mkoa wa Kusini
Pemba.
Alisema, Tafiti
zinafaida kubwa kwa jamii, hivyo ni vyema kwa waandishi wa habari kujikita
katika eneo hilo la uwandishi wa habari za utafiti na kuzichambua kwa ajili ya kufichua
shida za wananchi ili zipatiwe kwa ufumbuzi.
‘’Tafiti zinazofanywa ni
haki ya kila mmoja na sio kubakia Makabatini, hivyo zichukueni mzichambue na
mziandikie zipate kujulikana, ili kama kuna jambo linahitaji kufanyika basi
lifanyiwe kazi kwa urahisi na kwa wakati muafaka,’’alisema.
Kwa upande wake Mkuu
wa Kitengo cha Tafiti na Uratibu kutoka Tume ya Mipango Zanzibar Omar Juma Ali alisema,
tafiti zinazofanywa zinamchango mkubwa wa kuwasaidia wandishi wa habari kupata vyanzo sahihi vya kuibua habari ambazo zitaleta maslahi bora kwa
umma.
Alisema, endapo waandishi
wa habari watazitumia tafiti hizo kwa usahihi, zitasaidia kupatikana kwa taarifa
na kufahamu matukio yaliyoibuliwa, kuifahamisha jamii na kusaidia kuchukua
hatua juu ya jambo lililofanyiwa utafiti.
‘Ndugu zangu waandishi
wa habari katika tafiti muna uwezo wa kupata vyanzo vya kuandika habari, hivyo
mkizitumia kwa usahihi mtauwelewesha umma juu ya jambo lililoibualiwa baada ya
utafiti,’’alisema.
Alisema, imeonekana waandishi
wa habari hawana uwelewa juu ya kuandika habari za tafiti, hivyo Tume ya
Mipango Zanzibar kwa sasa imeweka mpango mkakati wa kuwaelimisha waandishi wa
habari juu ya matumizi sahihi ya Takwimu kuzifahamu na kuzifanyia kazi, kwani
kutasaidia kuibua kero zilizojificha, ambazo ni kikwazo kwa wananchi.
Nao waandishi wa
habari waliohudhuria mafunzo hayo walisema, mafunzo yamewafumbua macho huku
wakiahidi kuyafanyia kazi kwa kuwandika vyema habari zinahusiana na takwimu na
kuleta mafanikio kwa jamii yao.
MWISHO.
Comments
Post a Comment