Jeshi la Polisi lamsaka aliehusika na mauwaji ya mtoto wa kidato cha kwanza

 


NA FATMA HAMAD, PEMBA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba linaendelea na uchunguzi wa tukio la kuuwawa mtoto wa kike anaejulikana kwa jina la Raiyan Hemed Amour mwenye umri wa miaka 15 mkaazi wa kijiji cha Kwale Mpona shehia ya Finya Wilaya ya Wete, aliekutwa kwenye kichaka amefariki huku kiganja cha mkono wake wa kulia kukatwa na kitu chenye ncha kali.

Kamanda wa Polisi Mkoa huyo  Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) William Mwampagale alisema kuwa, marehemu huyo alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika skuli ya Sekondari Kizimbani Wete, ambapo kabla ya kifo chake, Oktoba 2, 2026 saa tatu usiku, baba mzazi wa mtoto huyo alikwenda kituo cha Polisi Wete kutoa taarifa ya kupotea kwa mtoto huyo.

“Imeelezwa kuwa Oktoba 2, mwaka huu mtoto huyo aliondoka saa 12:00 asubuhi kwenda skuli, ambapo hakurudi tena nyumbani kwao mpaka mwili wake ulipoonekana kwenye kichaka akiwa ameshafariki dunia,” alisema.

Kamanda huyo alieleza kuwa, mwili wa marehemu huyo ulifanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Wilaya ya Wete iliyopo Kinyasini na tayari umeshakabidhiwa jamaa zake kwa ajili ya taratibu nyengine za mazishi.

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kutumia vituo vya Polisi kuripoti matukio yoyote ya kihalifu yanayotokea katika maeneo yao, na kuacha kujichukulia sheria mikononi.

 Sambamba na hilo aliwasisitiza wananchi kuliachia Jeshi hilo lianzishe taratibu za kiupelelezi, ili watuhumiwa watafutwe,na watakapokamatwa wafikishwe Mahakamani.  

Awali Daktari wa kitengo cha wagonjwa Mahututi na Dharura katika hospitali ya Wilaya Kinyasini Wete, Brighton Victor Kinyunyu alisema, siku ya tarehe 4 saa 5:00 mchana alipokea mwili wa marehemu wa binti huyo mwanafunzi wa skuli ya Sekondari Kizimbani Wete ambae inasemekana alipotea Oktoba 2, mwaka huu.

Alisema kuwa, mwili wa marehemu ulifikishwa hospitalini hapo na Jeshi la Polisi pamoja na jamaa zake, ambapo uchunguzi wa awali uliofanyika walibaini kwamba, marehemu alipoteza kiganja cha mkono wa kulia na pia alikuwa na majeraha katika sehemu ya juu ya mkono huo.

“Pia nguo za marehemu zilikuwa zimejaa damu na hatukuweza kuona jeraha jengine lolote, hivyo marehemu alipoteza maisha baada ya kupoteza damu nyingi kutokana na majeraha aliyoyapata, yaliyotokana na kuchomwa kitu chenye ncha kali kwenye mshipa mkubwa wa damu, “alisema daktari huyo.

Daktari huyo aliishauri jamii kwamba, wanapaswa kuwalinda watoto wao na wala wasijichukulie Sheria mikononi kuondoa uhai wa watu wengine.

Awali mwananchi Rashid Hamad Salim alioshuhudia tukio hilo alisema kuwa, wakati wanakwenda kwenye mashamba yao kwa ajili ya kufanya kazi zao za kila siku za kilimo, ghafla aliitwa na mdogo wake na kumwambia kwamba, yule mtoto alopotea amemuona.

Alihadithia kuwa, baada ya kuambiwa hivyo alianza kujawa na hofu, kwani hakujua atakuwa katika mazingira gani huku akimuuliza mdogo wake hali aliyomkuta nayo binti huyo, ambapo alimwambia kuwa ameshafariki.

“Baada ya hapo tulikwenda kumuona na tukabaini kuwa ameshafariki huku akiwa amekatwa kiganja chake cha mkono, lakini alikuwa na nguo zake kamili na pia amevaa soksi miguuni,” alisema.

Kwa upande wa mdogo wake Rashid, ambae alimwita kaka yake baada ya kuuona mwili wa mtoto huyo alisema, yeye alikuwa anaenda kupiga tanu, lakini baada ya kufika eneo hilo alikuta mwili huo kichakani na ndipo alipokimbilia kumwita kaka yake.

“Tukaenda kumuangalia na tukaanza kupiga simu kwa watu wa Kwale tunaowajua lakini simu ilikuwa hazipatikani, ndipo akapita kijana mmoja mkaazi wa kijiji hicho tukamwita na akampigia baba wa marehemu huyo, na akaja jirani yake kwenye eneo hilo

Nae Katibu Tawala Wilaya ndogo Kojani Ali Mmanga Khamis alisema, tukio hilo ni la kuhuzunisha na Serikali itajitahidi kumtafuta mtu aliehusika na mauwaji hayo, huku akiiasa jamii iliachie Jeshi la Polisi lifanye kazi yake ya uchunguzi, na pale litakapokamilisha watatoa taarifa kwa wananchi.

“Tulipata taarifa Oktoba 2, kupotea kwa mtoto huyo na tulichukua jitihada za kuanza kumtafuta, na kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi liendelee na utaratibu, na ndio tumepata taarifa hii ya kufariki kwake,” alisema Katibu huyo.

Baada ya tukio hilo, wananchi wa kijiji hicho waliiomba Serikali kuwajengea skuli na barabara, kwani wameshaingiwa na hofu kutokana na usalama umeshakuwa mdogo kwao na watoto wao.

Walisema, vijana wa Kwale wanalazimika kwenda Wete kupata elimu, ambapo hutumia masafa marefu yaliyo na vichaka ambavyo ni hatari kwani hakuna usalama.

Wazara ya Elimu na Mafunzo Amali Zanzibar, imesema imepokea  kwa huzuni na masikitiko taarifa ya kifo cha Mwanafunzi Raiyan Hemed Amour miaka 15 wa darasa la Tisa katika skuli ya Sekondari Kizimbani Wete Kaskazini Pemba.

Taarifa ya kitengo cha Habari, Uhusiano na Mawasiliano, Wizara hiyo imeeleza tukio hilo limetokea wakati mwanafunzi akirudi skuli na aliripotiwa kupotea na baadae kupatikana akiwa amefariki.

‘’Wizara inalaani kitendo hicho cha kikatili, na inatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, wanafunzi, walimu na jamii kiujumla kutokana na msiba huu mkubwa’’ilifahamisha taarifa hiyo.

Ilieleza kwamba Wizara inaviomba vyombo vya ulinzi na Usalama kufanya ulinzi wa kina na kwa haraka, ili kuwabaini na kuwakamata wahalifu waliofanya mauaji hao na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pia Wizara imetoa wito kwa jamii kushirikiana na vyombo vya kisheria kwa kutoa taarifa zozote muhimu zitakazo saidia uchunguzi.

                                          MWISHO.

 

 


Comments

Popular posts from this blog

WANDISHI WA HABARI ANDIKENI HABARI ZA UCHAMBUZI

NAJIVUNIA KUONA WANANCHI WA MJINI KIUYU WAKIKANYAGA BARABARA YA LAMI

HOFU YA UDHALILISHAJI MTANDAONI INAVYOWANYAMAZISHA WANAWAKE