HADIA OMAR DADI, SHEHA WINGWI NJUGUNI KIONGOZI DHAHABU KWA WANANCHI WAKE
Katika miaka ya hivi karibuni, ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi, unaendelea kupewa kipaumbele nchini Tanzania na Zanzibar.
Kupitia Katiba, sera za usawa wa kijinsia pamoja na mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa CEDAW na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 5), ambayo yanasisitiza ushiriki sawa wa wanawake katika uongozi na maamuzi ya maendeleo.
Kwa muda mrefu, nafasi za uongozi zinaonekana kuwa ni za wanaume zaidi, ingawa wanawake wengi wanaendelea kuthibitisha kuwa wana uwezo mkubwa wa kusimamia maendeleo ya jamii pale wanapopewa nafasi.
Miongoni mwao ni Sheha wa Njuguni, Bi Hadia Omar Dadi, (48) mzaliwa wa Wingwi, ambaye wananchi wengi wanamwelezea kama kiongozi anayesikiliza, anayeshirikiana na jamii na anayesimamia maendeleo kwa vitendo.
Safari ya Hadia Omar Dadi, haikuanza alipoteuliwa kuwa sheha, ilianza akiwa mwanachama wa kikundi cha ushirika katika jamii yake.
Bi Hadia, kwa sasa anaishi kijiji cha Michungani Wingwi anaishi na mume wake, na nimama wa watoto sita.
Ingawa Hadia anafamilia inamtegemea, aliweza kuihudumia na huku akitekeleza vyema majukumu ya kwenye kikundi chake, ikiwemo kuhamasisha maendeleo.
Anasema kwa kutokana na alivyokua mkakamavu na anajali wenzake, wanajamii wakamkubali na mwisho wa siku wakamchagua kua katibu wao katika kikundi chao cha ushirika.
‘’Majukumu hayo yalinipa nafasi ya kushiriki mafunzo na ziara mbalimbali ndani na nje ya Pemba, jambo lililonijengea uzoefu katika masuala ya maendeleo ya jamii, usimamizi na uongozi,’anasema.
Anasema wakati akitumikia nafasi hiyo ya ukatibu na kuonekana anaongoza vizuri, aliteuliwa tena kuwa Katibu wa Sheha shehia ya Njuguni.
‘’Baada ya kuteuliwa tena nafasi hiyo niliendelea kuonyesha uwezo mkubwa wa kuwahudumia wananchi na kushirikiana na viongozi wa Serikali, katika kutatua changamoto za shehia, bila itikadi yoyote,’anasema.
Anafahamisha kwamba kutokana na utendaji wake uliotambuliwa, alipata nafasi ya kuteuliwa kuwa Sheha wa Wingwi Njuguni, ambako anaendelea kuongoza kwa karibu na wananchi, anahamasisha ushirikiano kati ya Serikali na jamii katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Anasema miongoni mwa mafanikio yanayoonekana zaidi katika kipindi cha uongozi wake ni kuimarika kwa sekta ya elimu, kupitia ushirikiano kati ya Serikali na wananchi.
Sasa anajivunia kwa ushirikiano wake na serikali kuu kujengwa kwa Skuli ya Sekondari Dk. Shein na skuli ya Msingi Kije.
Anasema kabla ya kupatikana kwa skuli hizo, wanafunzi walikuwa wakitegemea skuli ya Wingwi, jambo lililosababisha msongamano madarasani.
‘’Skuli hizo muakilishi wa jimbo la Wingwi alikua anataka zijengwe katika shehia yake ya Sizini, mimi kama mwanamke nilipambana hadi nikafanikiwa zikajengwa shehiani kwangu,’’anasema.
Anasema anajivunia kuwepo kwa skuli hizo, katika shehia yake zinaleta faida kwani, zinaongeza ufanisi wa ufundishaji, na idadi ya ufaulu kwa wanafunzi kwenye mitihani yao ya Taifa.
WALIMU WA SKULI WAKIELEZEA SHEHA ALIVYOPAMBANA
Juma
Othman Nahoda, Msaidizi mwalimu mkuu skuli ya sekondari Wingwi, anasema kabla
ya kuwepo kwa skuli hizo ilikuwa wakifundisha madarasa, yenye wanafunzi wengi
takribani 70 ama 78 kila darasa, ambapo kisheria darasa linatakiwa liwe na 45.
‘’Mwaka jana wanafunzi wetu wa darasa la kumi wote walifaulu, darasa la kumi na mbili walifaulu 49 kati ya wanafunzi 81, hili ni kutokana na kuondokana na msongamano,’’anasema.
Anasema walikua wanaingia mikondo miwili na maranyengine wakilazika kuingia mitatu, ingawa kwa sasahivi wanakwenda mara moja tu.
Mwalimu mkuu skuli ya Wingwi msingi, Mohammed Ali Rubea, anasema uwepo wa skuli hiyo Msingi na Maandalizi ya Kije, imepunguza msongamano wa wanafunzi katika skuli yao.
''Tulikua tunaingia mikondo mitatu, na kila darasa lilikua linawanafunzi 150 hadi 160 na wengine, tulikua tunawaweka nje, kwani madarasa ilikua hayatoshi,’’anaeleza.
Anasema kujengwa skuli ya Kije wamepunguza mzigo, ambapo kila darasa lina wanafunzi 70 na wamekua wakiingia mikondo miwili tu, badala ya mitatu.
‘’Sheha wetu ni mwanamke, ila huyu mama anapambana katika suala la elimu na hata kwenye yanja nyengine, anapenda mabadiliko,’’anasimulia.
Anaeleza kwamba sasa hata ufaulu umeongezeka kwani, mwaka 2023, wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la saba walikua ni 194 waliofauli 60 wanaume 24 na wanawake ni 36.
Mwaka 2024 waliofanya mtihani ni 170 waliofaulu 48 wanawake 30 wanaume 18.
Ikiwa kwa mwaka 2025 waliofanya mtihani ni 227 waliofaulu 51 wanawake 39 wanaume 12, halihiyo ni tofauti na miaka nyuma, kwani ilikua wakipasisha wanafunzi wawili ama wamefika mbali basi ni wanne licha ya uwingi wa wanafunzi waliokua nao.
WANAFUNZI
Hadia Othman (sio jina halisi) mwanafunzi wa darasa la kumina mbili, skuli ya Wingwi Sekondari anasema kwa sasa wanaingia mkondo moja tu, tofauti na zamani kwani ilikua wakiingia mara mbili.
‘’Tunafahamu tunayosomeshwa na walimu wetu na tumekua tukifanya vizuri mitihani yetu, kwani darasani hatuko wanafunzi wengi, kama ilivyokua zamani,’’anasema.
Ali Othman Hamad mwanafunzi wa skuli ya msingi wingi anasema, zamani wakiingia skuli mikondo mitatu, huku wengine wakiwa wanasoma chini ya miti.
‘’Lile kundi kubwa la wanafunzi tumepungua, tunasomeshwa angalau tunafahamu ni tofauti na zamani tulikua tuko 160 hapo mwenyekipaji chake ndo anaefahamu,’’anaeleza.
WAZAZI WANASEMAJE
Time Ali ni mmoja wa mzazi wa mwanafunzi ambae akisoma Wingwi Msingi anasema kuwepo wa Skuli mpya ya Kije inasaidia wanafunzi kuondokana na changamoto ya msongamano kwenye madarasa.
Mzazi mwengine Ali Juma Ali anasema licha ya kuondokana na msongamano mkubwa wa wanafunzi wa bali, watoto wanaoishi eneo hilo la Kije, ilikua wakilazimika kwenda skuli ya Wingwi ambako ni masafa marefu.
''Skuli hii mpya ya Kije tunaifurahia kwani watoto wetu wameondokana na kwenda masafa ya mbali ambako ni Wingwi,'anaeleza.
Anasema anamshukuru sheha wao kutokana na juhudi anazozichukua Kuona watoto wa wingwi wanapata haki yao ya elimu na katika mazingira rafiki.
WANANCHI
Khator Ali Hassan mwananchi wa Wingwi Maisha Siri anaeleza kuwa moja ya sifa za kiongozi wao, ni kusikiliza kero za wananchi wake na kuzifanyia kazi.
''Kiongozi wetu huyu hajali chama wala kabila, anatujali na anatusikiliza shida zetu, na ndio maana akasikiliza kilio chetu na sasa tumeshapata skuli mpya, mbili ndani ya shehia yetu,'anasema.
Salama Mbarouk Khamis mkaazi wa Wingwi Michungani anasema, kupatikana kwa skuli hizo mpya kunaondosha idadi kubwa ya wanafunzi, katika skuli ya Wingwi.
''Tunashukuru sheha wetu kwa kupambana hadi tumejengewa skuli nyengine, na sasa watoto wanasoma kwa amani,''anafahamisha.
Anasema maendeleo hayo katika elimu,na huduma nyingine yametokana na ushirikiano alioujenga kati ya wananchi na Serikali.
WANAHARAKATI
Afisa mawasiliano kutoka Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA ZANZ Sofia Ngalapi anasema wamekua mstari wa mbele katika kumuinua Hadia na wanawake wengine.
Anasema katika tamko lao la Machi 2024, linasisitiza kwamba ‘’sera za jinsia lazima ziwepo katika sekta zote, ili wanawake wasiachwe nyuma katika uongozi.’’
‘’Tunataka wanawake washiriki kila sehemu ili walete mabadiliko katika
jamii,’’ anasema
Katibu
Twala wilaya ya Micheweni Sheha Mpemba Faki anasema siku zote eneo linalokua na
kiongozi wanawake ni rahisi kupatikana kwa mabadiliko.
‘’Tutake tusitake wenzetu wanawake wanabidii, na siku zote ukitaka sehemu, iendelee na iwe na mabadiliko basi apewe kiongozi mwanamke,’’anasema.
Anasema uongozi wa sheha wa Njuguni ni mfano tosha na unaendelea kuonyesha kuwa, wanawake wanaweza kushika nafasi za juu za maamuzi na kusimamia maendeleo ya taifa.
Historia ya Tanzania na Zanzibar, inaonesha kuwa wanawake wengi wanaonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza katika ngazi mbalimbali.
Hilo si kwa sheha wa Njuguni pekee bali hata Rais wa
Tanzania
Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa
mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa
Tanzania.
Shehia ya Njuguni inayoidadi ya watu 3518 wanawake 1875 wanaume wakiwa ni 1643 huku idadi ya kaya zikiwa ni 618.
MIKATABA
Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa lililotolewa azimio Oktoba 31 mwaka 2000, limesema
kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi, inazidisha demokrasia ya
nchi, uchumi, amani na utulivu.
Eneo jengine ni katiba
ya Zanzibar ya 1984, kifungu cha 21 (1) kinaeleza kila mzanzibari
anayo haki na uhuru wa kushiriki kikamilifu, katika kufikia uamuzi juu ya mambo
yanayomuhusu mwanamke na taifa lake.
Kwa mujibu
wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi za Kusini mwa
Afrika, uliotiwa saini mwaka 2008, kupitia ibara ya nambari 13 cha
mkataba
huo, kinaelezea kuwekwa mikakati madhubuti
ya kuwawezesha wanawake, kimafunzo na kuwashajiisha katika nyanja mbalimbali.
Kimataifa, ni asilimia
26.7 tu wanawake kote ulimwenguni ambao ni wabunge, huku asilimia 35.5 wakiwa
katika nafasi za serikalini.
Huku asilimia
28.2 tu ya wanawake wanaoshika nafasi za kiutawala mahali pa kazi.
Emma Rubagumya Mbunge
na mwanakamati wa Kamati ya masuala ya jinsia katika Bunge la Rwanda, anayewakilisha nchi
yake katika Mkutano wa 63 wa Kamisheni ya hali ya wanawake CSW, katika Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, anasema ushiriki wa wanawake katika
maamuzi ya ngazi zote imewaweka mahali pazuri.
Bi Emma Rubagumya
akizungumza nje ya mkutano huo anasema, wanawake wanapokuwa wengi katika ngazi
za maamuzi, inakuwa rahisi kujua matatizo hasa
yanayowakabili wanawake.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi sasa nchi za Rwanda, Cuba na Bolivia, zinaongoza kwa kuwa na wawakilishi wanawake zikiwa na zaidi ya asilimia 50.
Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na watoto Zanzibar ya mwaka 2024/2025 imebainisha kuwa, tafiti zinaonesha kuwa, nchi zinazozingatia usawa wa kijinsia, zimeweza kuimarika kiuchumi kwa kasi kuliko nchi ambazo hazizingati.
MWISHO


Comments
Post a Comment