ZRA yafanya mabadiliko Sheria za Kodi
NA ZUHURA JUMA, PEMBA
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikifanya mabadiliko ya Sheria za kodi, ili kuleta unafuu kwa walipakodi sambamba na kupatikana kodi vizuri.
Akizungumzia Sheria zilizofanyiwa maboresho, Ofisa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Walipa Kodi, kutoka Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Makame Khamis Mohamed alisema, kabla ya kurekebishwa Sheria, Serikali hufanya utafiti kwanza ili zisimuathiri mlipakodi wala Serikali.
Alisema kuwa, hatua hiyo ya kuzifanyia maboresho Sheria za kodi ni katika kuwajali wananchi wake, kwani kuna baadhi ya vitu vimeondolewa ushuru na vyengine vimepunguzwa kwa asilimia 25, jambo ambalo litasaidia sana katika kuboresha utekelezaji wao wa majukumu, pamoja na kuleta unafuu kwa walipakodi.
“Mabadiliko haya yamekuja kuleta unafuu kwa walipakodi na wananchi kwa ujumla, hivyo kama waandishi wa habari tunapaswa kuuhabarisha umma, ili waelewe maboresho haya na kuyafanyia kazi,” alisema Makame.
Alieleza kuwa, lengo la kufanyia maboresho Sheria hizo ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato, na kuhakikisha kodi hizo hazimkwazi mlipakodi, na ndio maana kabla ya maboresho hayo Serikali hufanya Tathmini.
Ofisa huyo alitaja Sheria zilizofanyiwa maboresho kuwa ni, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la thamani nambari 4 ya mwaka 1998 kifungu cha 16 (a), Sheria ya Fedha ya mwaka 2015 (kodi ya Miundombinu) kifungu 20 (3), kipendele cha 2, 3 na 4.
Sheria nyengine ni ya Ushuru wa Stempu nambari 7 ya mwaka 2017 kifungu 65 (2) na kifungu 77 (3), Sheria ya ada za Bandari nambari 2 ya 1999, jedweli la pili (kipengele 1(a) na (c) na Sheria ya Ushuru wa bidhaa nambari 8 ya 2017 kifungu 18 kipya.
“Pia kuna Sheria ya Hoteli nambari 1 ya mwaka 1995 kifungu cha 3 (3) na Sheria ya Usimamizi wa kodi nambari 7 ya mwaka 2009,” alifafanua Ofisa huyo.
Kwa upande wake Mwanasheria Muandamizi kutoka ZRA, Maryam Ishau Abdalla aliwataka waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi, ili wapate uelewa katika masuala ya kodi.
Alisema kuwa, hata wafanyabiasha wakubwa wa mtandaoni sasa wanatakiwa kulipa kodi, ambapo mwezi Julai mwaka jana walifanya mazungumzo ambayo yatasaidia walipe kodi kupitia mtandao.
Nao waandishi waliohudhuria mkutano huo waliahidi kuielimisha jamii juu masuala hayo ya kodi, kwani kuna baadhi ya wafanyabiashara hudhani kwamba, wanakatwa kodi mara mbili, jambo ambalo sio sahihi.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya waandishi wa habari, Mkurugenzi Uratibu Shirika la Magazeti Pemba Haji Nassor Mohamed, aliahidi kuandika habari mbalimbali kwa ufanisi mkubwa, kwani maboresho hayo ni utekelezaji wa maagizo ya Dk. Mwinyi kwa ZRA.
Comments
Post a Comment