NA FATMA HAMAD,
PEMBA
Wizara ya Ardhi na
Maendeleo ya Makaazi Zanziba imesema, imo kwenye mchakato wa kuandaa Sheria ya Biashara ya Majengo na
Ardhi kwa lengo la kuimarisha sekta ya uwekezaji wa majengo pamoja na usimamizi
bora wa ardhi visiwani Zanzibar.
Hayo yameelezwa na Afisa Mdhamini wizara ya Ardhi na Maendeleo
ya Makaazi Bakar Ali Bakar katika kikao cha uwasilishaji wa ripoti ya uandaaji
wa sheria ya sekta miliki Zanzibar
kilichofanyika ukumbi wa Wizara ya Fedha Gombani kisiwani Pemba.
Afisa huyo alisema kwamba Hatua hiyo inalenga kuweka mfumo rasmi
wa kusimamia biashara ya nyumba, viwanja, upangishaji wa nyumba pamoja na mauzo
ya mali zisizohamishika, ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa uwazi na
kwa kufuata sheria.
‘’Tunandaa sharia ya biashara ya Majengo na Ardhi ili kuepo na
usimamizi mzuri wakati watu wanapouziana Ardhi ama kukodishana Majengo, ambapo
kutaimarisha sekta ya uwekezaji Nchini,’’alisema.
Kwa upande wake Muezeshaji wa kikao hicho Ali Ali Hassan alisema
sheria hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi pamoja na kuongeza uwazi
katika shughuli za ununuzi, uuzaji na ukodishaji wa majengo na viwanja.
‘’Naamini kuwepo kwa Sheria hiyo itapunguza madalali matapeli
ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa kuzuka kwa migogoro ya ardhi katika jamii zetu,’’alisema.
Alisema kumekuepo na madalali wengi wanaofanya shughuli za
udalali bila ya kua na elimu ya kazi hiyo na bila ya utambulisho wowote, hivyo
serikali imeamua kuweka sheria hiyo ambayo itakua ni chachu ya kupunguza
mifarakano isiyoyalazima.
Nao washiriki wa kikao hicho walisema kuwa kuwepo kwa sheria
hiyo kutasaidia kulinda haki za wanunuzi, wauzaji pamoja na mawakala wa
majengo, sambamba na kuimarisha mazingira salama ya uwekezaji Zanzibar.
Uandaaji wa Sheria ya Biashara ya Majengo na Ardhi Zanzibar
unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya uwekezaji, kuongeza
mapato ya serikali, pamoja na kuleta maendeleo endelevu katika matumizi bora ya
ardhi na majengo.
MWISHO
Comments
Post a Comment