Wanawake wanaolima kilimo msitu Mchanga mdogo walia kukosa ardhi
NA FATMA HAMAD, PEMBA
WANAWAKE
ambao ni wakulima wa kilimo msitu, shehia ya Mchanga mdogo wilaya ya Wete
Pemba, wamesema wanakabiliwa na changamoto ya umiliki wa ardhi, jambo linalowalazimu
kuzitumia za wenzao wao.
Walisema hawana mashamba yao, na badalayake hulima katika
ardhi za waume zao, jambo linalowapa hofu juu ya kuendeleza kilimo chao hicho ama kinyume
chake.
Wakizungumza na mwandishi wa habazri hizi kwa nyakati tofauti
juu ya maendeleo ya kilimo chao, walisema hilo haliwapi uhakika wa kilimo hicho,
kutokana na hofu ya kibinaadamu.
Walisema licha ya
matamko mbalimbali za kisheria na kidini, kuelezea haki zao juu ya umiliki wa
ardhi, lakini bado jamii hawajalipa kipaumbele na kuendelea kutumia ardhi za watu
wingine.
Mmoja kati ya wakulima hao,
Fatma Hamad Bakar, alisema kwa mwaka wa pili sasa, anaendeshe kilimo
hicho, katika shamba la aliyekuwa muume wake, ambae hadi sasa hawajarithi.
Nae Zaituni Khamis, alisema kwa hakika ndoto za maisha yao
kwenye kilimo msitu, huwa hazifikiwi kutokana na kutokuwa na ardhi ya uhakika.
Alifafanua kuwa, umaskini wa kipato ni moja ya jambo
linalochochea kukosa aradhi, na kuwaacha kwenye njia ya panda ya ndoto zao za kufanikiwa
kimaisha.
‘’Lakini jingine ambalo linatukosesha ardhi, ni baadhi ya
wanaume kuendelea kuzikalia mali za urithi, na kuwa wazito kutekeleza sheria hiyo,’’alifafanua.
kwa upande wake Asha Khamis mkaazi wa Gombeume Mchanga mdogo,
alisema yeye alifanikiwa kununua ardhi miaka mitatu iliyopita, baada ya kujichanga
kidogo kidogo.
Alisema, ijapokuwa lipo shamba la familia na anaweza kuendesha
kilimo msitu, lakini aliona njia ya kufikia ndoto zake ni kujipanga na kununua
ardhi yake.
‘’Kwa sasa naendesha kilimo cha msitu chenye miti mchanganyiko
kama mparachichi, michungwa, migomba pamoja na minanasi, nikiwa kwenye shamba
langu bila ya hofu,’’alisema.
Mpema mtetezi wa masuala ya wanawake kutoka Jumuia ya
Uhifadhi wa misitu kisiwani Pemba ‘CFP’ Sada Juma Segenya , alisema bado umiliki wa ardhi kwa wanawake ni tatizo
ndani ya jamii.
Alieleza moja ya changamoto inayowakabili katika mradi wao
wa uhifadhi mazingira, ni baadhi ya wanawake kutomiliki ardhi, kwa ajili ya kuendeshea
shughuli hizo za uhifadhi na kuongeza kipato.
‘’Mradi wetu wa uhifadhi wa mazingira, ambao tunautekeleza
katika shehia za Chwale, Mchanga mdogo, Kambini na Mjini kiuyu, changamoto
kubwa ni baadhi ya wanawake kukosa ardhi, na badalayake hutumia za waume
zao,’’alisema.
Mkuu wa kitengo cha
mawasiliano kutoka Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania -TAMWA
Zanzibar, Sofia Ngalapi, alisema kufuatia changamoto ya mabadiliko ya
tabianchi, wameamua kuleta mradi wa kuwawezesha wanawake, kutunza mazingira na
kuingiza kipato.
Alieleza kua mradi huo ni ushirikiano wao na Jumuia ya
Uhifadhi wa Misitu Pemba ‘CFP’ na Jumuia ya uhifadhi wa Misitu ‘CFI’ kutoka
Canada, ukiwa na lengo la kuwainua kiuchumi na kuepukana na athari za
mabadiliko ya tabianchi.
‘’Bado wanawake wanaachwa nyuma juu ya kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi, kwani hawana maeneo ya kuhifadhia, na kuepukana na
athari hizo,’’alifafanua.
Naibu Mrajisi kutoka
Kamisheni ya ardhi Pemba Asha Suleiman
Said alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi namba 12 ya mwaka 1992, inaeleza
kuwa ardhi ya Zanzibar ni mali ya umma, hivyo kila mwananchi anahaki ya kutumia
ardhi.
Alisema katika Kifungu cha 7 cha sheria hiyo, kinaeleza wazi,
kwamba haki ya kutumia ardhi ya Zanziba ni kwa wazanzibari wote.
Akitaja moja ya njia ambayo mtu anaweza kupata ardhi ni
kurithi, kununua, kupewa kama zawadi na kuiomba serikalini.
Amirati kutoka Jumuia ya wanawae wa kiislamu Pemba (JUMA WA
KIPE), Asya Amour Abrahman alisema, uislamu umemnyanyua
mwanamke, na anayo haki ya kumiliki ardhi.
‘’Mwanamke ana haki ya kumiliki
ardhi na akaweza kuitumia kwa shughuli za kilimo, maana sio kosa kuwa na uwezo
na kipato,’’alifafanua.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki
lililopo Mkungu Malofa Chake chake, Robert Miguwa Ndalami, alisema mwanamke
anahaki ya kumiliki ardhi, kama mwanamme.
Comments
Post a Comment