SARATANI YA SHINGO YA KIZAZAI ADUI MWINGINE MPYA KWA WANAWAKE, HUATHIRI MFUMO WA UZAZI

 


Kumbe kukosa mtoto, na magonjwa nyemelezi ni sehemu yake

              NA FATMA HAMAD, PEMBA

SARATANI ya shingo ya kizazi ni ile ambayo, hutokana na mabadiliko ya mfumo wa chembe chembe au seli zilizomo katika shingo ya kizazi na wingine wakiita mlango wa kizazi.

Saratani hii huathiri shingo ya kizazi, ambayo ni sehemu ya chini ya mfuko wa kizazi, ambapo kwa kawaida huonekana pale tu mwanamke, anapolala chali na inaweza kuonekana kupitia uke wake.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni ‘WHO’ inathibitisha kuwa, saratani hii, ni ya nne kwa kuathiri wanawake, ikiwa na wagonjwa wapya 604,000 mnamo mwaka 2020.

 

Takriban asilimia 90 ya vifo 342,000 vilivyosababishwa na saratani ya shingo ya kizazi, vilitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

 

Viwango vya juu zaidi vya saratani hiyo na vifo ni kutoka Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara, Amerika ya Kati na kusini Mashariki mwa Asia.

 

Takwimu za WHO, zinaonesha kuwa kila mwaka Tanzania ina wagonjwa wapya wa saratani 42,000 ambapo wagonjwa hao wapya wanaofika kwenye vituo vya afya, ni takribani 15,900 tu. 

 

Ripoti za utafiti wa kisayansi zimeafiki kuwa saratani za shingo ya kizazi, hutokana na maambukizi ya virusi vya 'Human Papillomavirus' au ‘HPV’ vilivyoko katika jamii ya papiloma.

 

 VIRUSI VYA PAPILOMA

 

Virusi aina ya Human Papiloma (HPV) ni maambukizi ya kawaida ya zinaa, ambayo yanaweza kuathiri ngozi, sehemu za siri na koo, takriban watu wote wanaofanya ngono wataambukizwa wakati fulani wa maisha yao, kwa kawaida bila dalili.

 

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na mkufunzi wa kitaifa wa saratani ya shingo ya kizazi, Amina Jumanne Yusuph, anasema, virusi hivi huambukizwa kwa njia ya kujamiiana.

 

Akaeleza kuwa, kwa hivyo hawa vigumu mno kujua uliyejamiiana naye ana maambukizi au hana, ingawa suluhu ya hilo na kuchunguuza afya kila wakati.

 

“Mtu yeyote ambaye amewahi kujamiiana, karibu asilimia 80 ya watu wote, wamewahi kuambukizwa mara moja au mara mbili, kwasababu kinaambukizwa kutoka kwa mtu mwenye maambukizi kwenda kwa mtu asiye na maambukizi”, anasema.

 

Kwamba mwanaume anaweza akakichukua kirusi hicho kutoka kwa mwanamke mwenye nacho, ingawa mwanaume hawezi kuugua saratani kwasababu wao hawana mlango wa kizazi.

 

“Mwanaume anaweza kuwa amejamiiana na wanawake wengi, miongoni mwao, mwanamke mmoja akiwa na kirusi kuna uwezekano wa kuwaambukiza wingine, ingawa siyo lazima wote waugue,’’anafafanua.

 

 

Hayo, aliyatanabahisha, wakati wa mazungumzo na UN News yaliyofanyika katika hospital ya Kanda ya Bugando, mkoani Mwanza kaskazini magharibi mwa Tanzania.

 

DALILI ZAKE NI ZIPI? 

Sababu za hatari zinazoweza kusababisha saratani ni pamoja na kiwango cha aina ya ‘HPV’ iitwayo ‘oncogenicity’ ya hali ya kinga mwilini, uwepo wa magonjwa mengine ya zinaa, idadi ya kuzaa watoto, ujauzito wa kwanza katika umri mdogo.

 

Anafafanua kuwa, sababu kubwa ni kirusi aina ya ‘HPV’ ambacho iwapo ukiambukizwa na kukaa mwilini kwa muda mrefu, kinaweza kuleta shida ya saratani, ambapo huanza kuonesha dalili kwa muda wa miaka 10 hadi 20. 

 

Inachukua muda mrefu mfano, binti akianza kujamiiana akiwa na umri wa miaka 15, maana yake mpaka kuanza kutengeneza mabadiliko ya awali.

 

Hii ni kwenye mlango wake itachukua miaka 10 hadi 20, kwa hiyo binti huyu ataanza kuonesha mabadiliko ya awali akiwa na miaka 30.

 

WALIOKO WENYE HATARI 

Kwa mujibu wa Dk. Amina ni watu wanaoishi na maambukizi ya VVU, wanawake waliobeba mimba na kuzaa watoto wengi kuanzia watano, wanawake wenye mahusiano na zaidi ya mtu mmoja, anakuwa katika hatari ya kupata maradhi.

 

“Mabinti wanaoanza kujamiiana mapema, inawaweka katika hatari kwasababu wanakuwa na muda mrefu wa kujamiiana, lakini pia hata wale wanaoishi na maambukizi ya magonjwa ya zinaa, nao ni hatari kubwa ya kupata ugonjwa huu,”anafafanua. 

 

SHUHUDA

 

‘’Nilipata tatizo la saratani ya mlango wa kizazi mwaka 2013, nilikua natoka maji kama mfano wa chai ya rangi, na nikifanya  tendo landoa na mwenza wangu ilikua,’’anahadithia.

 

 ‘’Napata maumivu makali, nikakaa hali ikaendelea kuwa mbaya nikaenda Hospitali ya Chake chake wakanipima ule uchafu ila wakaniambia hawajajua ni kitu gani,’’anasema Sikuzani Omar ambae sio jina lake halisi.

 

Aliamua kurudi tena hospitalini, ingawa mara hiyo sasa alitakiwa kwenda hospital ya Oceacn road Tanzani bara, na kutii agizo hilo, na kisha alikakatwa kinyama kwa uchunguuzi.

 

‘’Hapo nikambiwa nirudi nyumbani hadi miezi miwili baadae, na ilipofika nilirudi na kuanza matibabu ya miozi,’’anasimulia Sikuzani.

 

‘’Tokea mwaka huo nilikua narudi Hospitali kila baada ya miezi mitatu, na nimekua nikiendelea na dawa hadi sasa nipo vizuri, naishi na familia yangu pamoja na mume wangu na nafanya kila ninachojiskia,’’anasema.

 

Mgonjwa mwingine ambae pia hakutaka kufahamika jina lake ni kutoka Kaskazini Pemba, alijikuta akitokwa na damu saa 24, kwa muda wa miezi sita bila ya kujua sababu.

 

Ingawa baadae anasema, alikimbilia hospital ya Bugando Mwanza kwa matibabu, na sasa anasema yuko vyema baada ya kuelezwa kuwa ilikuwa ni dalili ya saratani.

 

WATAALAMU WA AFYA

 

Daktari bobezi wa saratani ya mlango wa kizazi kutoka Hospitali ya Lumumba Zanzibar, Hellen Robart Makwani anasema, ugonjwa huo unaathiri kizazi, kwani mwanamke anaweza asibebe ujauzito kabisa.

 

Hata akibeba, inaweza kutoka, kutokana na mlango wake wa kizazi, kuwa hauko salama na uimara kama ya wingine.

 

‘’Mama anapopata saratani ya kizazi, hawezi kubabe mimba na ikitokea amebeba, basi hawezi kujifungua ni lazima afanyiwe upasuaji,’’anaeleza.




 

Mapema dokta Rahila Salum Omar wa Chake chake, anaeshughulikia huduma za watu wanaishi na VVU, anasema saratani ya shingo ya kizazi, yaweza kutibika iwapo itagundulika mapema.

 

Anasema, Pap Test, Pap-smear ni kipimo, ambacho hutumika kuchunguza mabadiliko ya chembe, zilizoko katika mlango wa kizazi wa mwanamke.

 

Lengo ni kugundua mabadiliko yanayotokea katika chembe hizo, na hivyo kuwahi kuyakabili mapema, iwezekanavyo. 

 

‘’Kuna chanjo, kinga pekee kabla haujaanza kujamiiana apewe, tunawataka watu waelewe chanjo, kwa hivyo mpeleke binti akapate chanjo,”anasisitiza.

 

WHO, lilitangaza kuwa kila mwezi Januari ni mwezi wa kuhamasisha jamii kuhusu satarani ya shingo ya kizazi.

  

Wataalam wa afya, katika mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania, wamekuwa wakitoa elimu ya ugonjwa huo, katika jamii na kuhamasisha wanawake kujitokeza katika vituo vya afya vinavyotoa huduma hiyo.

 

Ili kupima afya zao kujua iwapo wana mabadiliko ya awali, au kudhaniwa kuwa na saratani ya mlango wa kizazi.

 

Mkakati wa WHO, ni kupunguza idadi ya wagonjwa wapya kila mwaka hadi wanne au pungufu zaidi, kwa kila wanawake 100,000 na kuweka malengo matatu yatakayofikiwa ifikapo mwaka 2030.

 

            


 

 

 

 

 


Comments

Popular posts from this blog

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO

‘’KATIBU MKUU ELIMU ‘’TOENI ELIMU YA MALEZI BORA’’