Wananchi wa Njuguni wampa tano sheha wao

 


NA FATMA HAMAD, PEMBA

WANANCHI wa shehia ya Wingwi Njuguni Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wamesema, kuwepo kwa sheha mwanamke katika shehia yao kumewasaidia kupata mambo mbali mbali ya kimaendeleo, ikiwemo huduma za maji safi na salama.

 Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini kwao Njuguni wamesema, kupata sheha mwanamke katika shehia yao wameimarika kiuchumi na kimaendeleo, kwani wamepata huduma ambazo ilikua ni kilio cha muda mrefu.

Wamesema wakati wa uongozi wa sheha aliepita, vijiji vingi vilikua havina huduma ya maji safi kama vile Pwana, Mtemani, lakini ndani ya mwaka mmoja baada ya kukaa sheha mwanamke, vijiji vingi ambavyo vilikua havina maji vimefikishwa huduma hiyo.

‘’Kwa kweli sheha wetu huyu tunajivunia sana, maana amekuwa mtetezi wa hali ya juu ya mambo mbali mbali ambayo yamekuwa yakitukwaza,’’wameeleza.

Aidha, wamesema kwamba pia katika shehia yao kumeanzishwa timu malumu ya mpira wa miguu, ikiwa na lengo la kuinua vipaji vya vijana katikamichezo, ili kujiepusha na vitendo viovu, ikiwemo udhalilishaji, wizi na uvutaji wa sigara na dawa za kulevya.

Kwa upande wake mwananchi Abdulkadir Amour Rubea (Kidundo) amesema, ipo haja kwa jamii kubadilika na kuondokana na dhana potofu juu ya uongozi kwa mwanamke, kwani siku zote yeye ndie anaejua shida za wanawake wenzake na hata kwa jamii kiujumla.

‘’Mwanamke ni mama na siku zote mama anakua na huruma zaidi kwa watoto wake, hivyo tuwapeni nafasi ili waweze kutuletea mabadiliko vijijini kwetu,’’ameeleza.

Nae sheha huyo, Hadia Omar Dadi amesema, amekua akichukua jitahada mbali mbali ili kuona wananchi wake wanapata mabadiliko baada ya kuondokana na changamoto zinazowakabili.

Sambamba na hilo amewataka wananchi wa kuendelea kumpa mashirikiano, ili aendelea kuwatumikia zaidi kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla.


Comments

Popular posts from this blog

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO

‘’KATIBU MKUU ELIMU ‘’TOENI ELIMU YA MALEZI BORA’’