Gharama za Chaguzi bado kikwazo kwa wanawake wanaotaka kugombea
NA FATMA HAMAD,PEMBA
Wanawake Kisiwani Pemba ambao wanania ya kugombea wameitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar pamoja naya Mungano kuhakikisha wanapunguza vikwazo ikiwemo gharama za uchaguzi, ili kuona nawao wanaingia kwa wingi majimboni na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baaadhi ya wanawake ambao waligombea Uchaguzi uliopita wa 2020,walisema ili kuona wanawake wanajitokeza kwa wingi kuchukua fomu za uongozi ni vyema kupunguza vikwazo ambavyo vinawafanya washindwe kugombea.
Tumu Mwalimu mkaazi wa Wingwi ambae aligombea Ubunge jimbo la Wingwi kupitia Chama cha Mapinduzi CCM alisema bado suala la uchukuaji wa fomu za kugombea ni gharama kubwa, hali inayopelekea wanawake wasio na uwezo kushindwa kujitokeza majimboni, jambo linalopelekea wenye pesa zao kuyahodhi majimbo.
Amesema Kwa mujibu wa utaratibu ulivyo, anaetaka kugombea uwakilishi anatakiwa alipie chamani shilingi laki 100,000 kwa kuchukua fomu.
Pia ameeleza kua anatakiwa kulipa Tume ya uchaguzi shilingi laki 200,000, wakati huo huo ukitakiwa kuchukua fomu ya pingamizi ambayo ni shilingi 300,000.
Amesema Licha ya gharama hizo za kununua fomu ya uwakilishi ili uweze kugombea na kutambulika kuna mambo ya lazima mgombea anatakiwa ayafanye ambayo yanawakwaza.
Amesema kua miongoni mwa mambo hayo ni kuprinti picha kwa ajili ya kupachika kwenye kuta katika jimbo lako, kuwalipa viongozi siku ambayo wanakwenda kupiga kampeni ya nyumba kwa nyumba.
Ziada Khalfan Saleh miaka (48) mkaazi wa Machomane Wilaya ya Chake Chake yeye ameshagombea ubunge Jimbo la Ziwani zaidi ya mara tatu kupitia Chama Cha Tanzania Labour Party (TLP) amesema amekua akishindwa kufanya mikutano kutokana na ukosefu wa fedha.
‘’Ninachokifanya mimi ni kupiga hodi nyumba baada ya nyumba na kuomba kura, kweli kwa hali hii nitalipataje Jimbo wakati nyumba siwezi kuzimaliza na sina uwezo wa kufanya mikutano ya kampeni,’’ ameeleza.
Amesema, ni wakati sasa Serikali kutoa ruzuku kwa vyama vyote na sio tu kwa vyama vikubwa, ili ziwawezeshe wanawake kwenye kampeni ambapo itakuwa ni sababu ya wao kufanikiwa kuwa viongozi.
Juma Kombo Hamad mwanachama wa Chama cha Alliance for Change and Transpareny (ACT WAZALENDO) mkaazi wa Wingwi Micheweni, amesema suala la uchaguzi linahitaji gharama, kwani wanawake wengi wanaogombea hawana ajira rasmi.
‘’Kama Serikali hawajalikalia kitako, hio 50 kwa 50 ya usawa wa kijinsia kwenye ngazi ya mamuzi haitofikiwa,’’anasema.
Mapema Abass Mohamed Khatib Mratibu wa Chama cha Demokrasia Makini (DP) kisiwani Pemba ameeleza kuwa, mara nyingi chama chao kimekua kikiwasaidia wagombea wanawake gharama za uchukuaji wa fomu tu na sio kwenye kampeni.
‘’Hatuna ruzuku yoyote tunayoipata kutoka Serikalini, hivyo hatuna msaada wowote wa kuwasaidia ili waweze kujigharamia kwenye kampeni wakati wa uchaguzi,” amekiri Abass.
Mohamed Haji Kombo ambae ni Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Chake Chake amesema, umasikini ni kilio kikubwa kinachowakosesha nafasi wanawake waliopo kwenye siasa kupata nafasi za uongozi.
‘’Tume ya Uchaguzi Zanzibar ni chombo kinachoendeshwa na Serikali, kwanini kishindwe kuwasaidia wanawake na kuonekana wameingia kwa wingi kwenye nafasi za Uongozi,’’ ameuliza.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Mahusiano kutoka chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Zanzibar Sophia Ngalapi amesemakuwa , wamekua wakitoa elimu kwa wanawake ili waweze kuingia majimboni kugombea.
‘’Ndoto zetu ni kuona wanawake wanaingia kwa wingi kwenye vyombo vya maamuzi, lakini gharama za uchaguzi bado zimekua zikiwakosesha kufikia malengo yao,’’amesema.
Nae Abdul-Razak Said Ali ambae ni Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Zanzibar amekiri kuwepo kwa gharama katika chaguzi na kusema, kwasasa baadhi ya kanuni zinazoonekana kuwa zina ukakasi tayari zipo katika mchakato wa kufanyiwa marekebisho.
‘’Sasa hivi kanuni zipo katika hatua za mwisho za kufanyiwa marekebisho, hivyo tusubirie mabadiliko vipi Sheria itatoa kipaombele katika suala la gharama kwa wanawake,’’amefahamisha.
.jpg)
Comments
Post a Comment