MIDIPAO YAIKUMBUSHA JAMII
NA FATMA HAMAD, PEMBA
Jamii imetakiwa kurejesha malezi ya pamoja katika kuwalea watoto wao jambo ambalo litasaidia kuwakinga na vitendo viovu ikiwemo udhalilihaji.
Ushauri huo umetolewa na Msaidizi wa sheria wilaya ya Micheweni (MIDIPAO) Ali Khatib Hassan wakati akizungumza na wananchi wa Chamboni Micheweni kisiwani Pemba.
Alisema licha ya mikakati mbali mbali inayofanywa ili kuondosha udhalilishaji, lakini bado suala hilo linaendelea kuwatesa watoto,hivyo ni vyema wazazi kushikamana katika malezi na kila mmoja kuumwa na mtoto wa mwenzake ili kuwalinda na vitendo hivyo.
‘’Kila mzazi na mtoto wake, hata ukimuona wa mwenzako anafanywa kitu gani unanyamaza kwa vile si wa kwako, hivyo tabia hiyo si nzuri na ndo inayosababisha kuengezeka kwa udhalilishaji mitaani mwetu,’’alisema.
Aidha kwa upande mwengine aliwataka wananchi hao kutoa tarifa kwa vyombo husika wakati wanapoona viashiria vya udhalilishaji ili viweze kukemewa na kuchukuliwa hatua mapema.
‘’Niwaombe wananchi wenzangu tuchukue tahadhari mapema wakati tukiona tu kuna jambo ambalo litapelekea kufanyika kwa udhalilishaji, nasio kusubiri mpaka pakatokea uharibifu’alieleza’’.
Kwa upande wake Said Salim Khamis Msaidizi wa sheria shehiaya Msuka aliwataka wazazi na walezi kufuatilia nyenendo za watoto wao wanapokwenda kutafuta elimu ili kuepusha kufanyiwa matendo machafu.
‘’Jamani watoto hatuwasimamii tunawacha tu kama wa wanyama, ukisha kumpeleka Skuli au Madrsa tunahisi ndo kazi imekwisha hujui jee anakwenda au anaishia njiani, alisema’’.
Alisema mporomoko wa madili umepungua kwa kiasi kikubwa katika jamii, hivyo ni jukumu la Wazazi kuwasimamia watoto kwa hali ya juu ili kuweze kupatikana kwa kizazi bora ambacho kitaleta maendeleo kwa familia zao na Taifa kiujumla.



Comments
Post a Comment