WANAWAKE WENYEULEMAVU WASHIKA MKIA KWENYE KAMATI ZA SHEHIA
NA FATMA HAMAD, PEMBA
WATU WENYE ulemavu, wana
haki ya kushirikishwa katika nyanja zote za kiuchumi, kama raia wote, bila ya
kujali ulemavu wao, maana kinachoangaliwa sio ulemavu bali ni haki zao na uwezo
wao.
Na ndio maana, serikali, ikaweka
muongozo maalumu, ili maendeleo ya nchi yasiwaache nyuma kwa kuimarisha muundo
wa tasisi za watu wenye ulemavu.
Tanzania imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa
wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), wa mwaka 2006 unahimiza serikali,
kuhakikisha ushiriki sawa wa watu wenye ulemavu katika siasa na maamuzi.
Hata Katiba ya Zanzibar ya 1984, ambayo ndo
sheria mama, kupitia kifungu chake cha 21(1) nacho kinatambua haki ya kila raia
kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi bila ubaguzi.
Sheria ya watu wenye ulemavu namba 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 29
kinaeleza, umuhimu wa watu wenye ulemavu kufikia miundombinu pamoja na taarifa,
mawasiliano na haki zote za kibinadamu.
Tathmini ya Utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya wanawake na Jinsia
Zanzibar mwaka 2000, imebainisha upungufu na changamoto zilizoathiri
utekelezaji wa Sera hiyo ikiwa ni pamoja na kutofikiwa kwa usawa wa kijinsia.
Hali hii imethibitishwa na
vipimo vya usawa wa kijinsia (Gender Inequality Index – GII na Social
Institutions and Gender Index – SIGI, 2022) ambapo Tanzania, imepata alama
0.539 kwa ‘GII’ na 0.262 kwenye ‘SIGI’, ikiwa ni viwango vya chini vya kufikia
usawa wa kijinsia.
Nchini China, takwimu zinaonyesha kwamba kipato cha wanawake wenye
ulemavu ni sawa na asilimia 42.5 ya kipato cha wastani kwa mtu bila ulemavu.
Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia
Wazee na watoto Zanzibar ya mwaka 2024/2025 imebainisha kuwa, tafiti zinaonesha
kuwa, nchi zinazozingatia usawa wa kijinsia, zimeweza kuimarika kiuchumi kwa
kasi kuliko nchi ambazo hazizingatii usawa huo.
Licha ya kuwepo kwa miongozo hiyo
bado ushiriki wa wanawake wenye ulemavi ni mdogo, katika ngazi za maamuzi,
kuanzia ngazi ya familia, shehia na hata
Taifa.
Makala hii inatuonesha kwamba ni
kwa kiasi gani wanawake wenye ulemavu wameshirikishwa katika kamati za masheha
za shehia.
JEE HALI HALISI IKOJE KWENYE KAMATI ZA SHEHIA ZA MICHEWENI
Mkoa wa Kaskazini Pemba unaoundwa na wilaya mbili
za Wete na Micheweni, ambapo Micheweni
pekee inazo shehia 25 zenye wajumbe wa kamati 260.
Kati ya wajumbe hao wa kamati 260 wanaume ni 150
wanawake wenye ulemavu ni watatu tu (3), kati ya wajumbe wanawake 110 sawa na
asilimia 2.7 ya wanawake hao.
Sheha wa Tumbe Magharibi, Masoud Khamis Hamad
anasema kamati yake inao wajumbe 12, ikiwa na idadi sawa ya wanawake na wanaume
‘’Ni kweli ndani ya hawa wajumbe sita wanawake,
hakuna hata mmoja, mwenye ulemavu, na nahisi sio kwamba hawawezi, bali nimekosa
uzingatiaji,’’anakiri.
Hamad anasema hajamshirikisha mwanamke mwenye
ulemavu katika kamati yake, kwani
anahisi hawatoweza kufanya kazi kutokana na hali zao.
Sheha wa Mtemani wingwi Mohamed Ali Kombo anasema
kamati yake inayo wajumbe 10 idadi ya wanaume na wanawake ikiwa sawa, ingawa
anae mmoja mwanamke mwenye ulemavu.
Sheha Mohamed anasema kati ya wajumbe hao wote 10,
huyo mwenye ulemavu ndio ambae akimpa kazi ndie anaeifanyakazi kwa umakini na
kwa wakati.
‘’Mjumbe huyo mwenye ulemavu nimemueka kama
kumjaribu tu, ingawa naona mtndaji mzuri kuliko wajumbe wote, nimevutiwa na
sasa ninampango wa kuongeza mwengine,’’anaeleza.
Sheha wa Chamboni Bikuu Juma Alawi anasema
hajamshirikisha mwanamke mwenyeulemavu katika kamati yake, kwani alikua hana
elimu kwamba wenye ulemavu na wao wana uwezo wa kufanya kazi.
‘’Muwandishi ushaniamsha na sasa nitamtafuta
mwanamke mwenyeulemavu nimueke kwenye kamati yangu nafikiria ataweza,’’anasema.
Sheha wa Shumba vyamboni Time Said Omar anasema anao
wajumbe tisa, kati ya hao anae mmoja mwanamke mwenye ulemavu na tena ameupata
akiwa kashakua mwanakamati.
WANAKAMATI
Fatma Rashid Abdullah mwanakamati shehia ya Sizini
anasema bado wanawake wenyeulemavu, hawajashirikishwa ipasavyo katika kamati
hizo.
‘’Nikweli wanawake wenye ulemavu kwenye kamati zetu
hizi tumewasahau, na nnaimani wakipewa nafasi watafanya vizuri kuliko sisi
tusio na ulemavu,’’anasema.
Maryam Hassan Abdallah (23) mwenye ulemavu wa
viungo ambae ni mwanakamati ya Shehia ya
Mtemani anasema mwanzoni amepatashida, ingawa kwasasa amekua akishirikiana na
wenzake katika utekelezaji wa kazi zao.
‘’Sijatengwa, sijabaguliwa, nafanyakazi sawasawa na
wajumbe wenzangu,’’anasema.
Ali Omar Ali ambae ni mmoja wa wanakamati hiyo ya
Mtemani anasema mjumbe huyo mwenye ulemavu amekua akifanya kazi wakati wowote,
haijalishi kuna malipo ama hakuna.
‘’Kwa kweli mwenzetu huyo ni mchapa kazi, haangalii kama kuna malipo ama kuna
nauli, nnaimani kama baadae huo usheha hatoupewa yeye,’’anafahamisha.
Katibu Tawala wilaya ya Micheweni Sheha Mpemba Faki
anasema kamati zote zimekua zikifanya vizuri, ila kamati ya Sheha wa Mtemani
imekua ikifanya vizuri kulikoa kamati zengine, huyu mjumbe mwanamke mwenye
ulemavu ndie anaechangia hilo.
‘’Tunae
mwanamke mmoja mwenye ulemavu katika Kamati ya shehia ya Mtemani, imekua
ikifanya vizuri, sijawahipo hata siku moja kupewa kesi kwamba wamegombana na
Sheha wao,’alieleza.
Sheria namba 8 ya mwaka 2014 ya Tawala za mikoa
imesema sifa ya wajumbe wa kamati wawe wanajua kusoma na kuandika, huku sheha
awe ametimia miaka 40 na ajue kusoma na kuandika.
JAMII
Rabia Alei Salim (42) mwenye ulemavu wa ngozi
mwananchi kutoka Wesha, anasema sio kamati za Micheweni pekee ambazo inaonekana
wanawake wenye ulemavu ni kidogo, hata za wilaya nyengine, hali inafanana.
Anasema kamati ya Sheha wa Wesha inayowajumbe 10
ingawa hakuna hata mwanamke mmoja mwenye ulemavu wa aina yoyote.
‘’Binafsi
sheha wangu, aliniambia anataka aniweke kwenye kamati, ingawa hakuniweka bado
hawajatuamini, wanahisi sisi hatuwezi,’’anasema.
Maryam Nuhu Hamad Kutoka Ole anasema, ushiriki wa
wanawake wenye ulemavu katika nafasi za uongozi, bado ni mdogo, kuanzia ngazi
za chini, ikiwemo usheha hadi juu.
‘’Sio kwenye kamati tu bali hata ngazi nyengine bado
mambo ndo hayohayo,’’anafahamisha.
SERIKALI
Mwanaisha
Ali Masoud Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto
Pemba anasema usawa wa kijinsia unahitajika kuanzia hata kwenye ngazi ya
familia, ili kujenga miundimbinu rafiki ya ushirikishwaji.
‘’Tunatoa
mafunzo mbalimbali kwa jamii, kuona wanawake wote wanapata uwelewa juu ya
umuhimu wa ushiriki wao katika ngazi
zote za maamuzi,’anaeleza.
Salma Haji Saadat aliekua
Mwenyekiti wa Baraza la watu wenye ulemavu Zanzibar anasema moja ya mkakati wa
serikali ni kuondoa ubaguzi, na kuongeza ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu
katika ngazi za maamuzi kutoka asilimia 2 hadi 5 ikifikapo mwaka 2030.
Mashavu Juma Mabrouk ni Mratibu kutoka Baraza la
watu wenye ulemavu Pemba, anasema bado wanawake wenye ulemavu hawajaonekana katika fursa hasa
kwenye nafasi za maamuzi, ambapo hupelekea sikuzote kubaki mkiani na kuchelewa
kufikiwa na maendeleo.
WANAHARAKATI
Juma Kombo Hija Katibu wa Jumuia ya wanawake wenye
ulemavu (JUWAUZA) upande wa Pemba anasema hata katika ngazi za chini wanawake
wenye ulemavu wamekua wakisahauliwa kwenye teuzi mbalimbali.
‘’Sio kwenye
kamati peke yake hata hao masheha, kwa mfano katika masheha 25 wa wilaya ya
Micheweni, na 36 wa wilaya ya Wete hakuna hata mmoja mwanamke mwenye ulemavu,’’
anasema.
Pia wilaya hiyo hiyo ya Micheweni inayo Madiwani 15
nane wa kuchaguliwa, watano wa kuteuliwa, na wawili viti maalumu, ingawa hakuna
hatammoja mwanamke mwenye ulemavu.
Hata Madiwani wa Wilaya ya Wete wapo 19 ingawa
hakuna hata mmoja mwanamke mwenye ulemavu.
Ikiwa
kwa Zanzibar wapo masheha 388 wanawake
81 wanaume 307 huku madiwani wanawake wakiwa ni 27 kati ya Madiani wote 110.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka TAMWA Zanzibar Sofia Ngalapi anasema idadi ya wanawake wenye
ulemavu ni ndogo katika yanja zote za maamuzi, na hii ni kutokana na mitazamo
kwa baadhi ya watu juu ya watu hao.
‘’Wapo wenye ulemavu katika baadhi ya tasisi na
wamekua wakifanya vizuri zaidi kuliko na
wasio na ulemavu,’’anaeleza.
Anasema kwa mujibu wa ripoti walioifanya
inaoneonesha kwamba idadi ya wanawake Zanzibar katika maamuzi bado ni ndogo,
kwani ni asilimia 38 tu.
Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022
inaendelea kuwabeba wanawake kwani inaonesha wako asilimia 51 ambao ni wengi ukilinganisha na
wanaume
Huku wanawake wenye ulemavu Zanziba wapo
asilimia
11.4 kati ya watu milioni 1.8.
Anaendelea kusema
kutokana na hilo wamekuja na mradi wa Wanawake Viongozi kwa ajili Usawa,
Uwajibikaji na Demokrasia (W-LEAD)
unaolenga kuimarisha nafasi za uongozi na ushiriki wa wanawake, hususani
wanawake vijana na wanawake wenye ulemavu, katika mifumo ya kidemokrasia na
kushika nafasi mbalimbali za maamuzi.
Mradi huo wanautekeleza kwa ushirikiano na Jumuia ya
wasiona (ZANAB), chuo kikuu cha Taifa
cha Zanzibar (SUZA) na Zanzibar
University (ZU).
Ambapo
unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia mpango wa Ushiriki wa wanawake na Vijana
katika Demokrasia na kuanza utakelezwaji
wake mwaka huu 2026 hadi 2027.
ATHARI YAKE
Hafidh Abdi Said Mkurugenzi mtendaji kutoka Pegao,
anasema endapo wanawake wenye ulemavu hawatoshirikishwa kwenye maamuzi,
watakosa mtetezi wa kuwasemea shida zao, na kupelekea siku zote kuishi
kinyonge.
NINI KIFANYIKE
Hidaya Mjaka Ali mwenye ulemavu wa viungo anasema
Ipo haja kwa sasa kuona wanawake wenyeulemavu
wanashirikishwa katika maamuzi, na kutetea kero zao na kupata haki
zao,’’wanasema wanaharakati wa haki za watu wenye ulemavu.
MWISHO.


Comments
Post a Comment