WANAWAKE WENYEULEMAVU WASHIKA MKIA KWENYE KAMATI ZA SHEHIA
NA FATMA
HAMAD, PEMBA
WATU WENYE ulemavu, wana
haki ya kushirikishwa katika nyanja zote za kiuchumi, kama raia wote, bila ya
kujali ulemavu wao, maana kinachoangaliwa sio ulemavu bali ni haki zao na uwezo
wao.
Na ndio maana, serikali, ikaweka muongozo maalumu, ili
maendeleo ya nchi yasiwaache nyuma kwa kuimarisha muundo wa tasisi za watu
wenye ulemavu.
Tanzania imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa
wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), wa mwaka 2006 unahimiza serikali,
kuhakikisha ushiriki sawa wa watu wenye ulemavu katika siasa na maamuzi.
Katiba ya
Zanzibar ya 1984, Kifungu kidogo cha 3 kinaeleza kwamba, kila mzanzibari
anayohaki ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyoko chini ya
mamlaka ya Zanzibar.
Sheria ya
watu wenye ulemavu namba 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 29 kinaeleza, umuhimu wa
watu wenye ulemavu kufikia miundombinu pamoja na taarifa, mawasiliano na haki
zote za kibinadamu.
Tathmini ya
Utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya wanawake na Jinsia Zanzibar mwaka 2000,
imebainisha upungufu na changamoto zilizoathiri utekelezaji wa Sera hiyo ikiwa
ni pamoja na kutofikiwa kwa usawa wa kijinsia.
Hali hii imethibitishwa na vipimo vya usawa wa
kijinsia (Gender Inequality Index – GII na Social Institutions and Gender Index
– SIGI, 2022) ambapo Tanzania, imepata alama 0.539 kwa ‘GII’ na 0.262 kwenye ‘SIGI’,
ikiwa ni viwango vya chini vya kufikia usawa wa kijinsia.
Nchini
China, takwimu zinaonyesha kwamba kipato cha wanawake wenye ulemavu ni sawa na
asilimia 42.5 ya kipato cha wastani kwa mtu bila ulemavu.
Bajeti ya
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na watoto Zanzibar ya mwaka
2024/2025 imebainisha kuwa, tafiti zinaonesha kuwa nchi zinazozingatia usawa wa
kijinsia, zimeweza kuimarika kiuchumi kwa kasi kuliko nchi ambazo hazizingatii
usawa huo.
Licha ya kuepo kwa miongozo hiyo bado ushiriki wa
wanawake wenye ulemavi ni mdogo, katika ngazi za maamuzi, kuanzia ngazi ya
familia, shehia na hata Taifa.
Makala hii inatuonesha kwamba ni kwa kiasi gani
wanawake wenye ulemavu wameshirikishwa katika kamati za masheha za shehia.
JEE HALI
HALISI IKOJE KWENYE KAMATI ZA SHEHIA ZA MICHEWENI
Mkoa
wa Kaskazini Pemba unaoundwa na wilaya mbili za Wete na Micheweni, ambapo Micheweni pekee inazo
shehia 25 zenye wajumbe wa kamati 260.
Kati
ya wajumbe hao wa kamati 260 wanaume ni 150 wanawake wenye ulemavu ni watatu tu
(3), kati ya wajumbe wanawake 110 sawa na asilimia 2.7 ya wanawake hao.
Sheha
wa Tumbe Magharibi, Masoud Khamis Hamad anasema kamati yake inao wajumbe 12, ikiwa
na idadi sawa ya wanawake na wanaume
‘’Ni
kweli ndani ya hawa wajumbe sita wanawake, hakuna hata mmoja, mwenye ulemavu,
na nahisi sio kwamba hawawezi, bali nimekosa uzingatiaji,’’anakiri.
Hamad
anasema hajamshirikisha mwanamke mwenye ulemavu
katika kamati yake, kwani anahisi hawatoweza kufanya kazi kutokana na
hali zao.
Sheha
wa Mtemani wingwi Mohamed Ali Kombo anasema kamati yake inayo wajumbe 10 idadi
ya wanaume na wanawake ikiwa sawa, ingawa anae mmoja mwanamke mwenye ulemavu.
Sheha
Mohamed anasema kati ya wajumbe hao wote 10, huyo mwenye ulemavu ndio ambae akimpa
kazi ndie anaeifanyakazi kwa umakini na kwa wakati.
‘’Mjumbe
huyo mwenye ulemavu nimemueka kama kumjaribu tu, ingawa naona mtndaji mzuri
kuliko wajumbe wote, nimevutiwa na sasa ninampango wa kuongeza
mwengine,’’anaeleza.
Sheha
wa Chamboni Bikuu Juma Alawi anasema hajamshirikisha mwanamke mwenyeulemavu
katika kamati yake, kwani alikua hana elimu kwamba wenye ulemavu na wao wana
uwezo wa kufanya kazi.
‘’Muwandishi
ushaniamsha na sasa nitamtafuta mwanamke mwenyeulemavu nimueke kwenye kamati
yangu nafikiria ataweza,’’anasema.
Sheha
wa Shumba vyamboni Time Said Omar anasema anao wajumbe tisa, kati ya hao anae
mmoja mwanamke mwenye ulemavu na tena ameupata akiwa kashakua mwanakamati.
WANAKAMATI
Fatma
Rashid Abdullah mwanakamati shehia ya Sizini anasema bado wanawake wenyeulemavu,
hawajashirikishwa ipasavyo katika kamati hizo.
‘’Nikweli
wanawake wenye ulemavu kwenye kamati zetu hizi tumewasahau, na nnaimani
wakipewa nafasi watafanya vizuri kuliko sisi tusio na ulemavu,’’anasema.
Maryam
Hassan Abdallah (23) mwenye ulemavu wa viungo
ambae ni mwanakamati ya Shehia ya Mtemani anasema mwanzoni amepatashida,
ingawa kwasasa amekua akishirikiana na wenzake katika utekelezaji wa kazi zao.
‘’Sijatengwa,
sijabaguliwa, nafanyakazi sawasawa na wajumbe wenzangu,’’anasema.
Ali
Omar Ali ambae ni mmoja wa wanakamati hiyo ya Mtemani anasema mjumbe huyo
mwenye ulemavu amekua akifanya kazi wakati wowote, haijalishi kuna malipo ama
hakuna.
‘’Kwa
kweli mwenzetu huyo ni mchapa kazi,
haangalii kama kuna malipo ama kuna nauli, nnaimani kama baadae huo usheha
hatoupewa yeye,’’anafahamisha.
Katibu
Tawala wilaya ya Micheweni Sheha Mpemba Faki anasema kamati zote zimekua
zikifanya vizuri, ila kamati ya Sheha wa Mtemani imekua ikifanya vizuri kulikoa
kamati zengine, huyu mjumbe mwanamke mwenye ulemavu ndie anaechangia hilo.
‘’Tunae mwanamke mmoja mwenye ulemavu katika
Kamati ya shehia ya Mtemani, imekua ikifanya vizuri, sijawahipo hata siku moja
kupewa kesi kwamba wamegombana na Sheha wao,’alieleza.
JAMII
Rabia
Alei Salim (42) mwenye ulemavu wa ngozi mwananchi kutoka Wesha, anasema sio
kamati za Micheweni pekee ambazo inaonekana wanawake wenye ulemavu ni kidogo,
hata za wilaya nyengine, hali inafanana.
Anasema
kamati ya Sheha wa Wesha inayowajumbe 10 ingawa hakuna hata mwanamke mmoja
mwenye ulemavu wa aina yoyote.
‘’Binafsi sheha wangu, aliniambia anataka
aniweke kwenye kamati, ingawa hakuniweka bado hawajatuamini, wanahisi sisi
hatuwezi,’’anasema.
Maryam
Nuhu Hamad Kutoka Ole anasema, ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika nafasi
za uongozi, bado ni mdogo, kuanzia ngazi za chini, ikiwemo usheha hadi juu.
‘’Sio
kwenye kamati tu bali hata ngazi nyengine bado mambo ndo hayohayo,’’anafahamisha,’’.
SERIKALI
Mwanaisha Ali Masoud Mkuu wa
Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto Pemba anasema usawa wa
kijinsia unahitajika kuanzia hata kwenye ngazi ya familia, ili kujenga
miundimbinu rafiki ya ushirikishwaji.
‘’Tunatoa mafunzo mbalimbali kwa
jamii, kuona wanawake wote wanapata uwelewa juu ya umuhimu wa ushiriki wao katika ngazi zote za maamuzi,’anaeleza.
Salma Haji Saadat aliekua
Mwenyekiti wa Baraza la watu wenye ulemavu Zanzibar anasema moja ya mkakati wa
serikali nu kuondoa ubaguzi, na kuongeza ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu
katika ngazi za maamuzi kutoka asilimia 2 hadi 5 ikifikapo mwaka 2030.
Mashavu
Juma Mabrouk ni Mratibu kutoka Baraza la watu wenye ulemavu Pemba, anasema bado
wanawake wenyeulemavu hawajaonekana katika fursa hasa kwenye nafasi za maamuzi,
ambapo hupelekea sikuzote kubaki mkiani na kuchelewa kufikiwa na maendeleo.
WANAHARAKATI
Juma
Kombo Hija Katibu wa Jumuia ya wanawake wenye ulemavu (JUWAUZA) upande wa Pemba
anasema hata katika ngazi za chini wanawake wenye ulemavu wamekua wakisahauliwa
kwenye teuzi mbalimbali.
‘’Sio kwenye kamati peke yake hata hao
masheha, kwa mfano katika masheha 25 wa wilaya ya Micheweni, na 32 wa wilaya ya
Wete hakuna hata mmoja mwanamke mwenye ulemavu,’’ anasema.
Pia
wilaya hiyo hiyo ya Micheweni inayo Madiwani 15 nane wa kuchaguliwa, watano wa
kuteuliwa, na wawili viti maalumu, ingawa hakuna hatammoja mwanamke mwenye
ulemavu.
Hata
Madiwani wa Wilaya ya Wete wapo 19 ingawa hakuna hata mmoja mwanamke mwenye
ulemavu.
Ikiwa kwa Zanzibar wapo masheha 388 wanawake 81 wanaume
307 huku madiwani wanawake wakiwa ni 27 kati ya Madiani wote 110.
Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano kutoka TAMWA Zanzibar
Sofia Ngalapi anasema idadi ya wanawake wenye ulemavu ni ndogo katika
yanja zote za maamuzi, na hii ni kutokana na mitazamo kwa baadhi ya watu juu ya
watu hao.
‘’Wapo
wenye ulemavu katika baadhi ya tasisi na wamekua wakifanya vizuri zaidi kuliko na wasio na ulemavu,’’anaeleza.
Anasema
kwa mujibu wa ripoti walioifanya inaoneonesha kwamba idadi ya wanawake Zanzibar
katika maamuzi bado ni ndogo, kwani ni asilimia 38 tu.
Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 inaendelea kuwabeba wanawake kwani inaonesha
wako asilimia 51 ambao ni wengi
ukilinganisha na wanaume
Huku wanawake wenye ulemavu Zanziba wapo
asilimia 11.4 kati ya watu
milioni 1.8.
Anaendelea
kusema kutokana na hilo wamekuja na
mradi wa Wanawake Viongozi kwa ajili Usawa, Uwajibikaji na Demokrasia (W-LEAD) unaolenga kuimarisha
nafasi za uongozi na ushiriki wa wanawake, hususani wanawake vijana na wanawake
wenye ulemavu, katika mifumo ya kidemokrasia na kushika nafasi mbalimbali za
maamuzi.
Mradi
huo wanautekeleza kwa ushirikiano na Jumuia ya wasiona (ZANAB), chuo kikuu
cha Taifa cha Zanzibar (suza) na Zanzibar University
(ZU) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya kupitia mpango wa Ushiriki wa
wanawake na Vijana katika Demokrasia na
kuanza utakelezwaji wake mwaka
huu 2026 hadi 2027.
ATHARI YAKE
Hafidh
Abdi Said Mkurugenzi mtendaji kutoka Pegao, anasema endapo wanawake wenye
ulemavu hawatoshirikishwa kwenye maamuzi, watakosa mtetezi wa kuwasemea shida
zao, na kupelekea siku zote kuishi kinyonge.
NINI
KIFANYIKE
Hidaya
Mjaka Ali mwenye ulemavu wa viungo anasema Ipo haja kwa sasa kuona wanawake
wenyeulemavu wanashirikishwa katika
maamuzi, na kutetea kero zao na kupata haki zao,’’wanasema wanaharakati wa haki
za watu wenye ulemavu.
MWISHO.

Comments
Post a Comment