ZAMECO YAITAKA SERIKALI KUHARAKISHA MSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI ZANZIBAR
NA FATMA HAMAD, PEMBA
Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) imeiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuharakisha mchakato wa kuuwasilisha Barazani Mswada wa Sheria ya Huduma za Habari Zanzibar ili uweze kujadiliwa na hatimaye kuwa sheria, baada ya kusubiriwa kwa zaidi ya miaka kumi.
Kwa mujibu wa ZAMECO, sekta ya habari Zanzibar bado inasimamiwa na sheria mbalimbali zilizotungwa katika nyakati tofauti, hali inayosababisha kuwepo kwa mfumo wa kisheria usioendana kikamilifu na mahitaji ya sasa ya sekta hiyo pamoja na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Kamati hiyo imeeleza kuwa baadhi ya sheria zilizopo zimezipa mamlaka makubwa taasisi za Serikali katika kusajili na hata kufungia vyombo vya habari, jambo ambalo linaonekana kutokidhi kikamilifu misingi ya demokrasia, uwazi na utawala bora wa sheria.
Ahadi za Muda Mrefu
ZAMECO imekumbusha kuwa taarifa za kukamilika kwa Mswada huo zimekuwa zikitolewa na viongozi mbalimbali wa Serikali kwa nyakati tofauti. Mwaka 2015, aliyekuwa Waziri wa Habari, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alieleza kuwa mchakato wa sheria hiyo ulikuwa unaendelea.
Mwaka 2023, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani, aliyekuwa Waziri wa Habari Bi. Tabia Maulid Mwita alisema kuwa Mswada huo ulikuwa umekamilika kwa asilimia 80.
Hivi karibuni, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Riziki Pembe, alieleza katika kikao chake cha kwanza na wadau wa habari Januari 2026 kuwa anatarajia kuuwasilisha Mswada huo katika Baraza la Wawakilishi ifikapo Septemba mwaka huu.
Wawakilishi Wahoji Ucheleweshaji
Katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Habari kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Wawakilishi kadhaa walitaka Serikali kutoa maelezo ya wazi kuhusu hatma ya sheria hiyo.
Mwakilishi wa Jimbo la Paje, Mhe. Jaku Hashim Ayoub, alieleza kutoridhishwa kwake na ucheleweshaji wa muda mrefu wa Mswada huo huku akisema kuwa wadau wa habari wameendelea kupewa ahadi kwa miaka mingi bila kuona matokeo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Pandani, Profesa Omar Fakih, alisisitiza umuhimu wa Serikali kueleza tarehe mahsusi ya kuwasilishwa kwa sheria hiyo ili wananchi na wadau wa habari waweze kupata uhakika badala ya kuendelea kusubiri ahadi zinazojirudia.
Sheria Itaimarisha Uhuru wa Habari
ZAMECO inaamini kuwa kupitishwa kwa Sheria ya Huduma za Habari kutasaidia kulinda haki za msingi za wananchi za kupata na kutoa taarifa pamoja na kuimarisha uhuru wa kujieleza.
Kamati hiyo imebainisha kuwa sheria hiyo itachangia kuimarisha uwajibikaji, uwazi, utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa pamoja na maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini.
Aidha, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi akiwemo Mhe. Seif Hamad wa Jimbo la Ole na Mhe. Said Ali Mbarouk wa Jimbo la Gando walisisitiza kuwa sheria zilizopo zimepitwa na wakati na zinahitaji kufanyiwa maboresho ya haraka ili kuendana na mazingira ya sasa ya sekta ya habari.
Changamoto za Waandishi wa Habari
Mbali na suala la sheria, ZAMECO imeeleza kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili waandishi wa habari wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo mazingira yasiyoridhisha ya kufanyia kazi hususan kwa waandishi wanaoripoti shughuli za Baraza la Wawakilishi.
Kamati hiyo imeeleza kuwa kuboresha mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari ni hatua muhimu katika kuongeza ubora wa taarifa zinazowafikia wananchi na kuimarisha utendaji wa vyombo vya habari.
Wito kwa Serikali na Waandishi wa Habari
ZAMECO imeendelea kuiomba Serikali kutekeleza ahadi yake ya kuuwasilisha Mswada wa Sheria ya Huduma za Habari Zanzibar ifikapo Septemba 2026 ili kuweka mfumo wa kisheria unaoendana na mabadiliko ya kidijitali na unaolinda uhuru wa habari.
Wakati huo huo, Kamati imewahimiza waandishi wa habari kuendelea kuzingatia maadili ya taaluma yao kwa kuzingatia uadilifu, usahihi, uwajibikaji na maslahi ya umma katika kazi zao za kila siku.
ZAMECO ni muungano wa mashirika na wadau wa sekta ya habari na haki za binadamu Zanzibar, ukiwemo Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), Baraza la Habari Tanzania Zanzibar (MCT-ZNZ) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania Zanzibar (THRDC-ZNZ).
MWISHO

Comments
Post a Comment