TAMWA YAWAFUMBUA MACHO WANAWAKE, WANAWAKE VIJANA NA WANAWAKE WENYE ULEMAVU
NA FATMA HAMAD, PEMBA
CHAMA CHA Wandishi wa Habari Wanawake
Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZANZIBAR ), kimezindua mradi wa Wanawake Viongozi kwa
ajili Usawa, Uwajibikaji na Demokrasia(
W-LEAD) unaolenga kuimarisha nafasi za uongozi na ushiriki wa wanawake, hususan
wanawake vijana na wanawake wenye ulemavu, katika mifumo ya kidemokrasia na
kushika nafasi mbalimbali za maamuzi.
Akizungumza
katika uzinduzi huo kwa wanawake vijana na wanawake wenye ulemavu katika ukumbi wa Ofisi za Tamwa Mkanjuni
Chakechake Pemba, Afisa Tathmini na
ufatiliaji Mohammed Khatib Mohammed alisema mradi huo utaimarisha uongozi wa
wanawake , wanawake wenye ulemavu na wanawake
vijana Zanzibar.
Alisema
kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya
mwaka 2022 wanawake wako asilimia 51
ambao ni wengi ulkilinganisha na wanaume,
lakini katika nafasi za uongozi wanawake
ni asilimia 38 tu idadi ambayo bado
haijaridhisha ipasavyo.
Alisema kwa
sasa Zanzibar idadi ya wanawake viongozi ni ndogo kwani ni asilimia 38 tu ukilinganisha na wanaume.
‘’ Sensa ya
watu na makazi ya mwaka 2022 inaonesha wanawake wako wengi ni asilimia 51,
hivyo Tamwa tumekuja , na mradi huo kuona wanawake, wanawake vijana na wanawake
wenye ulemavu wanahamasika kushiriki na kushika nafasi mbalimbali za
uongozi,’’alisema.
Alisema
kwamba miaka ya zamani Zanzibar ilikua imetawaliwa na mfume dume, hivyo kufuatia
mradi huo utahakikisha inaondoa
mawazo mgando kwa wanawake na
wanajamii juu ya mfumo huo.
Aliendelea
kusema kuwa Tanzania na Zanzibar
zimeridhia kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, hivyo mradi utasaidia kufikiwa kwa lengo la
asilimia ya 50 kwa 50 katika maamuzi.
‘Baada ya
mafunzo hayo wanawake vijana 60 wataunganishwa na taasisi mbalimbali za umma,
sekta binafsi na asasi za kiraia kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo masuala ya
uongozi, wajiamini na kujiandaa kuchukua nafasi za uongozi, ili kufikiwa kwa
lengo hilo la 50 kwa 50 katika uongozi,’alisema.
Kwa upande
wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka TAMWA Zanzibar Sofia Ngalapi alisema lengo hasa
ni kuwawezesha wanawake, wanawake
vijana na wanawake wenye ulemavu, kwa kuwajengea uwezo ili waweze wajiamini na kushiriki
kikamilifu katika mifumo ya kidemokrasia na nafasi za maamuzi huku wakiongeza ajira
kwa vijana.
Alisema
Zaidi ya wananchi 100,000 wanatarajiwa kunufaika na mradi huo, huku watetezi wa
haki za wanawake 60 wakijengewa uwezo wa kufuatilia,kuripoti na kushughulikia
vitendo vya ukatili kwa wanawake.
Nae Afisa
kutoka kituo cha Utafiti na Uchambuzi wa sera za kijamii Zanzibar Mohamed Salum
Ali amewataka wanawake kuhakikisha wanajitokeza kugombania nafasi mbalimbali za
uongozi, ili kuleta mabadiliko katika jamii zao.
Mradi huo wa
kuimarisha uongozi wa wanawake Vijana Zanzibar ( W-LEAD ) unatekelezwa na TAMWA
Zanzibar kwa ushirikiano na Jumuia ya wasiona (ZANAB), chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (suza) na Zanzibar Univesity
(ZU) chini ya ufadhili wa Umoja
wa Ulaya kupitia mpango wa Ushiriki wa wanawake na Vijana katika Demokrasia na kuanza
utatekelezwa wake kuanzia mwaka huu 2026 hadi 2027.
Kauli mbiu ya
mradi huo ni Kujenga Zanzibar ambayo wanawake na wanaume
wanashiriki kwa usawa katika kuunda na kuendeleza jamii zenye demokrasia na
ujumuishi kwa wote.
MWISHO.

Comments
Post a Comment