SERIKALI YAAHIDI KUWEKA MAZINGIRA RAFIKI KWA MTOTO



 NA FATMA HAMAD, PEMBA

 Naibu waziri wa wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zawad Amour Nassor,  amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kupitia Wizara hiyo  imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha ustawi na ulinzi wa watoto.

 

Naibu waziri huyo ameyasema hayo wakati  akifungua Kongamano la Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afirika lililofanyika Viwanja vya kufurahishia watoto Tibirinzi Chkachake mkoa wa Kusini Pemba.

 Alisema Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto katika ngazi zote, kuendeleza kampeni za kupinga ukatili dhidi ya watoto, kuimarisha huduma za afya na lishe, kuhamasisha malezi chanya pamoja na kuendeleza ushiriki wa watoto katika masuala yanayowahusu.

 ‘’Maisha bila udhalilishaji yanamaanisha mtoto kulindwa dhidi ya ukatili wa kimwili, kihisia, kingono, kutelekezwa, unyanyasaji mtandaoni, ajira za watoto na mila au desturi zinazoweza kuathiri ustawi wake,’’alisema.

 Alisema Pamoja na mafanikio yaliyopo, bado kuna  changamoto  mbalimbali  ambazo zimekua zikiwakumba Watoto kama vile matukio ya ukatili na udhalilishaji na baadhi ya watoto kukosa malezi stahiki.

Alisema kila Mtoto anastahiki kupata haki muhimu kama vile kulindwa, kuishi, kushiriki katika shughuli na kuwendelezwa, hivyo ni jukumu la kila mtu kuona haachwi mtoto nyuma hasa katika fursa za maendeleo.

Aidha aliisisitiza serikali kuhakikisha sera,Sheria,  Bajeti zinazingatia na kulinda  masuala ya mtoto na kudhibiti haki zao.

Mapema Afisa Mdhamini wa wizara hiyo Hafidhi Ali Mohamed alisema siku hii ya Mtoto wa Afrika inatoa fursa ya kujadili ni namna gani watoto wataishi bila ya udhalilishaji, na kupata haki zao za msingi.

‘’Ndugu mgeni rasmi sikuhii inatufanya tujadili ni kwa kiasi gani tunaweza kuwalinda watoto dhidi ya ukatili, na kuishi kwa Amani,’’alisema.

Mkurugenzi wa wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Siti Abass Ali alisema Serikali ya Mapinduzi itahakikisha inashirikiana na watoto, na kwa mwaka huu wa 2026/2027 imetenga bajeti maalumu kwa ajili ya masuala ya watoto.

Akitoa salamu kwa niaba ya Watoto wa Zanzibar Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Taifa Khamis Abdalah Mbarouk, aliipongeza serikali pamoja na wadau wengine kuweka siku hii maalumu ya kuwaunganisha watoto wote, na kupewa somo ni namna gani kufahamu udhalilishaji na kujua wajibu wao pamoja na haki zao stahiki.

Kila mwaka tarehe 16 Juni, nchi za Afrika huwa zinaadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, ambapo Siku hii ilianzishwa na Baraza la Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika mwaka 1991.

 Ikiwa  lengo lake hasa ni  kuwakumbuka watoto waliopoteza maisha yao katika maandamano ya Soweto nchini Afrika Kusini tarehe 16 Juni 1976, ambapo Watoto hao walikuwa wakipinga mfumo wa ubaguzi wa rangi uliowanyima haki yao ya kupata elimu bora na yenye usawa.


 Kauli mbiyu ya mwaka huu ni mtoto mwenye afya bora na anayeishi katika mazingira salama yasiyo na aina yoyote ya udhalilishaji ana nafasi kubwa ya kukua, kujifunza, kufanikiwa na kuchangia maendeleo ya taifa pamoja na familia kwa ujumla. 

 MWISHO.



 

Comments

Popular posts from this blog

WANDISHI WA HABARI ANDIKENI HABARI ZA UCHAMBUZI

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

UROHO WA MALI KWA WANAUME UNAVYONYIMA WANAWAKE ARDHI