BANDA LA DHARURA LA KULALA WANAFUNZI LAUNGUA MOTO
Banda la dharura la wanafunzi 80 wa Kiume katika Skuli ya Sekondari ya Chwaka tumbe Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, limeteketea kwa moto na kuunguza kila kitu kilichokuwemo katika jengo hilo.
Akizungumzia kutokea kwa moto huo mmoja kati ya wanafunzi wa Skuli hiyo Ibrahim Bakar Hamad alisema moto huo ulitokea majira ya saa nne wao wakiwa madarasani na ndipo walipowapigia simu zimamoto kutoa taarifa ya moto huo .
Alisema waliona moto unawaka kwenye Banda hilo wakaanza kuitana na walimu wao na kuchukua hatua ya kuwasilina na Kikosi Cha Zima Moto na Uokozi kuja kusaida kuuzima Moto huo.
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Chwaka tumbe Abdalla Hamad alisema banda hilo lilikuwa linatumika kwa dharura kama kambi kwa wananfuzi wanaotarajia kufanya mitihani na hadi moto huo unazimwa hakuna mwanafunzi aliyepata majereha.
Alisema walikuwa watumia banda hilo kwa dharura kusubiri kumalizika kwa ujenzi wa Bweni unaoendelea Skulini hapo lakini hatimaye Banda hilo limewaka moto.
‘’Tunashukru hadi sasa hakuna mwanafunzi aliyeathirika na tukio hilo ,Banda hili tulikuwa tunalitumia kwa wanafunzi kujiandaa na mitihani yao ya taifa wakati tukisubiri ujenzi wa Bweni letu kukamilika’’amesema Mwalimu Mkuu.
Mkuu wa kituo cha Zimamoto na Uokozi Kituo cha Kijichame Ali Khamis Mdungi alisema baada ya kupata taarifa walifika haraka kuzima lakini bado chanzo cha kuzuka moto huo hakijajulikana .
‘’Tumepata taarifa majira ya Sanne na tulipofika tukapambana kuzima moto huo tukafanikiwa lakini hadi sasa hatukufahamu chanzo Cha Moto huo’’amesema Kamanda huyo.
katika tukio hilo Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Aamali Zanzibar,Khamis Abdalla Said alisema tayari alishatoa maelekezo kwa uongozi wa Skuli kama hizo kuhakikisha wanafunzi wanakuwamakini kwa kuacha vitu wanavokatazwa ikiwemo kuchezea suwichi na kuunganisha Umeme kiholela ili kujiepusha na majanga yanayoweza kujitokeza.
‘’ Wizara ya Elimu itaendelea kuweka mazingira Rafiki kwa wanafunzi kuhakikisha wanakuwa salama na kuendeleza masomo yao kikubwa niwatake mujiepushe katika kuchezea suwichi za umeme pamoja na kuunga umeme’’amesema Abdalla.
Aidha Katibu huo alisema atahakikisha wanafunzi wote waliounguliwa na vitu vyao ikiwemo sare watapatiwa vyengine, kuona wanaendelea na masomo yao bila usumbufu wowote.
Mkuu
wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mgeni Khatib Yahya amewataka wanafunzi hao kua na
subra katika kipindi hichi kigumu huku akimtaka mkandarasi kuharakisha
ujenzi wa Bweni unaoendelea kujengwa katika Skuli hio.
‘’Niwaombe wanafunzi,wanangu kuweni pole sisi Serikali tupo pamoja n ani mtake Mkandarasi ahakikishe anamaliza ujenzi wa Dakhalia kwa haraka liweze kutumika’’amesema Mgeni.
MWISHO.


Comments
Post a Comment