Mkurugenzi wa TAMWA–Zanzibar Dk. Mzuri Aaga Rasmi, Aweka Alama Kubwa ya Mageuzi ya Kijinsia

 


NA MWANDISHI WETU

Baada ya zaidi ya miongo miwili ya kujitolea, uongozi na harakati za kutetea haki za wanawake, watoto na uhuru wa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, Tawi la Zanzibar (TAMWA–ZNZ), Dk. Mzuri Issa Ali ameaga rasmi waandishi wa habari kutokana na kuondoka katika wadhifa wake, akiacha taasisi imara yenye mifumo thabiti na mafanikio yanayotambulika kitaifa na kimataifa.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na wanachama wa TAMWA–ZNZ, Mkurugenzi huyo amesema waandishi wa habari ndio nguzo kuu ya taasisi hiyo licha ya changamoto kubwa wanazokumbana nazo lakini bado waliendelea kushirikiana na Tamwa Zanzibar katika kutumia kalamu zao kuelezea harakati za shughuli za Tamwa Zanzibar.

“Kama kuna kundi la watu wanaojua kuuliza maswali magumu, kufuatilia ukweli bila kuchoka, na bado malipo yakawa madogo au hakuna kabisa, basi hao ni waandishi wa habari. Na cha kufurahisha zaidi, hao ndio nguzo kuu ya TAMWA–Zanzibar,” alisema.

Alisema kuwa katika kipindi cha kuwa mtendaji mkuu wa Tamwa Zanzibar alifarijika sana na waandishi wa habari kutokana na kutumia vyema kalamu na vipaaza sauti katika kueleza changamoto za kijamii hususan masuala ya haki za binaadamu pamoja na vitendo vya udhalilishaji vya wanawake na watoto.

“kalamu za waandishi ilikuwa ndio nguzo kuu ya kutegemea katika kipindi cha uongozi wangu nikiwa mkurugenzi kalamu zilipaaza sauti za wasio na sauti pamoja na kueleza changamoto za kijamii hususan katika masuala ya ukiukwaji wa haki za binaadamu”, alifafanua mkurugenzi.

Akieleza kuwa mashirikaino hayo ya karibu yameweza kwa kiasi kikubwa kusaidia jamii na kupungua changamoto za wanawake na watoto pamoja na makundi mengine ya pembezoni kama walemavu na wazee.

“Nguvu yetu ilikuwa ni ya waandishi wa habari tukiamini kuwa nguvu ya habari inaweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii lakini pia kuibua kero za wananchi pamoja na kuizundua serikali” alisisitiza.

Kupitia miradi mbalimbali, TAMWA–ZNZ imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wanawake na watu wenye ulemavu 11,120 kupitia vikundi 572 vya kuweka na kukopa, kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, na kuchangia mabadiliko ya sheria muhimu ikiwemo Sheria ya Ushahidi, Sheria ya Mahakama ya Kadhi na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Leo, TAMWA–Zanzibar ina wanachama 82 waandishi wa habari kutoka Unguja na Pemba, wafanyakazi 23 wenye weledi, mifumo imara ya kifedha inayoendeshwa na wahasibu wenye ithibati ya CPA, pamoja na ukaguzi wa hesabu unaofanywa na kampuni zilizosajiliwa kitaifa. Taasisi hiyo pia inamiliki majengo yake yenyewe ambayo yameanza kuchangia mapato ya ndani.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi huyo alitangaza rasmi kukabidhi majukumu kwa Bi. Nairat Abdulla Ali, aliyekuwa Meneja wa Programu, akimtaja kuwa kiongozi mwenye maadili, uwezo na maono thabiti ya kuiendeleza taasisi hiyo.

“Nawaomba wanachama, waandishi wa habari na wadau wote kumpa ushirikiano mkubwa. Taasisi imara haijengwi na mtu mmoja, bali hudumu pale uongozi unapobadilika na dira ikibaki ile ile,” alisema.

Katika hafla hiyo waandsihi wa habari waliohudhuria waliishukuru kwa dhati Tamwa Zanzibar kwa kuwa nao karibu pamoja na kuwajengea uwezo katika kuimarisha weledi na umahiri katika taaluma ya habari.

Khatib Suleiman kutoka Habari leo amesema kuwa Tamwa imewasaidi kuwajengea uwezo hususan katika kuandika kwa weledi na kuimarisha uwezo wetu katika namna ya kuripoti masuala ya haki za wanawake na watoto pamoja na haki za binaadamu kwa ujumla.

“Tamwa Zanzibar imekuwa ni chuo katika kuimarisha taaluma ya uandishi na tumeweza kuandika kwa weledi na umahiri huku tukizingatia maadili ya wanahabari”, alifafanua.

Berema Suleiman kutoka Zenji Fm alisema kuwa tamwa Zanzibar imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha taaluma lakini pia katika kuwapatia mafunzo waandishi chipukizi katika kuimarisha utendaji wa kazi zao.

“Mafunzo tuliyoyapata yamesaidia katika kuimarisha taaluma na kutujengea uwezo hususan katika kufuatilia habari zetu pamoja na kuwa na vyanzo tofauti na kuwapa nafasi makundi ya wanawake na vijana pamoja na walemavu”, alifafanua.

Wafanyakazi wa tamwa Zanzibar walishukuru kwa uongozi wa Dk. Mzuri hususan katika kuimarisha utendaji wa kazi zao huku wakizingatia weledi na umahiri katika kuandika ripoti na pia kufanya kazi kwa kuweza kupata matokeo

Zaina Mzee Afisa mwandamizi wa Tamwa Zanzibar alisema kuwa ulipokuja kuongoza taasisi hii, hukurithi tu ofisi na majukumu, bali pia changamoto nyingi. Kwa busara, maono na uongozi wako thabiti, uliweza kuibadilisha taasisi yetu na kuifanya kuwa mfano wa uwajibikaji, mshikamano na utendaji bora. Chini ya uongozi wako, tulijifunza kuwa kazi si wajibu tu, bali ni wito na dhamana ya kulitumikia taifa kwa uadilifu.

Akitoa neno la shukurani mkurugenzi mpya wa Tamwa Zanzibar Nairat Abdulla amesema kuwa anapokea dhamana hii akiwa na ufahamu kwamba uongozi si kauli, bali ni vitendo; si ahadi, bali ni uwajibikaji. Ninapokea nafasi hii nikitambua kuwa taasisi huimarika si kwa mipango iliyoandikwa vizuri pekee, bali kwa utekelezaji thabiti, wenye nidhamu na mwelekeo unaofahamika.

Ninawaahidi kushirikiana nanyi kwa karibu, kusikiliza kwa makini, na kuchukua hatua kwa wakati. Milango yangu itakuwa wazi kwa hoja, mawazo na suluhisho, kwa sababu uongozi wa pamoja na mashirikiano ni muhimu katika kuimarisha kazi zetu, alisisitiza.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa kutoa zawadi mbali mbali kwa mkurugenzi aliyemalaiza muda Dk. Mzuri Issa ikiwa ni sehemu muhimu ya kutunza kumbukumbu ya utumishi wake uliotukuka.




Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO