UISLAMU NA UMILIKI WA ARDHI KWA MWANAMKE

 


Je, ni vipi uislamu unampa nafasi mwanamke kumiliki

ardhi?

NA FATMA HAMAD, PEMBA

Kwa muda mrefu, kumekuwepo na dhana potofu katika

baadhi ya jamii, hususan Zanzibar, kwamba mwanamke

hana haki ya kumiliki ardhi.

Dhana hii imejikita zaidi katika mila na tamaduni kuliko katika misingi ya dini ya Kiislamu.

Viongozi wa dini na wanaharakati wa haki za

wanawake wamekuwa mstari wa mbele kupinga

mtazamo huo, wakisisitiza kuwa Uislamu unamtambua

mwanamke kama mmiliki halali wa mali, ikiwemo

ardhi.

Ingawa viongozi wa dini ya kiislamu wanapinga

mtazamo huo, wanaeleza kuwa mwanamke ana haki ya

kurithi, kununua, na kutumia mali au ardhi kwa ridhaa

yake mwenyewe.

Kiongozi wa dini ya kiislamu kutoka kijiji cha Wingwi Njuguni kisiwani Pemba Juma Othman Nahoda  anasema ‘’Urithi ni haki ya mwanamke, na si hisani’’

Anasema katika Suratul- Nisa, aya ya saba (7) ‘’wanaume

wanafungu katika walichoachiwa na wazazi wao na

wanawake pia wanafungu katika walichoachiwa, iwe

kidogo au kikubwa, ni fungu lililowekwa’’.

Hii inamaanisha kuwa urithi wa ardhi au mali ni haki

ya mwanamke kwa amri ya Allah, na si kwa hiari ya

binadamu.

Sheikh Abdallah Mnubi Abass kutoka Jumuia ya Maimamu Zanzibar

alinukuu Hotuba ya Mtume Muhammad

(S,A,W) :

‘’Mtume alisema Mali zenu, damu zenu, na heshima zenu

ni takatifu’’ hii inajumuisha mali ya mwanamke, ardhi

yake haichukuliwi kwa nguvu wala hila, bali kwa ridhaa

yake tu.’’

Sheikh Said Ahmed Mohamed kutoka Ofisi ya Mufti kisiwani Pemba, anasema wanawake pia wanahaki ya kuchuma

na kumiliki.

Anasema katika aya ya 32 ya suratul Nisai, inaeleza

kuwa ‘’Wanaume watapata walichokichuma na

wanawake watapata walichokichuma.’’

Aya hii inathibitisha kuwa mali anayopata mwanamke

ni yake halali, akinunua ardhi, hakuna kizuwizi cha dini

kinachomzuia.’’

Hata Bi Amirat kutoka Jumuiya ya wanawake wa kiislamu

Pemba (JUMA WA KIPE) Asya Amour Abrahman anasema

Uislamu umemnyanyua mwanamke, hivyo kwa mujibu wa

Sheria ya Dini ya Uislamu na yeye anahaki ya kumiliki Ardhi.

‘’Mwanamke anahaki ya kumiliki ardhi na akaweza

kuitumia kwa shughuli za kilimo, na akajipatia kipato

kutokana na Shamba lake, isipokua kuna mipaka yake katika

suala la mirathi tu,’’anafafanua.

Anasema mwanamke anahaki ya kufanya shughuli zozote za

kimaendeleo na kujipatia kipato, ambacho kinakubalika

katika uislamu.

JAMII/WANAWAKE WENYEWE

Fatma Mkubwa Ali mkaazi wa Mjini Ole ambae

anajishughulisha na kilimo Msitu anasema yeye ana miliki

shamba lake mwenyewe.

‘’Wazazi wangu walipofariki nilipewa ardhi yangu , na sasa

naitumia kwa shughuli za kilimo Msitu, nazalisha mazao,

kwa ajili ya chakula nyumbani na mengine ninakuja kuuza

nipate pesa,’’anasema.

Anasema umuhimu mkubwa wa mwanamke akiwa na ardhi

yake mwenyewe ni kujipatia kipato kwani anaweza kulima

kilimo cha muda mfupi na cha muda mrefu ambacho atapata Chakula, Pesa pamoja na kulinda athari za mazingira.

Afisa sheria kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Pemba, Massoud Ali Massoud , akiwakumbusha wananchi, wa Micheweni kurithi mali za marehemu mapema, ili kuepusha migogoro inayozuilika,  kwenye mkutano wa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, uliofanyika Skuli ya Michweni.

WANAHARAKATI

Kaimu Mratibu wa Chama cha Wandishi wa Habari

Wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar, Ofisi ya Pemba Amina Ahmed Mohamed anasema wanawake wanahaki ya kumiliki ardhizao wenyewe kama Dini na Sheria zinavyoelekeza.

Anasema moja ya mkakati wanaoufanya ni kuihamasisha jamii kuhakikisha wanawake nawao wanakua na ardhi zao wenyewe, ima kwa kununua ama kurithishwa wakati wanapofariki wazazi wao.

‘’Kutokana na janga la Mabadiliko ya tabianchi linalotukumba,ni vyema wanawake nawao wakawa na ardhi zao wenyewe, ili wajipatie kipato chao kutokana na ardhi zao wenyewe,’’anasema.

Sada Juma Segeja mtetezi wa masuala ya wanawake kutoka

Jumuia ya Uhifadhi wa misitu kisiwani Pemba CFP, anasema

bado jamii imekua na mitazamo potofu kwamba mwanamke

hawezi kumiliki ardhi.

Anasema moja ya changamoto inayowakabili katika mradi

wao wa uhifadhi mazingira ni baadhi ya wanawake kukosa

rasilimali Ardhi, kwa ajili ya kufanyia shughuli hizo za

uhifadhi, jambo linapelekea kuanguka kiuchumi, na

kuathirika na mabadiliko ya tabianchi.

‘’Katika mradi wetu wa uhifadhi wa mazingira ambao

tunautekeleza katika Shehia za Chwale, Mchanga mdogo,

Kambini na Mjini kiuyu, tunapata changamoto kubwa ya

baadhi ya wanawake kukosa ardhi zao wenyewe,’’anasema.

Anasema licha kwamba wanawake wamekua wakirithi

ardhi baada ya wazazi wao wanapofariki, bado mali hizo

huhodhiwa na kaka ama ndugu zao wa kiume, na kupelekea

wao kukosa sehemu ya kufanyia shughuli ambazo zinaweza

zikazalisha kipato.

NINI KIFANYIKE

Kwa mujibu wa viongozi wa dini, hakuna aya wala hadithi

inayomnyima mwanamke haki ya kumiliki ardhi, kinyume

chake uislamu unampa ulinzi, heshima kamili katika mali

yake, isipokua ni mila na tamaduni za jamii, hivyo ipo haja

sasa kuondokana na mila hizo kuona mwanamke na yeye

anamiliki ardhi yake mwenyewe,  aweze kuzalisha na kujipatia kipato.

MIKATABA

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu

cha 12 (a) kinaeleza kuwa watu wote ni sawa mbele ya

Sheria, na wanayohaki, bila ubaguzi wowote, kulindwa na

kupata haki sawa mbele ya Sheria.

Hata Sheria ya ardhi Zanzibar namba 12 ya mwaka 1992 inaeleza kuwa ardhi ya Zanzibar ni mali ya umma, hivyo kila mwananchi anahaki ya kutumia ardhi.

Mkataba wa Umoja wa Mataifa CEDAW wa mwaka 1986, unapiga marufuku ubaguzi wa kijinsia katika umeliki wa mali.

Itifaki ya Maputo (kifungu cha 21) inahakikisha wanawake wanapata urithi bila kubaguliwa na tamaduni.

Makadirio  ya  Bajeti  kwa  mwaka wa  Fedha  2023/2024   ya Wizara  ya  Ardhi  na  Maendeleo  ya  Makaazi,  Kuendelea  kutoa  elimu  kwa  jamii  kuepuka  kujiingiza  kwenye  migogoro  ya  ardhi  kwa kufuata  Sheria  za  ardhi

Katika tamko la Machi 2024, lilotolewa na Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanziba  linasisitiza kwamba ‘’Sera za jinsia lazima ziwepo katika sekta zote, ili wanawake wasiachwe nyuma.’’

Kwa mujibu wa Utafiti alioufanywa na Mkurugenzi wa Chama hicho Mzuri Issa Ali, mwaka 2025, ulionesha kuwa mitazamo ya jamii na vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuendeleza au kupunguza mitazamo hiyo potofu.

MITANDAO YA KIJAMII/MWANANCHI

Mkurugenzi wa huduma za kisheria wa kituo cha sharia cha Haki za binadamu(LHRC), Funlgence Massawe anasema serikali imepiga hatua kubwa katika kurekebisha sharia zinazokua zinakwamisha umiliki wa ardhi kwa wanawake.

Mkurugenzi huyo ameyasema hao Novemba 26, 2020 jijini Dar es Salaam wakati akichangia kwenye mjadala wa Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communication ltd (MCL), anasema tofauti ya kipato ni sehemu kubwa inayochangia ukatili wa kijinsia, huku akigusia katiba ya Tanzania kuhusu haki ya kila mtu kumiliki mali, akisisitiza kuwa haijasema mwanamme au mwanamke bali mtu yoyote.

Anasema sheria  ya mirathi inamatatizo na inatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kutoa fursa kwa wanawake tofauti na ilivyo sasa.

Anabainisha kuwa ardhi ndio chanzo kikubwa cha migogoro katika jamii na wanawake wamekua wakinyanyaswa kwa kunyimwa umiliki wa ardhi. 


 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO