JAMII YAHIMIZWA KUITUNZA AMANI ILIYOPO NCHINI

 


NA FATMA HAMAD, PEMBA

Viongozi wa kamati za  dini mbali mbali kisiwani Pemba (Pemba Interfaith Committee) wameipongeza jamii ya  wazanzibari kwa kuendelea kuishi kwa umoja na mshikamano, jambo lililoifanya Zanzibar kua mfano bora wa ustaarabu na utulivu.

Akitoa tamko la kamati hiyo katika kikao cha kufanya tathmini ya juhudi zilizofanywa na kamati hiyo za kushajihisha amani  kabla, wakati na baadhi ya uchaguzi mkuu uliofanyika Zanzibar mwenzi Oktaba mwaka huu, Mwenyekiti wa kamati ya dini mbali mbali kwa upande wa wanawake Amina Salim Ahmed  katika ukumbi wa mikutano wa Samail Gombani Pemba aliipongeza jamii ya kwa kuendelea kuishi kwa umoja na mshikamano jambo lililoifanya zanzibar kua mfano bora wa ustaarabu.

Alisema hali hiyo ilikuja kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na viongozi wa dini, Serikali, na wananchi katika kudumisha misingi ya maelewano ambayo imeijenga Zanzibar.

Alieleza tamko hili ni mwendelezo wa wito wa kila mara unaosisitiza kwamba amani tulionayo ni tunu na kial mmoja anapaswa kuithamini na kuilinda kwa matendo ya kheri na kauli zenye hekima.

Alifafanua kua dini zote upendo, ustahamilivu, na kuheshimu utu wa kila mwanadamu, hivyo ni vyema kila mmoja kuendeleza kuyaishi mafunzo haya katika maisha ya kila siku.

"Dini zote zinafundisha upendo, ustahamilivu na kuheshimu utu wa kila mmoja, hivyo ni vizuri muendelee kuyaishi mafunzo haya katika maisha ya kila siku" alieleza.

Aidha aliendelea kusisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kutumia marifa, busara na subira katika kushughulikia mambo mbali mbali ya kijamii na kifamilia ili kudumisha amani iliopo katika visiwa vya Zanzibar.

Aidha alisisitiza matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuelimishana na kuhamasishana mambo yenye faida kwa jamii  pamoja na kuepuka taarifa zisizo za msingi au kauli zinazoweza kupunguza heshima baina ya watu.

Aidha taasisi hiyo ilitoa shukrani kwa taasisi zote zinazounga mkono juhudi za kukuza amani, kujenga uwezo wa vijana na kuimarisha huduma za kijamii.

Awali  akiizungumza katika mkutano huo Mratibu Ofisi ya Mufti Pemba Said Ahmad Mohamed aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kuhubiri amani katika maeneo yao, pamoja na kutoa taarifa za viashiria vya uvunjifu wa amani katika vyombo vya sheria.

"Endeleeni kuhubiri amani katika maeneo yenu kwa kutumia njia mbali mbali ili kuhakikisha amani iliopo inadumu toeni taarifa ya viashiria vya kuvunjwa kwake katika vyombo vya sheria ili hatua ziweze kuchukuliwa, " alieleza.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo Fadhil Juma Mohamed  Naibu katibu wa Jumuiya ya walimu wa Madrasa Pemba alisema, wamekua wakifanya juhudi mbali mbali za kuelimisha jamii kwa kuwafikia watu wa makundi mbali mbali wakiwemo vijana na wanawake katiika kulinda amani kwa kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani katika kipindi chote cha uchaguzi mpaka kumalizika kwake.

Aidha waliahidi kuendeleza kutoa elimu hiyo kwa kila kundi lililopo katika jamii zao, ili kuona Zanzibar inaendelea kudumumu katika amani kwa maslahi ya nchi.

Kwa upande wake Afisa Mradi wa Swahili Coast wa kamati hiyo Khelef Nassor Rashid alisema, kamti hiyo inayojumuisha viongozi wa dini, Vijana na wanawake inalengo la kuhubiri amani pamoja na kushajihisha  maadili  ambayo yatawafanya vijana kuishi katika ustaarabu wa  jamii zao.

Kamati za dini mbali mbali imekua ikifanya kazi ya kutoa elimu ya utunzaji wa amani  kwa kushirikiana na shirika la Norway Church Aid (NCA) kupitia mradi wake wa Swahili Coast kwa mashirikiano ya ubalozi wa Norway nchini Tanzania.



                                                          

 

Comments

Popular posts from this blog

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO

‘’KATIBU MKUU ELIMU ‘’TOENI ELIMU YA MALEZI BORA’’