SAFARI YA WANAWAKE WENYE ULEMAVU KUELEKEA UONGOZI

 

                        NA FATMA HAMAD,PEMBA

Kadri Tanzania inavyoelekea katika uchaguzi kuu kunakua na mijadala mingi kuhusu ushiriki wa makundi maalum hasa Wanawake Wenye Ulemavu.

 Kwani ni muda mrefu kundi hili linakuwa likipigania nafasi sawa katika siasa, uongozi na maamuzi, safari yao inaendelea kuwa yenye milima na mabonde, ingawa mwakahuu inaonesha matumaini.

Nasra Fakih Hassan mwanamke mwenye ulemavu wa mguu   mzaliwa wa Kangagani Wete Pemba , ambaye amejitosa kugombea nafasi ya uwakilishi viti maalumu, anasema mchakato wa uchaguzi umewaonesha matumaini, ingawa bado unahitaji mageuzi kwa watu wenye ulemavu

‘’Mara hii tunashukuru na ndio maana wanawake wengi wenye ulemavu tumejitokeza kuchukua fomu na kuwania nafasi mbali mbali za uongozi, ingawa si hayo tu bali hata kwenye kampeni tunashiriki kwa wingi na kusikiliza sera za wagombea,’’anasema.

Nasra anabainisha kuwa, licha ya changamoto hizo, mwaka huu anaona hatua za matumaini, hasa baada ya Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar kushirikiana na Tume ya Uchaguzi (ZEC) kutoa elimu ya uraia na kuhimiza ushiriki wa watu wenye ulemavu.

Halima Suleiman Ali mkazi wa Mtambile  amejitosa kuania udiwani Wadi ya Mtambile anasema uchaguzi unaonesha mwanga kwao, kwani wanawezeshwa kimafunzo, amekua na uthubutu, amejitokeza kwenye kinyn’ganyiro cha kuwania uongozi.

‘’Sijawahipo hata siku moja kuchukua fomu, ila Kutokana na ushirikishwaji kupitia mashirika na jumuiya mbalimbali  mwaka huu nimethubutu kujitupa jimboni na kuusaka udiwani, ingawa sikufanikiwa”

Kwa upande wake Amina  Abdala Saidi mwenye ulemavu wa viungo mteule wa nafasi ya udiwani viti maalum, kupitia Chama cha ACT WAZALENDO Wadi ya Changaaweni Mkoani Pemba, anasema uchaguzi wa mwaka huu 2025, baadhi ya mambo yamebadilika, na ndio maana akafanikiwa kupata nafasi hiyo.

‘’Nashukuru sijabaguliwa wananiona nafaa, na hata kwenye kampeni nachukuliwa siku zote, bila vikwazo vyovyote,’anafahamisha

Amina anasema yapo mambo kadhaa ambayo yanafanya Wanawake Wenye Ulemavu kuonekana hawawezi kushiriki kikamilifu kwenye chaguzi, Kuanzia gharama za uchukuaji wa fomu, kampeni hadi upigaji kura.

‘’Katika chaguzi zilizopita hata baadhi ya vituo vya uchaguzi  havikua na mazingira rafiki kwa Mtu Mwenye Ulemavu, ingawa uchaguzi huu tunaimani mambo yatabadilika,’’anasema.

JAMII

Katika mazungumzo na baadhi ya wakazi wa Unguja na Pemba, wengi wanakiri kuona hamasa kubwa ya wanawake wenye ulemavu kushiriki katika harakati za kisiasa.

Ali Otman Bakari mkaazi wa Unguja na Asha Ali mkaazi wa Ziwani Pemba, wanasema kundi la Watu Wenye Ulemavu linaonekana kwa wingi kwenye kampeni.

Wanasema moja ya sababu inayochangia kushiriki kwenye kampeni hizo ni mazingira rafiki ya Uchaguzi ya kupewa elimu kufahamu haki zao, sambamba na Amani na utulivu uliopo.

 “Ni vizuri kuona kundi la watu hawa wanashiriki harakati zote za chaguziji, kwani wanaonyesha uwezo wao, ingawa bado jamii yetu inahitaji elimu zaidi juu ya kuzifahamu haki, fursa za watu Wenye Ulemavu,”wanaeleza.

WANAHARAKATI

Hidaya Mjaka Ali, mwanaharakati  kutoka Jumuia ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar JUWAUZA anasema uchaguzi wa 2025, mambo yamebadilika, na kupelekea jumla ya Wanawake Wenye Ulemavu 12 kujitosa na kuchukua fomu za kuwania uongozi, ambapo haijawahi kutokea.

“Ni kweli, Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC wanaanza kujumuisha vipengele vya upatikanaji wa huduma kwa Watu Wenye Ulemavu kwenye sera zao za uchaguzi, ingawa utekelezaji wake bado ni changamoto,’’anasema.

Kampeni zimekua za kistarabu hakuna vurugu, jambo linalowapa hamasa Watu Wenye Ulemavu kushiriki kwa wingi kwenye kampeni kusikiliza sera za wagombea, ambao ni nadra  kwa chaguzi zinazopita.

Mashavu Juma Mabrouk kutoka Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Ofisi ya Pemba, anasema hali ya mwaka huu inaonyesha mabadiliko,licha kwamba bado kuna ukakasi.

“Wakati mwingine wananyimwa nafasi si kwa sababu hawawezi, bali jamii haijaamini uwezo wao, hilo ndilo tunalopigania kulibadilisha mwaka huu,” anafahamisha.

Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA Zanziba  kimekua kikichukua hatua mbali mbali, kuona wanawake wenyeulemavu wanapewa nafasi sawa, mafunzo na katika michakato ya kampeni na uchaguzi.

‘’Tumeona marahii hali inaonesha matumani, uzuri zaidi ni kuona kuna baadhi ya vyama vya siasa vikichukua wakalimani katika kampeni, jambo ambalo linapaswa kuigwa kwa vyama vengine,’’anasema Amina Ahmed kutoka Tamwa Zanzibar Ofisi ya Pemba.

Anasema huu ni mwaka wa mabadiliko wamechoka kuona wanawake wenye ulemavu wakitazamwa kama wakulima wa pembezoni, wanataka wawe viongozi, wabunge, wawakilishi, na hata mawaziri.

Afisa mfawidhi kutoka Tume ya Haki za Binadamu Ofisi ya Pemba  Suleimana  Salim  Ahmad  anasema kufuatia mabadiliko yanayofanywa na kuona ushiriki mzuri wa watu wenye ulemavu katika upigaji kura,ni vizuri vyama vya siasa kuweka ujumuishi wao katika kampeni zinazoendelea.

‘’Pamoja na jitihada zinazofanywa, bado baadhi ya vyama vya siasa, havijazingatia ipasavyo mahitaji ya watu wenye ulemavu katika mikutano yao, suala ambalo linawanyima haki yao ya msingi ya kufuatilia sera za vyama zitakazo wasaidia  kufanya maamuzi sahihi ya kura zao,anasema.

Anasema mazingira mazuri katika mikutano ya kampeni, inasaidia kufuatilia sera zinazotolewa na vyama vya siasa katika nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani,  ambapo itasaidia kuwachagua viongozi wanaowataka.

VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha Alliance for  Democratic  Change ADC Hamad Rashid Moh’d anasema katika chama chake wameweka miundombinu maalumu kwa watu wenye ulemavu,ili washiriki mikutano ya kampeni ikiwemo, usafiri.

Pia anasema katika mawakala wao watakaosimamia uchaguzi mkuu, wameweka nafasi maalumu kwa watu wenye ulemavu.

KAULI YA RAIS

 Mgombea wa Urais wa Zanziba kupitia chama cha Mapinduzi CCM ambae pia ni Rais wa Zanzibar Ali Hassan Mwinyi anasema wakati atakapopata ridhaa na kuingia madarakani, ataimarisha ustawi wa jamii, kupunguza ubaguzi, na kujenga Zanzibar inayompa kila mtu nafasi ya kufikia ndoto zake bila kikwazo, kulingana na hali yake ya kimwili na mahitaji yake.

Pia anasema ataongeza nafasi za ajira na uteuzi kwa watu wenye ulemavu, ili nao wawe sehemu ya maamuzi.  

TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR

Juma Msanif Sheha Mkuu wa Programu kwa wapiga kura na msimamizi kutoka Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC anasema ili kuona  Watu Wenye Ulemavu  wanashiriki kwenye harakati zot za uchaguzi wamekua wakiwapatia elimu, kufahamu haki na wajibu wao katika kipindi chote cha chaguzi.

‘’Tunawapa elimu ya uraia, wafahamu haki zao, kuona hawaachwi nyuma katika harakati zote za uchaguzi.

Sambamba na hilo anasema wamejipanga kuweka wakalimani, mashine ya nukta nundu vitambulisho maalumu kwa ajili ya Watu Wenye Ulemavu katika vituo vyote vya kupigia kura, ili kuwarahisishia kupata haki yao ya kikatiba ya upigaji kura bila vikwazo.

TAKWIMU

Jumla ya Watu 7891 Wenye Ulemavu wanatarajiwa kupiga kura, ikiwa Wenye Uwalbino ni 100, Wasiona 655, Viziwi 1573 na Uoni hafifu ni 2325.

Ambapo  wenye Ulemavu wa viungo ni 1998, huku Wenye Ulemavu mchanganyiko ikiwa ni 1240.

MIKATABA

Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Namba 8ya mwaka 2022, kifungu cha 20 kinaeleza umuhimu wa watu wenye ulemavu kuweza kufikia miundombinu mbali mbali, pamoja na taarifa, mawasiliano na haki zote za kibinadamu na za msingi.

 Aidha, Tanzania imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), unaohimiza serikali kuhakikisha ushiriki sawa wa Watu Wenye Ulemavu katika siasa na maamuzi.

Hata Mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na haki za kisiasa ya mwaka 1966 kifungu cha 25, kila raia ana haki ya kupiga kura na kuchaguliwa katika uchaguzi wa kweli, wa haki na wa mara kwa mara, uliofanywa kwa kura ya siri na kuhakikisha uhuru wa wapiga kura.

Hata Katiba ya Zanzibar ya 1984, ambayo ndo sharia mama, kupitia kifungu chake cha  21(1) nacho kinatambua haki ya kila raia kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi bila ubaguzi.




 

 

 

 


Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO