MARYAM ALI: MGOMBEA UWAKILISHI ANAEPANIA KUMALIZA KERO ZA JIMBO LA MTAMBWE


NA FATMA HAMAD, PEMBA

Maryam Ali Rashid ni mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM, anaewania uwakilishi jimbo la Mtambwe.

Binti huyu anaweka historia ni mfano tosha kwa wanawake, kwani amekua na uthubu wa  kuingia kwenye kinyan’ganyiro cha kusaka Jimbo akiwa bado ana umri mdogo, ana miaka 34.

 Ameanza kushiriki katika shughuli za kijamii kupitia vikundi vya wanawake na miradi ya maendeleo kijijini kwao, maji elimu ya watoto na uwezeshaji wanawake hapo ndipo alipoanza kuingizwa zaidi kwenye siasa za chama kwa sababu kazi zake zinaonekana.

‘’Nimeanza kwa kutetea shida ya maji kijijini kwangu, ambayo imekua inawakwaza wananchi  kwa muda mrefu, na nimefanikiwa na sasa shida imeondoka,’’anasema.

 Baada ya kuona matokeo hayo watu wakanza kumuomba aingie kwenye uongozi, afike kwenye ngazi za juu, aendelee kuwatetea.

NAFASI AMBAZO AMEWAHI KUSHIKA KABLA YA KUGOMBEA

Kabla ya kugombea uwakilishi Maryam alishika nafasi mbalimbali za kijamii na ndani ya chama katika ngazi ya shehia na wilaya.

Miongoni mwa nafasi ambazo ameshazishika ni kuwa msimamizi wa miradi ya wanawake,  Katibu wa Baraza la Vijana Tanzania.

Ya muhimu zaidi ni kazi zake kama mwenyekiti  wa kikundi cha Ujima Cooparative ambacho kinashughulikia ufadhili wa biashara ndogo ndogo na elimu ya kila raia, jukumu lililoijenga sifa yake kwa wanajamii.

KILICHO MSHAWISHI NA KILICHOMSAIDIA KUPATA NAFASI YA KUGOMBEA

Maryam anasema kuwa msukumo mkubwa ulitokana na wanajamii waliomuona akifanya kazi za kujitolea.

Alipata ushawishi kwa Wakulima, walimu wa Skuli za msingi, viongozi wa kijiji na wanawake, pia alipata ushawishi kutoka kwa viongozi wa chama jimboni ambao walimtambua kwa uwezo wake wa kutatua matatizo ya wanakiji chao.

‘’Kiongozi wa chama change ananiona nashughulikia malalamiko ya maji kijijini kwetu, akaanza kuniamini na akaona naweza kuleta mabadiliko katika baraza la uwakilishi,’’ anasema.

Kipengele chengine ambacho kimemsaidia ni mtandao wa wanawake na mashirika ya kijamii anayoshirikiana nayo, pamoja  na ujuzi wa usimamizi wa miradi na uwezo wa kuzungumza hadharani.

CHANGAMOTO ANAZOKUMBANA NAZO

Moja ya changamoto ambazo anakumbana nazo ni mtazamo potofu kwa baadhi ya wanaume kumtisha kwamba hawezi kupita kwani mwanamke si kiongozi.

SERA NA MATARAJIO YAKE

Miongoni mwa vipaumbele vyake ambavyo ameviweka Maryam ni kuendeleza ajira za vijana na wanawake kupitia ufadhili wa biashara ndogo ndogo, na uwajibikaji wa serikali katika utoaji wa huduma.

Pia ataziendeleza sheria zinazowezesha ushiriki wa wanawake katika ngazi zote za uongozi na kuimarisha utekelezaji wa sera za ardhi, ambapo ni kikwazo kwa wanawake wakulima.

Matarajio yake ni kuona Mtambwe inabadilika ndani ya muhula mmoja kwa kuongezeka upatikanaji wa maji safi, upanuzi wa huduma za afya za msingi, na elimu bora kwa wasichana.

‘’Nataka kila mtoto wa Mtambwe asome bila kikwazo, kila kijiji kipate maji na kila kijana awe na ajira’’.

Maryam anaishukuru familia yake kwa kumsaidia kila hatua anayopitia, ili atimize ndoto zake.

‘’Kiukweli siku nikipata ridhaa na kuwa muakilishi mama yangu ndie mtu wa mwanzo anaesababisha mimi kuwa kiongozi, kwani ile pesa ya  niliyokwenda kuchukulia fomu ya kugombea amenipa yeye, ni pesa yake ya kila mwisho wa mwezi anayoipata kwenye pesa za wazee,’’anasema.



FAMILIA YAKE

Mama yake anasema wakati mtoto wake huyo alipomshauri anataka kujiunga na harakati za kisiasa hajamzuia, bali anamuunga mkono na kumsaidia kila hatu.

‘’Sijamzuia mtoto wangu  kuingia kwenye siasa kwani naamini endapo atafanikiwa kulikamata jimbo, ambapo ndo kiyu yake, ataifanyia vyema  dhamana atakayopewa na wananchi wake,’’anafahamisha mama yake.

Hamad Ali Rashid (sio jina halisi) ni ndugu wa Maryam, anasema kutokana na  mambo ambayo anayafanya kusaidia wanawake, pamoja na wanafunzi wa Skuli, wanamatumaini makubwa dada yao huo anaweza kulikamata jimbo la Mtambwe na akalibadilisha kkwa maendeleo.

 ‘’Dadaetu tunamuamini na endapo wananchi watamchagua, jimbo la Mtambwe litan’gara kwa maendeleo, kwavile kiongozi mwenyewe ameonyesha uthubutu wake wa kuwatatatulia shida zao tokea mapema’’.

KIONGOZI WAKE WA CHAMA

Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Wete anamsifu Maryam kwa kuendelea kufanya kazi za kujitolea  ndani ya chama na kuwaonesha matokeo mazuri.

Mwalimu mkuu Skuli ya Msingi Kijumbani iliyopo Kisiwani kwa Bintiabedi Hamad Khamis Hamad anasema Maryam ni mwanamke anaefaa kupewa dhamana.

Anasema  mgombea huyo anaonesha matumaini kabla hajaingia kwenye maamuzi, kwani kupitia Ushirika wake wa Ujima Coperative amekua akisaidia  vifaa mbali mbali kama vile sare za Skuli za wanafunzi pamoja na karatasi kwa matumizi ya Ofisi.

 ‘’Tulikua tuna wanafunzi ambao sare zao zimechanika miguuni na magotini, hali zao zinatilisha imani kwekweli, ingawa Maryam amewasaidia na sasa wako hali nzuri wanaendelea na masomo,’’.anaeleza.

JAMII

Wazee na vijana wa kijiji cha Mtambwe, wanasema wanafurahi kuona mwanamke wa kwanza kusimama jimboni akiwa na shauku ya kwenda, kutetea matatizo yao kwenye maamuzi bila woga.

WANAHARAKATI

Wanaharakati masuala ya wanawake mfano Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar wanamuona Maryam kama mfano wa kuigwa, anauwezo mkubwa wa kuleta nafasi za ajira, kwa wanawake na kukuza elimu ya wasichana.

Kaimu Mratibu wa Chama hicho Ofisi ya Pemba Amina Ahmed Mohamed anasema, moja ya mkakati wao ni kutoa elimu kwa jamii, kuona wanawake wanahamasika kuingia kwenye maamuzi, watetee shida za wanawake wenzao.

VIONGOZI WA DINI

Viongozi mbalimbali wa dini wamekua wakisisitiza kwamba wanawake  wapewe nafasi, kwani wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kuleta mabadiliko.

Wanaendelea kusema kuwa Hakuna dini hata moja inayomzuia fursa mwanamke, ambayo itakuepo kwenye maeneo yao.

Safri ya Maryam ni mfano wa mabadiliko ya kijamii, ni kielelezo cha ndoto za wanawake kuingia kwenye uongozi  bila  kuogopa changamoto.

‘’Hii si safari yangu pekeyangu, ni safari ya wanawake wote wa Zanzibar”

Ilani ya Uchaguzi na serikali za mitaa  ya mwaka 2019 na  Uchaguzi Mkuu 2020  inalenga  serikali kuu iliyoko madarakani na ile itakayoshika madaraka na taasisi zake, ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa uwanja wa ushindani wa kisiasa ni huru na wa salama kwa makundi yote hususani wanawake.

Hata Mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na haki za kisiasa ya mwaka 1966 kifungu cha 25, kila raia ana haki ya kupiga kura na kuchaguliwa katika uchaguzi wa kweli, wa haki na wa mara kwa mara, uliofanywa kwa kura ya siri na kuhakikisha uhuru wa wapiga kura.

Hata Katiba ya Zanzibar ya 1984, ambayo ndo sharia mama, kupitia kifungu chake cha  21(1) nacho kinatambua haki ya kila raia kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi bila ubaguzi.



 

 

 

 

 

 

  

 

 

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO