KAMPENI ZA UCHAGUZI 2025, FURSA MPYA KWA WANAWAKE PEMBA
NA FATMA HAMAD, PEMBA
WAKATI kampeni za
uchaguzi mkuu wa 2025 zikiendelea kupamba moto kila kona kisiwani Pemba, wananchi
wanamiminika kwa wingi kusikiliza sera za viongozi wao, huku wakiwa na biashara
zao ndogo ndogo.
Hiyo inaonesha wazi
kwamba siasa siyo tu mjadala wa kura na wagombea, bali pia ni chanzo kipya cha
ajira na kipato kwa wanawake.
Fursa mbali mbali za kibiashara zinapatikana katika mikutano ya
kampeni kwa wauzaji wa chakula, mafundi vyarahani, hata kwa wanawake wanaofanya
kazi kwenye sekta za utalii na huduma.
Kwani, wengi wanasema kampeni zimewafungulia milango ya biashara
na kuleta matumaini katika mifuko yao.
Kipindi cha kampeni kila mkutano ni fursa
ya kipato kwani watu hupata kusikiliza sera za wagombea, huku wakiwa na
biashara zao mikobani.
Katika mkutano wa kampeni wa chama cha
Alliance for Democratic Change ADC uliofanyika Mchangamdogo,
mwandishi alikutana na muuza juisi na malai Asha Khamis Sheha mkaazi wa
Gombeume, anasema ni kawaida yake kufanya shughuli zake hizo za biashara katika
mikutano ya kampeni.
‘’Mara
nyingi nakwenda kwenye mikutano ya kampeni kusikiliza sera za wagombea, lakini huwa
nachukua biashara zangu, nashukuru kwa sababu imenisaidia sana kupata pesa za
matumizi,’’ anasema.
Raya Ali Mohamed mkaazi
wa Chake Chake ambae ni mjasiriamali wa kuuza vyakula kama maandazi,
chapati, supu na ugali, anasema kampeni kwake zimekua zimemchanyua kiuchumi
kwani zimekuwa msimu wa mavuno kwake.
‘’Natamani hizi kampeni zisimalize, kwani mauzo ya biashara
zangu yameongezeka, kwa siku nauza mpaka laki 500,000, ambapo kabla ya msimu
huu napata laki mbili ama tatu tu,’’ anasema.
Kutokana na wageni wanaoingia kwa ajili ya shughuli za kampeni, uuzaji
wa bidhaa umeongezeka, hivyo kampeni zimeinua kipato chao kwa asilimia kubwa.
Hamad Omar Othman mkaazi wa Sizini Kijichame mwenye umri wa miaka
25, yeye anauza biashara ya karanga (njugu nyasa) anasema, mikutano ya kampeni ni
fursa kubwa kwake ya kujiinua kiuchumi.
Anasema, tangu zilipoanza harakati za kampeni, ameshauza karanga
za zaidi ya shilindi laki moja, ambapo zamani zilikuwa hazinunuliwi sana.
‘’Sio wanawake pekee wanaonufaika na uuzaji wa bidhaa kwenye
mikutano ya kampeni bali hata sisi pia zinatusaidia kuinua kipato, kwani
biashara zetu zinapata sokola uhakika,’anasema.
Hamad anasema, matumaini yake hata zikimaliza kampeni ni kuwa na
mtaji mkubwa wa kufungua genge, ili aongeze biashara nyengine.
Hadia Faki Juma mkaazi wa Micheweni anasema tangu kuanza kwa kampeni, kazi za ushonaji zinaongezeka mara dufu.
“Kampeni zimekua na baraka kwangu, kwani naletewa matenge nashona
mashati, madira na suruali, imenisaidia kulipa kodi na shida zangu nyengine
najitatulia mwenyewe,” anasema kwa tabasamu.
Hata vijana wanaofanya kazi za kuchapisha mabango, bendera,
mikoba ya wagombea na fulana nao wanasema wanapata kipato kizuri kuliko miezi
mingine ya kawaida.
Khamis Khamis mkaazi wa Chake Chake ambae anachapisha mabango, bendera
na fulana anasema, kampeni imeinua kipato chake, kwani kwa kipindi hiki kazi za
uchapishaji zinaongezeka.
‘’Hata kampeni zikimalizika nategemea kuzikamata zaidi ya
shilingi milioni mbili na fedha hizo nategemea kununua mashine nyengine kubwa
ya kuchapishia, ili biashara iendelee kukua,’’ anasema.
Anasema, kampeni sio tu kwa ajili ya chaguzi bali ina fursa
nyingi, kwani wanawake wengi wameanzisha biashara, hivyo wameondokana na
utegemezi.
SEKTA YA UTALII NAYO
YAFAIDIKA
Mratib wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Pemba Saleh Hamad
Juma anasema, katika kipindi cha kampeni wanajivunia, kwani idadi ya wageni inaongezeka
siku hadi siku na kuingiza kipato.
‘’Kampeni zina faida nyingi, zinachangia uchumi wa wananchi na
Taifa, idadi ya wageni inaongezeka siku hadi siku, hii ni kutokana na amani iliyopo
licha ya kua ni kipindi cha uchaguzi, hii ni fursa ambayo hatujaiona muda
mrefu,’’ anasema.
Anasema, Hoteli zimejaa, migahawa inafanya kazi usiku na mchana,
hivyo wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya malazi na chakula wanapata
kipato kizuri.
‘’Mbali na hayo hivi sasa tumeshapokea barua kwamba Oktoba 27
mwaka huu kuna meli ya wageni zaid ya 300 ambao wanakuja kutembea hapa kwetu
Pemba,’’ anamalizia.
VIONGOZI WA SERIKALI
Mwanaisha Ali Masoud ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto Pemba, anasema Serikali inatoa mikopo kwa wanawake, ili wafanye
biashara kwa ajili ya kuinua kipato chao.
‘’Kuna mikopo maalumu ambayo inaletwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi
ambao unawasidia wanawake kufanya biashara zao ndogo ndogo na kwa sasa wanauza mpaka
kwenye mikutano ya kampeni,’’anasema.
Afisa huyo anafafanua, licha ya hayo bali wanatoa elimu kwa
wanawake juu ya kujikinga na vitendo vya udhalilishaji, ambavyo vinakua
vikijitokeza katika kipindi cha kampeni.
“Kupitia kampeni, tunapata fursa ya kuzungumza na wanawake wengi
wa vijijini, wa mjni, kujikinga na vitendo vinavyochochea vya udhalilishaji,
ikiwemo kuvaa nguo za stara wanapokwenda mikutanoni,’’anasema.
SHUHUDA WA MKOPO
Habiba Jabu Dawa mama wa watoto sita mkaazi wa Sizini Micheweni
Pemba anasema, amepata mkopo wa shilingi laki tano ambapo anatengeneza Juisi,
ubuyu, kachori ambazo anauza dukani kwake na kwenye mikutano ya kampeni.
‘’Uchumi wangu unakua kipindi hichi, kwani biashara zangu
zinatoka zote, soko langu kubwa ni kwenye mikutano hii ya kampeni,’’anasema.
Anasema, hata zikimaliza kampeni anatarajia kuwanunulia watoto wake nguo za skukuu, pamoja na vifaa
vya skuli kama vile sare na viatu.
ZEC
Juma Msanif Sheha Mkuu wa Programu kwa wapiga kura na
msimamizi kutoka Tume
ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) anasema, uchaguzi na kampeni inatoa fursa mbali mbali
kwa wanawake na makundi yote kiujumla.
‘’Tunatoa mafunzo mbali mbali kwa wanawake na kwa wananchi wote
kiujumla, wafahamu haki na wajibu wao katika masuala ya uchaguzi,’’
anafahamisha.
Anasema, watahakikisha wanazingatia usawa wa kijinsia, wakati
watakapota ajira za muda za usimamizi wa uchaguzi, ili kupata uzoefu utakaowasaidia
hata baada ya uchaguzi.
WANAHARAKATI
Amina
Ahmed Mohamed Kaimu Mratib wa Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake (TAMWA)
Zanzibar anakiri kwamba kampeni zina fursa ambazo zinasaidia kuinua uchumi wa
wanawake, ingawa wapo waliokua hawajawa na muamko wa kuzitumia nafasi hizo.
‘’Wapo
wanawake wanaokwenda kusikiliza sera za wagombea huku wakiuza bishara, ambazo
zinawainua kiuchumi, ijapokua bado kuna kundi kubwa ambalo halijafahamu, bali wanakwenda
kwa ajili ya burudani tu,’’anasema.
Anasema,
wamekua wakitoa elimu kwa wanawake wa maeneo ya Pemba kuona wanaitumia fursa
hiyo kwa kuwania nafasi za uongozi, kuhudhuria kwenye kampeni kusikiliza sera,
sambamba na kuuza biashara na kupata pesa za kujiinua kiuchumi.
Mwanaharakati Hafidh
Abdi Said kutoka Jumuia ya PEGAO anasema, kampeni za mwaka huu zinaonyesha
picha mpya ya mwanamke wa Pemba.
“Wanawake sasa si watazamaji tena, wanauza bidhaa, wanapanga shughuli
zote za mikutano, siasa zinawapa kipato na ujasiri,” anasema.
Anaishauri Serikali na vyama vya siasa visiwaache baada ya
uchaguzi, bali viwashirikishe.
“Wakitambuliwa rasmi, hawa wanawake wanaweza kubadili uchumi wa
Pemba kabisa,” anaongeza.
Anaendelea kusema, kampeni za uchaguzi mkuu 2025 zimekuwa zaidi
ya siasa, kwani imekuwa darasa la uchumi kwa wanawake wa Pemba, zinawafunza kuishi
kwa kujitegemea, kushirikiana na kuthamini nafasi yao katika maendeleo.


Comments
Post a Comment