BARAZA LA HABARI TANZANIA (MCT ) LATOA SOMO KWA WANDISHI WA HABARI PEMBA KUELEKEA UCHAGUZI

 


 NA FATMA HAMAD, PEMBA

 BARAZA  la   Habari  Tanzania  (MCT) Ofisi ya Zanzibar , limewataka  Waandishi wa Habari kuzingatia miiko, kanuni na maadili yao wakati wanapoandika habari zao hasa  katika  kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu, ili kuepusha nchi kuingia kwenye migogoro.

 Ametoa nasaha hizo kwa Viongozi wa klabu ya Wandishi wa Habari kisiwani Pemba (PPC), pamoja na baadhi ya wanachama wao Mratibu mstaafu wa Baraza la habari Tanzania Ofisi ya Zanzibar,Bishifaa Said Hassan katika kikao maalumu cha kuwatembelea wanachama wake.

 Alisema kuwa Baraza la habari linajukumu kubwa la kuzungumza na Waandishi wa habari sambamba na kuwakumbusha wajibu wao kwani sauti na kalamu zao zikitumika vibaya vinaweza kupelekea machafuko yasio ya kutegemewa hasa katika kipindi hichi cha kuelekea Uchaguzi mkuu.

 Alieleza kuwa Baraza la habari Tanzania (MCT) Ofisi ya Zanzibar imeamuwa kuwatembelea wanachama wake ikiwemo klabu za waandishi wa habari na kukumbushana wajibu wao kwa vile wao ndio wenye waandishi wengi, sambamba na kumtambulisha Mratibu mpya wa Baraza hilo kwa Zanzibar.

 "Baraza limeamuwa kuwatembelea wanachama wake ikiwemo klabu za waandishi wa habari kwani nyinyi ndio wenye waandishi wengi na habari", alisema.

 Bi Shifaa Said Hassan alisema ni vyema waandishi wa habari kuzingatia maisha yao kwanza, wakati wakiwa katika majukumu yao hasa wanaporipoti habari za uchaguzi Mkuu kwani hakuna thamani ya maisha kama uhai.

 ‘’Ndugu zangu, kuna maisha baada ya uchaguzi, na maisha yenu ndio kitu cha mwanzo kuliko chochote, hivyo ni bora kuwa na tahadhari, mufuate maelekezo muliofundishwa na viongozi wenu wa kati mukiwa kwenye majukumu yenu  kipindi hichi kigumu msijemkafanya masihara,’’aliwanasihi.

 Nae Mratibu mpya wa Baraza hilo kwa upande wa Zanzibar Ziada Kirobo, alisema Baraza la habari ndio mlezi mkubwa wa Vyombo vya habari hivyo ujio wao ni kama wamekuja kuwatembelea watoto wao hivyo aliwataka Viongozi wa klabu kuendelea kuwaweka pamoja wanachama wao na kuwakumbusha wajibu wa kazi zao kila mara.

 Alifahamisha kuwa Waandishi wa habari ni moja ya kundi linaloweza kuipelekea nchi kuingia kwenye migogoro ama kubaki na amani, hivyo ni budi   kuandika habari zenye ukweli na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina ,ili  kuepusha nchi kutumbukia katika migogoro na chanzo kikawa ni waandishi wa habari.

  ‘’Ndugu zangu waandishi wa Habari mjue kwamba masikio, macho na midomo ya wananchi wote yanawaangalia nyinyi, hivyo jitahidini sana kuchunga maadili yenu na kuwa na uzalendo na nchi yenu na maisha ya watu wenu,’’alisema.

 Alisema mara nyingi katika baadhi ya nchi kunapotokezea machafuko sababu zimekua zikitajwa kuwa, ni kutokana na maandiko ya waandishi wa habari, hivyo jiepusheni kuandika habari za uongo na zenye uchochezi, hususan kipindi cha sasa cha uchaguzi mkuu wa 2025.

 Aliwataka waandishi wa habari kuandika habari zenye kuleta maslahi mapana kwa jamii na nchi kwa ujumla kwani wao ni sauti ya wasio na sauti, hivyo ni wajibu wao kuibuwa changamoto mbalimbali zilizopo kwa wananchi na kuzisemea kupitia Vyombo vyao vya habari.

Alisema lengo la ziara hiyo ya kutembelea Jumuia hiyo nakuwapa nasaha hizo ni kutaka waandike habari zisizokuwa na uchochezi, ili kuwafanya wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la uchaguzi kwa amani na utulivu bila woga na hofu yoyote.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Pemba ( PPC) Bakar Mussa Juma aliupongeza uongozi wa MCT kwa kuwapa elimu hiyo wanachama wao, ambayo itasaidia kuwa chachu ya mabadiliko kwao hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi mkuu.

 ‘’Tunawashukuru, tumefurahi sana kwa kuona umuhimu wa kuja na kutukumbusha, kwani kipindi cha uchaguzi sio kipindi cha mchezo, na kalamu za waandishi wa habari ndio zinazonyooshewa vidole pale amani inapotoweka katika maeneo mbali mbali Duniani, '’alisema.

 Alisema wataendelea kuwakaribu na wanachama wao na kuwafundisha kipi waandike na ambacho hakipaswi kuandikwa hasa kwa nyakati hizi, ili kuona Pemba inaendelea  kubaki na tunu yake ya amani, utulivu, na mshikamao.

 Nao baadhi ya wandishi wa habari walioshiriki kikao hicho  walisema wameupokea ugeni huo kwa matumaini, huku wakiahidi kuufanyia kazi ujumbe huo walioupewa sambamba na kuwafikishia wenzao, ili kulinda usalama wa maisha yao, wananchi na Taifa kwa ujumla.

 Baraza la habari Tanzania Ofisi ya Zanzibar,ilitembelea , klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) kuonana na Ofisa Mdhamini Wizara ya habari Pemba, Radio jamii Micheweni na Radio Istiqaama.

 

 

 

 


Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO