WWAANDISHI WA HABARI WAOMBA KUPATIWA TAARIFA SAHIHI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025
Zanzibar-
Sept 28, 2025
Siku ya
haki ya kujua duniani ni siku muhimu hasusan katika kuimarisha ufahamu wa
wananchi na waandishi wa habari kama nguzo kuu za kuimarisha demokrasia,
utawala bora na uwajibikaji ambapo ni vigezo muhimu katika kuleta maendeleo ya
nchi.
Ufanisi wa wananchi na haki yao
ya msingi ya kuweza kufahamu na kujua masuala mbali mbali ambayo yataweza kuimarisha
maisha yao na kuwa na maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.
Siku ya hii kujua
huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 28 Septemba, kwa lengo la kukuza uelewa
kwa wananchi na hata waandishi wa habari juu ya haki hii, kwani imekuwa ni
changamoto kupata taarifa muhimu pale wananchi au waandishi wa habari
wanapohoji masuala mbalimbali ya shughuli za serikali au taasisi za binafsi.
Katika maadhimisho
haya, tunapenda kuangazia umuhimu wa haki hii kama chombo cha kuimarisha
demokrasia na uwajibikaji ambapo kaulimbiu ya mwaka huu.
“Kuwezesha
Upatikanaji wa Taarifa za Mazingira katika Ulimwengu wa Kidijitali.” (“Ensuring
Access to Environmental Information in the Digital Age).
Katika dunia ya leo,
changamoto za kimazingira kama mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa hewa na
maji, uharibifu wa misitu na rasilimali asili zinahitaji wananchi wapate
taarifa kwa haraka na kwa usahihi ili kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya
maendeleo endelevu.
Siku hii haikuja kwa bahati mbaya bali ni muhimu
iliyotambuliwa na kuridhiwa na Umoja wa Mataifa chini ya tamko la haki za
binaadamu la (Universal Declaration of Human Right) mwaka 1948 na Tamko la
Umoja wa Mataifa la Haki za Kisiasa na Kiraia(ICCPR) kama ni sehemu ya uhuru wa
kujieleza kwa jamii.
Tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ni muhimu
kusisitiza nafasi ya haki ya kujua kama msingi wa demokrasia na ianyowapa
wananchi uwezo wa kupata taarifa sahihi, kwa wakati, na kwa uwazi kuhusu
wagombea, vyama vya siasa, sera, taratibu za uchaguzi na matumizi ya rasilimali
za umma kwani bila ya taarifa, wananchi hawawezi kufanya maamuzi sahihi katika
mchakato wa uchaguzi.
Aidha haki ya kujua huwezesha wananchi kufanya maamuzi
sahihi kwa kuzingatia sera na mipango ya wagombea, hupunguza uvumi na taarifa
potofu pia huimarisha uwajibikaji wa vyama vya siasa, wagombea na taasisi za
umma.
Hata hivyo ni lazima tukiri kuwa bado kuna upatikanaji mdogo
wa taarifa muhimu kutoka kwa taasisi za umma na ucheleweshaji wa taarifa rasmi
au utolewaji wa taarifa zisizo kamili na kuenea kwa habari za upotoshaji (fake
news) kupitia mitandao ya kijamii.
Changamoto nyengine
ni ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa taarifa na zaidi kwa waandishi wa
habari kuzingatia habari za matukio na sauti za viongozi na kuacha kuripoti
habari za makundi ya pembezoni na wananchi wa vijijini ambao nao wana nafasi
kubwa katika hatua mbali mbali za uchaguzi.
Hivyo wakati huu wa kuadhimisha siku ya kujua ni muhimu kwa
vyombo na waandishi wa habari kuhakikisha taarifa zinazotolewa ni sahihi, zenye
usawa, uhuru na bila kuwa na upendeleo wa vyama au wagombea.
Ni muhimu kufanyakazi kama walinzi wa demokrasia na
kuimarisha vyanzo tofauti vya habari pamoja na sauti za wasio na sauti ili
lengo la kuwa na siku ya kujua liimarike na kuzingatia makundi yote.
Pia ni muhimu kufahamu kuwa Katiba ya Zanzibar ya 1984 chini
ya Ibara ya 18 ambayo inaeleza haki ya kila mtu kutafuta, kupokea na kutoa
taarifa bila kizuizi, isipokuwa kwa mipaka ya kisheria inayolinda usalama wa
taifa, maadili au haki za wengine sambamba na kanuni za Maadili ya Uchaguzi
Zanzibar zinazohimiza vyombo vya habari na wadau wote kutoa taarifa sahihi, na
Tume kushirikiana na wananchi katika utoaji wa taarifa.
Mambo makuu yanayohusu haki ya wananchi kupata taarifa ndani
ya sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2017 ni:
Kutoa taarifa za uchaguzi: ZEC ina wajibu wa kutoa taarifa
kuhusu uandikishaji wa wapiga kura, maeneo ya kupigia kura, majina ya wagombea
walioteuliwa, na matokeo ya kura.
Uwajibikaji wa ZEC:
Sheria inailazimisha ZEC kuchapisha taarifa muhimu katika Gazeti la Serikali na
vyombo vya habari, ili wananchi wapate ufahamu wa mchakato mzima.
Uangalizi na uwazi:
Sheria inaruhusu wawakilishi wa vyama vya siasa, waangalizi wa uchaguzi na
waandishi wa habari kusimamia baadhi ya hatua za uchaguzi ili kuhakikisha uwazi.
Aidha kwa upande wa
waandishi na Vyombo vya habari pia kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa
taarifa, vitisho kwa waandishi wa habari pamoja na kutokuwepo kwa uhuru wa
uhariri katika vyombo vya habari na kuzingatia habari za matokeo bila ya kuwa na
uchambuzi yakinifu.
Katika muktadha huu ,
Kamati ya Wataalamu wa masuala ya habari Zanzibar (ZAMECO) inasisitiza umuhimu
wa Serikali na Taasisi husika kuzingatia Sheria na Kanuni zinazohakikisha
upatikanaji wa taarifa na Serikali kuimarisha mifumo ya uwazi, kutoa mafunzo
kwa watumishi wa umma, na kuhamasisha jamii kuhusu haki ya kujua.
Kwa waandishi wa habari kuzingatia weledi na umahiri katika
kuleta ufanisi wa kazi zao na kuripoti pale inapotokea vitisho, kuvunjiwa haki
na kudhalilishwa wakati wakiwa katika majukumu yao, Haki ya kujua si chaguo,
bali ni msingi wa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.
Tunatoa wito kwa wadau wote - Serikali, Tume ya Uchaguzi,
Vyombo vya habari, Asasi za kiraia na Wananchi — kushirikiana kuhakikisha kuwa
Uchaguzi Mkuu wa 2025 unafanyika kwa uwazi na wananchi wanapiga kura wakiwa na
taarifa sahihi.
Dkt. Mzuri Issa, Mkurugenzi , TAMWA ZNZ Abdallah Mfaume,
Mwenyekiti, ZPC
.jpg)
Comments
Post a Comment