KISIWAPANZA WALILIA HUDUMA ZA MAMA NA MTOTO

 


                     NA FATMA HAMAD, PEMBA

WANANCHI WA Kisiwapanza wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, wamelalamikia juu ya ukosefu wa huduma za uhakika kwa wajawazito  katika kituo chao cha afya,  jambo linalopelekea kuhatarisha maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Walieleza kuwa katika kituo chao huduma za mama na mtoto bado hazijakua rafiki kwao, kwani kituo  kizima kuna muhudumu mmoja tu ambae anazalisha, na huenda wakati wa mchana tu.

Walisema endapo mzazi atapata tatizo wakati anapokwenda kujifungua kituoni hapo, ama atakapoumwa na uchungu wakati wa usiku hulazimika kuvuushwa baharini na kupelekwa Hospitali kuu ya Abdallah mzee Mkoani, ambapo wengi  hujifungulia ndani ya boti, hali inayopelekea kuhatarisha usalama wa mama na mtoto.

‘’Kituo kizima daktari anaezalisha ni mmoja ivo vifaa vyenyewe navyo havipo vya kutosha, na ikifika jioni anaondoka ikitokezea mjamzito akiumwa usiku inabidi tumtie kwenye kidau ama kiboti tuvuuke nae tumpeleke Abdala mzee, ambapo wengi huzaa humo baharini hawawahi kufika huko Mkoani,’’walieleza.

Wananchi hao walitoa kero hiyo mbele ya mwandishi wa Habari hizi huko kijijini kwao  kisiwapanza,  walisema ingawa kituo cha afya kipo lakini bado huduma za  kujifungulia kwa mama wajawazito bado hazijaridhisha.

 

Khadija Othman Haji ambae ni mmoja wa shuhuda aliepata tatizo wakati wa kujifungua, alisema  kutokana na kukosekana kwa huduma ya uhakika kituoni hapo kulimsababishia kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua, jambo ambalo lilipelekea kukimbizwa katika Hospital kuu ya Abdalla Mzee.

Hivyo kutokana na kadhia hiyo ambayo imekua ikihatarisha maisha yao na vizazi vyao,  ameiomba  serikali kupitia Wizara ya Afya kuwapatia madaktari wa kutosha katika Hospitali hiyo ili wapate huduma ya kujifungulia.

Sheha wa kisiwapanza Haji Ali Shaali amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo  kwa akina mama kujifungulia mbali na kituo hicho.

Alisema tayari ameshachukua hatua ya kufikisha  maombi katika sehemu husika kwa lengo la kupatiwa utatuzi wa changamoto hiyo.

Kwa upande wake Muhudumu wa Afya wa kituo hicho Haroub Makame  ameiomba serikali kuweka kipaombele chao katika Kijiji cha kisiwa panza, sambaba na kuwapatia madaktari wa kudumu ambao ni wazawa wa  shehia hiyo.

‘’Kwa kwaeli wanawake wa kisiwapanza wanateseka, tunaomba serikali ilete madaktari kwa ajili ya kutoa huduma za mama na mtoto, ili kuepusha vifo vitokanavyo na uzazi,’’.

Nae Afisa Mdhamini wizara ya Afya Khamis Bilali   Ali amekiri kuepo kwa tatizo hilo kisiwani humo.

Allisema kisiwa hicho kimo katika mpango wa kujengewa kituo chengine ambacho kitakua kinatoa huduma za mama na mtoto kwa masaa 24.

‘’Tunategemea mwishoni mwa mwaka huu ujenzi wa  kituo chengine ambacho kitakua na madaktari wa kutosha wa huduma za mama na mtoto, ili kuondosha usumbufu huo kwa wananchi hao,’’alisema.

Alisema kituo hicho kitakua na nyumba za madaktari, ambao watalala hapohapo ili huduma za mama na mtoto ziwe zinapatikana kwa wakati wote.

Alisema pia kutakuwepo na Maboti maalumu ya dharura, ambayo yatabeba wajawazito ambao watakua na tatizo la kupelekwa Hospitali kubwa ya Abdala Mzee Mkoani.

Moja ya kipaumbele cha Bajeti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2024/2025, ni kuimarisha miundombinu ya Afya katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya.

Pia moja ya mpango mkakati wa Sera ya Afya Zanzibar Kupanua dhana ya afya ya msingi na kuwa na huduma bora za afya zinazoendana na wakati, endelevu na zinazowafikia wananchi wote.

 


Comments