NA FATMA HAMAD,
Dar-Es-Salaam
ELIMU ya malezi na
makuzi bora ya watoto inahitajika katika jamii ili kuhakikisha wazazi wanalea
watoto wao katika malezi yaliyobora.
Akizungumza na
waandishi wa habari katika Ukumbi wa wa hoteli ya Jamirex jijini Dar-Es-Salaam,
Mtaalamu wa Sayansi ya Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto nchini Tanzania
David Gisuka alisema, kuna baadhi ya wazazi wana tabia ya kushughulikia zaidi
kazi zao na kuwaacha watoto wao wapweke, hali ambayo inawasababishia udumavu wa
akili na kimwili.
Alisema kuwa, watoto
wanahitaji ukaribu wa wazazi wao ili kujifunza mambo mbali mbali ambayo
yatawajenga kiakili, hivyo ni vyema wakatenga muda maalumu kwa ajili ya watoto
wao.
"Mtoto anaanza
kujifunza akiwa tumboni mwa mama yake, hivyo tunatakiwa kuwa karibu nao zaidi
na tuwape malezi bora ili wakue vizuri, hii itamfanya awe imara na mwenye
uwelewa wa hali ya juu," alisema Mtaalamu huyo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa taasisi ya Makuzi na Malezi Bora ya watoto Zanzibar (MECP-Z)
Sharifa Suleiman Majid alieleza kuwa, watoto wanahitaji kutunzwa, kupatiwa lishe bora,
kuwa na afya njema pamoja na kutengenezewa mazingira mazuri ya kuishi.
"Kuna baadhi ya
wazazi hujitia pirika nyingi mpaka wakakosa muda wa kuwashughulikia watoto wao,
jambo ambalo ni hatari katika maisha yao ya baadae kwa sababu mtoto anajifunza
zaidi kuanzia pale mimba inapotungwa hadi miaka mitano kwa asilimia 80, hivyo
iwapo atakosa malezi bora hatokuwa vizuri," alifafanua Mkurugenzi huyo.
Aidha aliwanasihi
wazazi kuwapa watoto wao fursa ya kuzungumza na kuwasikiliza ili wawe huru
kusema chochote kinachowakabili katika maisha yao.
Meneja Huduma za Jamii
(ZPDB) Dk. Ibrahim Byatike Kabole aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu
zao vizuri kwa ajili ya kuwaelimisha wanajamii juu ya umuhimu wa malezi na
makuzi bora ya watoto.
"Tushirikiane
kuhakikisha kila mzazi anapata uelewa wa kutosha kuhusu malezi bora ya watoto,
hili litasaidia watoto kukua vizuri na kuwa na ufahamu wa hali ya juu,"
alisema.
Mapema Mkurugenzi wa
Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenethic Simbaya
alisema, wanahabari wana jukumu la kuielimisha jamii juu ya malezi na matunzo
ya watoto, hivyo wachukue jitihada mbali mbali kuhakikisha kila mmoja
anabadilika na kuwalea watoto wake vizuri.
Mafunzo hayo ya
utangulizi kuhusu -utelekezaji wa Programu Jumuishi ya Zanzibar ya Malezi,
Makuzi na Maendeleo ya Mtoto Zanzibar, yameandaliwa na UTPC kwa kushirikiana na
Zanzibar Presidential Delivery Bureau pamoja na Zanzibar Mult-Sectoral (ECCD)
kwa ufadhili wa Shirika la UNICEF Zanzibar pamoja na Big Win UK.
Comments
Post a Comment