‘’KATIBU MKUU ELIMU ‘’TOENI ELIMU YA MALEZI BORA’’
NA FATMA HAMAD, PEMBA
Katibu mkuu wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis
Abdala Said amewataka wandishi wa habari kuielimisha jamii kufahamu umuhimu wa
malezi na makuzi ya awali ya mtoto, ili kufahamu utaratibu wa kuwalea katika
kipindi hicho, na kupatikana kizazi
chenye afya njema.
Alisema katika
visiwa vya Zanzibar bado kuna tatizo la udumavu kwa watoto kutokana na kukosa huduma muhimu kama vile
Afya, Chakula bora, ulinzi pamoja na ushirikishwaji, hasa katika kipindi cha awali cha
malezi, makuzi na maendeleo ya
mtoto.
Katibu Mkuu
huyo aliyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya siku nne Waandishi Vinara wa ECD
Zanzibar, yaliofanyika Mjini Dar esalam.
Alisema
wandishi wa habari wanajukumu kubwa katika jamii, hivyo ipo haja kuwaelimisha
kufahamu umuhimu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, ili kupata
kizazi chenye madili na afya bora.
‘’Ndugu zangu
wandishi wa habari nyinyi mnadhima kubwa
katika jamii, hivyo ni wakati kuifahamisha ielewe dhana nzima ya malezi, makuzi
na maendeleo ya awali ya mtoto,’’ alisema.
Alisema kwa mujibu wa sayansi ya ECD katika
kipindi cha awali cha siku 2000 ndicho kipindi pekee ambacho mtoto anahitajika kupata huduma hizo,
kwani ndipo akili ya mtoto inatengenezwa,
na anakua na uwezo wa kuchukua kwa haraka chochote atakachokisikia.
Alisema
serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali,
Wizara ya Afya na Wizara ya Maendeleo ya Jamii inaendelea kutoa kipaombele
katika uwekezaji wa awali kwa mtoto, ili kutambua misingi bora ya malezi,
makuzi, na maendeleo ya awali ya mtoto.
Mapema Meneja Huduma za Jamii (ZPDB) Dk Ibrahim Byatike Kabole alisema endapo wandishi wa habari waitumia vyema taaluma walioipata kuwaelimisha Jamii juu ya umuhimu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, tatizo la udumavu kwa watoto litaondoka Zanzibar.
‘’Zanzibar
kuwa na watoto wenye afya bora inawezekana, endapo wandishi wa habari kama mtaitumia vizuri taaluma
mliyoipata,kuwaelimisha wazazi juu ya umuhimu wa malezi, makuzi na
maendeleo ya awali ya mtomto,’’alisema.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Programu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto kutoka UNSEF Alinune Nsemwa, alisema kwa mujibu wa tafiti, katika visiwa vya Zanzibar kuna asilimia 47 tu ya watoto kuanzia miaka miwili hadi chini ya miaka mitano, ndio waliofikia ukamilifu wa ukuaji wao.
Alisema
kutokana na takwimu hiyo ipo haja kwa wandishi wa habari kuhakikisha
wanaielimisha jamii, kufahamu umuhimu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali
ya mtoto, ili kupata kizazi chenye afya bora.
‘’Wandishi
wa habari tuwafahamisheni wazazi, jinsi ya kulea watoto wao katika hatua za
awali za makuzi na malezi bora,’’alisema.
Alisema
wataendelea kushirikiana na serikali ya
Tanzania, ili kuona watoto wote wanaozaliwa ndani ya Nchi hii wanakua salama.
Nao wandishi walioshiriki mafunzo hayo walisema mafunzo yamewasaidia vyema, huku wakiahidi kuyafanyia kazi.
Comments
Post a Comment