SHERIA RAFIKI NI NGUZO MUHIMU KWA WAANDISHI KUFANYA KAZI KWA UFANISI
Na Mwandishi wetu
Kupatikana kwa sheria mpya na
rafiki ya habari visiwani Zanzibar kutasaidia kuweka mazingira bora ya kazi kwa
waandishi wa habari, kwa kuhakikisha ulinzi na ushiriki wao unapatikana kikamilifu
hususan katika kipindi cha uchaguzi.
Akizungumza katika mkutano maalum
ulioandaliwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya
Habari Zanzibar (ZAMECO) huko Tunguu, Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa,
amesema kuwa ni haki ya waandishi wa habari kuwekewa mazingira bora ya kazi.
Alisisitiza kuwa kuwepo kwa sheria rafiki ya habari kutawawezesha waandishi
kufanya kazi kwa uhuru, ufanisi, na kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao.
Amesema kuwa kwa sasa teknolojia
ya habari imekuwa kwa kasi, na idadi ya vyombo vya habari, hususan vya binafsi,
imeongezeka kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, licha ya maendeleo hayo, waandishi
wa habari bado wanalazimika kufanya kazi kwa kutumia sheria zilizotungwa tangu
mwaka 1988, ambazo hazina mlingano na mahitaji ya sasa ya taaluma ya uandishi
wa habari pamoja na mazingira mapya ya kidijitali.
“Sheria zilitungwa kipindi hicho zilikuwa
zinategemea siasa ya ujamaa na kujitegemea ambapo kwa sasa tasnia ya habari
imekuwa kiteknolojia zaidi hivyo ushirikiano wa pamoja kwa mabadiliko
unahitajika”, alisema Dkt Mzuri Issa.
Kwa upande wake Muwakilishi wa Jimbo la Pandani, Profesa Omar Fakih alieleza kuwa mabadiliko ya sheria za vyombo vya habari ni muhimu kwa maendeleo ya tasnia ya habari, hivyo ni vyema kuendelea kusimamia ili mswada uweze kufikishwa Barazani.
“Nilifanya jitihada binafsi
kusaidia mswada kufikishwa Barazani lakini urasimu umechelewesha mchakato huo
kukamilika”, aliongeza Profesa Omar.
Kwa upande wake, Mheshimiwa
Machano Othman, Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, amesema kwamba wajibu wa
Wawakilishi ni kujadili na kuibua masuala yanayogusa maisha ya wananchi. Aidha,
amebainisha kuwa waandishi wa habari wana haki ya kudai sheria mpya ya habari
kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta hiyo, ili kuhakikisha upatikanaji
wa sheria iliyo rafiki na inayozingatia maslahi ya pande zote.
Kwa upande wao, Wajumbe wa ZAMECO
wameeleza masikitiko yao kuhusu kucheleweshwa kwa kupatikana kwa sheria mpya ya
habari Zanzibar, ambayo wamekuwa wakiidai kwa takriban miaka 20 sasa. Wamesema
kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha waandishi wa habari kushiriki katika
chaguzi kuu bila kuwepo kwa sheria madhubuti itakayolinda haki na wajibu wao
wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Mkutano huo umeandaliwa na
TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar
(ZAMECO), kwa lengo la kuendeleza juhudi za utetezi na uchechemuzi wa
kupatikana kwa sheria mpya na rafiki ya habari visiwani Zanzibar.



Comments
Post a Comment