Mdhamini Sheria ; ‘’Wasaidizi wa Sheria ifahamisheni jamii viashiria vinavyosababisha udhalilishaji’’.

 


                   Na Fatma Hamad, Pemba

AFISA MDHAMINI wizara ya Katiba Sheria na Utawala bora Halima Khamis Ali amewahimiza watoa msaada wa kisheria kuielimisha jamii, kufahamu mbinu za kuzuia vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, ambavyo vinaonekana kujitokeza siku hadi siku, ili waweze kujiepusha navyo

Mdhamini huyo aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo watoa msaada wa kisheria juu kujikinga na vitendo vya udhalilishaji yaliofanyika ukumbi wa Katiba na Sheria Gombani Chakechake Pemba.

Alisema vitendo vya udhalilisha bado vinaendelea kujitokeza na kuiathiri jamii, hivyo watoa msaada wanadhima kubwa ya kuwafahamisha wanajamii jinsi ya kujizuia na vitendo hivyo, ambavyo vimekua vikiwakosesha amani.

‘’Hata ukimshauri, ukimuelimisha aliepata hayo matatizo basi kunahitaji utaalamu, hivyo basi tuendeleeni kuisaidia jamii yetu ili kupata kizazi kilichosalama,’’alisema.

 Aidha aliwasisitiza watoa msada hao kuyafanyia kazi mafunzo hayo, kuhakikisha wanawajenga wanajamii, ili waweze kuleta mabadiliko  juu ya masuala hayo.

Alisema ipo haja kwa wasaidizi wa Sheria kuhakikisha wanazingatia takwimu katika ripoti zao, jambo ambalo litasaidia kujulikana ni kundigani zaidi ambalo limekua likiathirika na udhalilishaji.

‘’Takwimu ndio kila kitu mtakapoweka katika ripoti zenu, mfano wanawake wangapi, watoto wangapi au wanaume wangapi itaweza kujulikana shida ipo wapi na ikaweza kufanyiwa kazi ,’alifahamisha.

Mapema Mkurugenzi kutoka Idara ya Katiba na  Msaada wa kisheria Zanziba Hanifa Said Ramadhan alisema Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watoa msaada waweze, kuisaidia jamii iweze kuchukua hatua za makusudi juu ya kujikinga na kujiepusha na  udhalilishaji.

‘’Tunawapa mafunzo haya ili wakaisaidie jamii kufahamu viashiria vyinavyopelekea udhalilishaji, ili waweze kupambana navyo,’’alisema.

Alisema kinga ni bora kuliko tiba, hivyo ipo haja wananchi kupatiwa elimu ya kufahamu viashiria ambavyo vinaweza kupelekea kutokea kwa vitendo vya udhalilishaji, katika maeneo yao wanayoishi.

Akiwasilisha mada juu ya hatua ya kuzuia vitendo vya udhalilishaji Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Juma Ali Juma alisema ili kuhakikisha matendo hayo yameondoka ni lazima kurejeshwa kwa malezi ya pamoja, na isiwe kwa kila mzazi na mtoto wake.

‘’Endapo tutarudisha malezi ya zamani mtoto akilelewa na kila mzazi tunaweza tukafika tutakapo,’’alieleza. 

Nao washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo waliyoyapata, na kuhakikisha wameleta mabadiliko katika Shehia zao.

Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo watoa msaada hao wa kisheria kupitia mradi wa Shirika la UN Wemen ni muendelezo wa mafunzo ambayo hupatiwa wasaidizi wa Sheria kila baada ya muda.



Comments

Popular posts from this blog

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO

‘’KATIBU MKUU ELIMU ‘’TOENI ELIMU YA MALEZI BORA’’