WANASIASA WANAOGOPA KUTUMIA UHURU WA KUJIELEZA
NA
FATMA HAMAD-PEMBA
Kila
Raia ana haki ya kutoa maoni na kuwa na uhuru wa kujieleza
Kifungu cha 18 (1) cha Katiba ya Zanzibar
ya mwaka 1984 kinaeleza kuwa ‘’Bila ya kuathiri Sheria za nchi, kila mtu yuko
huru kuwa na maoni na mawasiliano yake bila kuingiliwa kati.”
Na hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 42 inaeleza kwamba, kila mtu anastahili kuwa
huru bila kuathiri sheria za nchi.
Kwa Zanzibar viongozi wa vyama vya siasa
wanasema, wamekua wakikosa kutumia uhuru wao wa kujieleza, licha ya kuwa ni
haki yao kikatiba.
Hivyo basi, makala hii imezungumza na
wadau mbali mbali pamoja na wanasiasa
ili kufahamu ni kwa nini wanasiasa wanaogopa kutumia uhuru wao wa
kujieleza.
WANASIASA
Maryam Nassor Juma ambae ni Katibu wa
Chama cha Chauma mkaazi wa Vitongoji Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba anasema,
wanaogopa kutumia uhuru wao wa kujieleza kutokana na mifumo pamoja na sheria
zilizopo za habari pamoja na za uchaguzi
zinaminya uhuru wao.
Anasema,
wamekua wakikosa ushirikiano na hata kwa waandishi wa habari kutoa kero zao,
kwani hata kwani hata nahao wandishi wenyewe wanaogopa kwa sababu Sheria zilizopo za Habari zinawanyima uhuru.
‘’Hata
ukiangalia kwenye mikutano ya kampeni, waandishi wa habari wengi wanaripoti
habari za chama tawala tu, lakini kwa nini hawaripoti habari za kwenye vyama
vya upinzani, hivyo ni wazi kwamba uhuru haupo,’’ anaeleza.
Anasema
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, walikatwa matokeo yao na walipojaribu
kuwatafuta waandishi wa habari ili wawaelezee malamiko yao, walikosa
ushirikiano, hivyo inaonesha wazi kwamba na wao wanaogopa.
Anaeleza,
kwa mujibu wa kifungu cha 127 cha Sheria ya kufuta Sheria ya Uchaguzi Namba 11
ya mwaka 1984 na kutunga Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2017 na mambo mengine
yanayohusiana nayo, kinanyima uhuru wao.
Kwa
sababu kifungu hicho kinaeleza kwamba ‘’ni marufuku chama cha siasa, kutangaza
matokeo ya uchaguzi kwa njia yoyote ya mawasiliano kabla ya matokeo ya uchaguzi
kutangazwa rasmi na Tume ya uchaguzi.
Au
kuitaka Tume itangaze matokeo ya uchaguzi kabla ya muda uliowekwa kumalizika,
atakua ametenda kosa na akitiwa hatiani adhabu yake ni chini ya shilingi
milioni mia moja’’.
Mohamed Haji Kombo ni Katibu wa Chama cha Wananchi CUF
Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba anasema, uhuru
wa kujieleza kwa vyama vya siasa upo, isipokua utekelezaji tu, haupo.
‘’Hatukamatwi,
hatugombwi, ila hayo tunayoyasema hayapokelewi vizuri na wala hayatekelezwi,
kwa hiyo wakati mwingine tunakaa kimya tu,’’ anaeleza.
Katibu
wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Chake Chake kichama Saleh Nassor Juma
anasema, wanaogopa kutumia uhuru wao wa kujieleza, kwa sasbabu haupo.
Anasema,
licha ya kuwa uhuru wa kujieleza kikatiba umetajwa kwamba, ni haki ya kila
Mzanzibari, ingawa bado kwenye vyama vya siasa hakuna uhuru wa kuzungumza, kwa
sababu hata unapojaribu kutafuta vyombo vya
habari, ili kuelezea kero zako basi hazitolewi hewani, hususani kwa
upande wa vyama vya upinzani.
‘’Kwakweli
sisi vyama vya siasa hususani vya upinzani hatuna uhuru wa kujieleza, kwani
tunapokua na malalamiko yetu wandishi wa habari hawatoi kwenye vyombo vyao, na
atakae jaribu kuzitoa anaweza akaingia kwenye matatizo, ama chombo chake
kinaweza kufungiwa,’’anasema.
Anaendelea
kufafanua, siku zote unapojaribu kuzungumza kitu kinachukuliwa vibaya,
unajikuta unaingia mashakani na kuambiwa ni mchochezi na unaikosoa Serikali.
Kwa
mfano mwaka 2001 anasema aliwekwa ndani kwa sababu aliambiwa
ameshawishi wafuasi wa chama chake
kufanya mandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.
‘’Nilishawekwa
ndani mara kadhaa, ikiwemo mwaka 2001
kwa sababu tu, tulifanya mandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2000, tukaonekana kama ni wachochezi na tumeikosoa Serikali,’’anasema.
Anaendelea
kusema kuwa, alifukuzwa kazi, kwani katika uchaguzi wa mwaka 1990 walilalamika
na kudai kwamba wanahitaji kuwapo uchaguzi utakaoshirikisha vyama vingi na sio
wa chama kimoja.
‘’Mimi
na wenzangu kadhaa tulifukuzwa kazi kwa sababu tu tulidai kuwapo na mfumo wa
vyama vingi,’’ anaeleza.
Khamis
Omar Juma Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini
Pemba anasema uhuru wa kujieleza kwa vyama vya siasa upo.
Anasema,
viongozi wote wa vyama vya siasa wamekua wakizungumza kero zao na kutoa malalamiko
yao bila ya woga wowote.
‘’Kwa kweli uhuru tunao na tunazunguza kila
ambalo tunaona linatukwaza, na wala hatupati tatizo lolote,’’ anasema.
WANANCHI
Batuli
Mussa Sharif mkaazi wa Micheweni anasema, vyama vya siasa bado havina uhuru wa
kutosha wa kutoa maoni yao, kwa sababu wanapozungumza jambo ijapokua lina
maslahi kwa jamii wanaonekana wanataka kuleta vurugu, hususani vyama vya
upinzani.
Anasema
siku zote wamekua wakishuhudia matukio
kadhaa ambayo huwatokea viongozi wa vyama vya siasa, wakati wanapozungumzia
kero zao.
‘’Kwa
kweli wanasiasa uhuru wao wa kujieleza ni mdogo, hivyo ipo haja ya kuwekwa
mifumo rafiki, ili kuona kila kiongozi wa chama chochote ana uhuru wa kutumia
haki yake ya kikatiba ya kuwa na uhuru wa kujieleza bila kikwazo,’’ anaeleza.
Mohamed
Khalfan mwananchi kutoka Mkoani Pemba anasema, vyama vya siasa vinaogopa
kutumia uhuru wao wa kujieleza kwani bado huo uhuru wenyewe wa kujieleza haupo,
yawezekana upo katika maandishi, lakini kihalisia haupo.
‘’Kwa
kweli vyama vya siasa bado havipati kutumia uhuru wao wa kujieleza, ni vyema
kungewekwa mifumo ambayo haingilii uhuru wao,’’ anaeleza.
MWANASHERIA
Khalfan
Amour Mohamed Mwanasheria wa kujitegemea kutoka kisiwani Pemba anasema,
wanachama wa vyama vya siasa wanaogopa kutumia uhuru wao wa kujieleza kwa
sababu mifumo iliyopo bado inawakwaza.
Anasema,
ndio maana wanawake wengi walio na elimu zao hawagombei nafasi za uongozi, kwa
sababu wanaogopa, hali ambayo wanapokuwa wanasiasa hukosa uhuru na wakati
mwingine wanaweza kukosa fursa za maendeleo.
‘’Vyama
vya siasa vinaogopa kutumia uhuru wao wa kujieleza, kwani ukijaribu kuzungumza
kitu chenye maslahi ya jamii na ikiwa kimewagusa watu wakubwa utakuta umeingia
kwenye matatizo,’’ anasema.
Anasema,
ipo haja kubadilishwa kwa mifumo iliyopo pamoja na Sheria mbali mbali zikiwamo
Sheria za Habari, ili kuona kila mmoja anapata uhuru wake wa kujieleza kama
Katiba ilivyoeleza.
WANAHARAKATI
Salim
Said Salim ambae ni Mjumbe kutoka Tasisi ya
Watalamu wa Masuala ya Habari Zanziba (ZAMECO) anasema, bado vyama vya
siasa havijakua na uhuru wa kueleza mambo yao hususan kwa upande wa vyama vya
upinzani.
Anasema,
uhuru wa kujieleza kwa vyama vya siasa haupo kwani inaweza ikatokezea vyama vyengine
vikaruhusiwa kufanya maandamano ya amani, ingawa baadhi ya vyama vikazuiliwa,
na vyombo vya habari vikashindwa kuripoti kwa kuhofia nawao kuingia matatizoni.
‘’Bado
mifumo pamoja na Sheria zilizopo za Habari
hazijawapa uhuru baadhi ya vyama vya siasa, bali zinawanyima,’’ anasema
Anasema
kama vyombo vya habari vinaaminika
kwanini wandishi wa habari wasiruhusiwe kuripoti matokeo ya uchaguzi
ambayo tayari yameshapachikwa kiambazani hadi mpaka isubiriwe tume itangaze.
Anasema,
ingekua Sheria zilizopo ikiwamo ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na
Vitabu nambari 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Nambari 8 ya
mwaka 1997 , wangeweza kuvitumia vyombo
mbali mbali vya habari kuzungumzia kero zao.
Anasema
ingelikuwa Sheria hizo ni rafiki kwao wangeweza kuondokana na malalamiko, kwani
wangetumia vyombo vya habari kuzungumza
matatizo yao yanayowakwaza, na yakaweze kusikika na mamlaka husika.
Anasema,
ni vyema Serikali ikabadilisha baadhi ya vifungu vilivyomo katika Sheria hiyo
ambayo vinanyima upatikanaji wa uhuru wa wanahabari pamoja na vyama vyote vya
siasa, na kuweka vyengine ambavyo vitatoa uhuru kwa wote,
Chama
cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA), imekua mstari wa
mbele kupigia kelele sheria zenye mapungufu hasa zinazogusa tasnia ya Habari
ziboreshwe, ili kuhakikisha kila raia anapata haki yake ya kuwa na uhuru wa
kujieleza.
‘’Tutahakikisha
tunapaza sauti zetu juu ya Sheria hizi za Habari na ambazo zinagusa tasnia hiyo,
ili tuhakikishe tunapata Sheria mpya na rafiki, ambazo zitawafanya wandishi wa
habari waweze kutekeleza majukumu yao wakiwa na amani na bila ya hofu yoyote,’’
Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar Mzuri Issa
Ali anaeleza.
NINI KIFANYIKE
Ipo
haja ya kurekebishwa kwa baadhi ya sheria kama vile Sheria za Uchaguzi, Sheria
za Habari pamoja na mifumo iliyopo, ili kuona kila mtu anapata haki yake ya
msingi ya kujieleza kama ilivyoeleza Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Comments
Post a Comment