Ndoto ya kupata Sheria Mpya ya Habari Zanzibar mwaka huu yazimika
Na Fatma Hamad, Pemba
SIKU ya Uhuru wa
Habari Duniani ni siku inayotambuliwa ulimwenguni kote kwa sababu ya umuhimu
wake. Kwa kuwa uhuru wa Habari ni haki ya msingi kwa binadamu wote na ndioyo
maana Umoja wa Mataifa ukaitangaza Mei 3 ya kila mwaka kuwa ni siku ya Uhuru wa
Habari.
Kwa watetezi wa
haki za binadamu. Wanahabari na wadau wa habari huiadhimisha siku hii katika
mwezi mzima wa Mei kwa kutafakari, kujadili na kutathmini uhuru wa habari
ulivyo katika eneo husika.
Kama ilivyo kwa
mataifa mengine waandishi wa habari Tanzania Zanzibar huadhimisha siku hiyo kwa
kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutathmini na kuchochea uwapo wa
uhuru wa habari nchini.
Makala hii
iliyoandaliwa na waandishi wa habari Kisiwani Pemba imebeba dhima ya kufanya
uchechemuzi ili kupata Sheria Mpya ya Habari ya Zanzibar ili uhuru wa habari
ulindwe na utekelezwe kama unavyoainishwa katika mikataba mbalimbali ya
kimataifa na kikanda.
Akizungumza na
Makala hii, Rehema Ramadhan Said amesema umefika wakati kwa waandishi wa habari
na wadau wengine wa habari kuwa na sheria rafiki ambazo zitakuwa ni msaada kwao
wakati wanapotekeleza majukumu yao.
“Tupo katika
ulimwengu wenye mabadiliko makubwa kihabari, hivyo tunapaswa kuwa na sheria
mpya ambayo itaendana na mazingira ya ukuaji wa teknolijia ya Habari,” anasema.
Naye Khadija
Rashid Nassor akizungumzia suala la kukosekana sheria rafiki kwa waandishi wa
habari ameshauri mamlaka husika kuharakisha kuupeleka mswada wa sheria mpya ya
habari ili ujadiliwe na kuwawezesha kupata uhuru wa kutumia taaluma yao
kuihabarisha jamii.
“Hofu ya kuweza
kufungiwa chombo cha habari au kukamatwa mwandishi wa habari ni moja ya sababu
zinazowafanya waandishi wa habari kufanya kazi kwa woga, lakini iwapo sheria
hii mpya itapishwa itakuwa mwarubaini wa haya yote,” anasema.
Wadau wa habari
nao wamekuwa wakiipigia chapuo sheria mpya na rafiki ya habari ipitishwe
wakiamini kwamba itawawezesha kupata taarifa zilizochakatwa kwa ufanisi na
zilizojaa maudhui tarajiwa.
“Mimi ni mdau
mkubwa na mfuatiliaji wa taarifa za habari, kwa kweli imefika wakati nakosa
kupata taarifa za uchunguzi zenye kuweza kuleta mabadiliko chanya, kwa sasa
kila ukisoma taarifa ni za matukio tu,” anasema.
Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amesikika akisema kuna mpango
wa kuifanyia marekebisho sheria ya habari, lakini ni kama vile kauli hizo
zimekuwa za kisiasa.
“Tunategemea sana
katika kikao cha bajeti cha Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Makamu wa Pili wa
Rais tunatarajia kuisoma na kuipitisha sheria ya habari ili nasi Zanzibar tuwe
na sheria mpya na rafiki kwa waandishi wa Habari.” Hiyo ndiyo ahadi aliyoitoa
Waziri Tabia mwanzoni mwa Aprili mwaka huu wakati wa Kikao Kazi cha Maafisa
Habari wa Serikali kilichofanyika Amani Complex mjini Unguja.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamesema kuwepo kwa sheria mpya na rafiki ya habari haitaleta faida kwa waandishi wa habari bali itakuwa ni ukombozi wa wadau wote wa masuala ya habari.
Mariam Saleh Juma
kutoka Chama Cha Umma, akizungumza na Makala hii amesema kuwapo kwa sheria mpya
itasaidia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa weledi na bila woga.
“Waandishi wa
habari kwa sasa najua kwamba mnashindwa kuwa huru kuandika na kutangaza baadhi
ya matukio ya kisiasa kutoka vyama vyote vya siasa, hivyo tunashauri sheria
ipitishwe ili kukuza demokrasia nchini,” anasema.
Naye Katibu wa
Idara ya itikadi na Uenezi wa CCM Jimbo la Micheweni Salim Jabu anasema
zipo sheria ambazo ni kikwazo kwa waandishi wa habari, ambazo zinahitaji
kufanyiwa marekebisho ili ziendane na wakati wa sasa.
Katibu wa ACT
Mkoa wa Chake Chake Saleh Nassor Juma, ameshauri mamlaka husika kuharakisha
kuipitisha sheria mpya ya habari ili kuwafanya waandishi na wadau wengine wa habari
kuwa huru kutekeleza majukumu yao.
Amefahamisha
mwarubaini wa changamoto zinazokwamisha uhuru wa habari na zinaweza kumalizwa
na uwepo wa sheria mpya ambayo itakuwa rafiki na yenye kuleta tija kwa
waandishi na wadau wa habari,
“Nina imani
waandishi wa habari muda sio mrefu mtapata sheria mpya ambayo itakuwa rafiki
katika utendaji kazi wenu, hivi juzi nilimsikia waziri mwenye dhamana ya habari
akitoa tamko la kupitishwa sheria mpya kwenye mkutano wa maafisa habari wa
serikali,” anafahamisha.
Si waandishi wa
habari pekee wanaohitaji kuwapo kwa sheria mpya na rafiki ya habari visiwani
Zanzibar bali hata wadau wa habari wakiwamo wana harakati na watetezi wa haki
za binadamu n ahata wananchi kwa sababu kupata Habari na kutoa maoni yao ni
miongoni mwa haki zao za msingi.
Akitoa taarifa
kwa waandishi wa habari Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Raya Issa
Msellem, amesema katika kikao cha 10 cha Baraza la Wawakilishi , mkutano wa 19,
Baraza litajadiliwa miswada miwili ambayo ni Muswada wa Sheria ya Fedha ya
mwaka 2025 – 2026 na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya mwaka 2025-2026.
Taarifa hiyo
inazima ndoto za waandishi wa habari na wadau wa habari visiwani Zanzibar ya
kupata Sheria Mpya ya Habari ambayo ni rafiki na itakayo wawezesha kufanya kazi
zao kwa uhuru na weledi.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania Zanzibar (TAMWA), imekua mstari wa mbele kupigia kelele sheria zenye
mapungufu hasa zinazogusa tasnia ya Habari ziboreshwe, ili kuhakikisha kila
raia anapata haki yake ya kuwa na uhuru wa kujieleza.
‘’Tutahakikisha tunapaza sauti zetu juu
ya Sheria hizi za Habari na ambazo zinagusa tasnia hiyo, ili tuhakikishe
tunapata Sheria mpya na rafiki, ambazo zitawafanya wandishi wa habari waweze
kutekeleza majukumu yao wakiwa na amani na bila ya hofu yoyote,’’ Mkurugenzi wa
TAMWA Zanzibar Mzuri Issa Ali ameleza.




Comments
Post a Comment