WAKULIMA BADO WALIA NA BEI NDOGO YA MWANI

NA FATMA HAMAD, PEMBA

WANAKIKUNDI CHA TUMAINI kilichopo shehia ya Michenzani Mkoani Pemba ambacho kinajishughulisha na ukulima wa  kilimo  cha Mwani,  wametupa kilio chao kwa  Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar  kuwangalia  tena   kwa jicho  la  huruma, kwa  kuongeza  bei  ya  mwani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi  mwanakikundi Biwanu Ngwali Faki  alisema bei ya mwani ya kilo shilingi miasaba (700)  ni ndogo, ukilinganisha na gharama wanazozitoa wakati wa kulima.

Alisema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya awamu ya Nane ni kuwaimarisha wakulima wa Mwani kichumi, hivyo ni wakati kuongeza bei hadi shilingi 2000.

 ‘’Kwaweli bei ya shilingi miasaba inatuumiza kazi ni ngumu, ukiangalia Tunanunua Kamba pamoja na taitai kwa gharama kubwa,hivyo tunaiomba Serikali ituengezee bei, ifike angalau elfu 2000,’’ alisema.

Kwa upande wake mwanakikundi Kazija Ali Bakar  alisema  bado wakulima wa mwani hawajanufadika na zao hilo, kwani kilimo hicho kina changamoto nyingi.

 ‘’Kiukweli hasa tusifichane wanaonufaika na zao la mwani ni makampuni yanayo nunua mwani na sio wakulima,  wakulima tunaishia kunyanyasika na kuumia tu,’’ alieleza.

Katibu wa kikundi hicho Zakia Omar Ngwali alisema  asilimia 80 ya wakaazi wa Shehia hiyo wanategemea kilimo cha mwani kuendesha maisha yao, hivyo ipo haja kwa  Serikali  kufikiria kuongeza bei.

Aidha alisema wanakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa vitendea kazi ikiwemo Boti za kuchukulia mwani.

‘’Tunasikia tu kama kuna boti za mkopo ila sisi hatujazipa, hivyo tunawaomba wahusika watufanyie msada na sisi watupatie tunateseka,’’alieleza.


Mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Mwani ya Serikali [ZASCO] Masoud Rashid Mohamed alisema kuwa bei ya mwani itaongezeka  mara baada ya kumalizika  ujenzi wa kiwanda cha mwani Chamanangwe.

Alisema  wanatarajia katika mwaka huu wa 2025  kiwanda hicho kitanza uzalishaji wa bidhaa  zinazotokana na mwani, hivyo wakulima watapata fursa ya kuuza bidhaa hiyo kwa bei nzuri.

Alisema  kiwanda hicho kitakua na uwezo wa kuchakata  tani zaidi 30,000 za mwani kwa mwaka, hivyo waendelea kuvumilia.



 

 

Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO