WADAU WALIA NA SHERIA ZINAZOKWAZA HAKI YA KUPATA HABARI
NA FATMA HAMAD - PEMBA
Baada
ya kilio cha muda mrefu waandishi wa habari visiwani Zanzibar wana matumaini makubwa juu ya kupata sheria
mpya za habari ambazo hazina vikwazo kwao na zinazoendana na mazingira ya sasa.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika hotuba zake kadhaa
amekua akizungumzia changamoto ambazo zimekua zikiikabili tasnia ya habari na
kuahidi kuzitatua changamoto hizo, ili kuona vyombo vya habari vinatekeleza
majukumu yake vikiwa huru.
‘’Tunatambua
changamoto zinazovikabili vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari,
hivyo Serikali itafanya kila jitihada kuviwezesha, ili kuona wandishi wa habari
wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi,’’alisema Rais Mwinyi
Dokta
Mwinyi katika miaka minne ya uongozi wake amekua ni kiongozi wa
mwanzo na wa mfano katika nchi hii kukutana mara kwa mara na waandishi
wa habari Visiwani Zanzibar, amebeba matumaini makubwa ya wadau wa habari
pamoja na wananchi wenye kuheshimu uhuru wa habari na haki ya kupata habari.
Bila shaka
kufanya hivyo kumempa nafasi kubwa ya kusikiliza moja kwa moja vikwazo
vinavyowakumba wandishi wa habari pamoja na vyombo vya habari hapa Zanzibar
katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kutokana na hayo waandishi
wa habari ambao ndio watafutaji na wasambazaji habari wamekua na kiu na shauku
kubwa ya kurekebishwa vifungu
vilivyomo katika Sheria za Habari
ambavyo vitawafanya wawe huru, ili waweze kutekeleza majukumu yao bila woga wala
hofu yoyote, kwani ni
muda wamekua wakipaza sauti zao ili kuona vifungu hivyo vinaboreshwa.
WAANDISHI WA HABARI
Mwandishi
wa habari mkongwe Mohamed Khalfan kutoka kisiwani Pemba anasema vyombo vya
habari vina wajibu wa kutoa taarifa mbalimbali kwa lengo la kuuhabarisha umma
juu ya mambo yanayohusu nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Anasema
ili waandishi waweze kufanya kazi zao bila ya hofu na woga, ipo haja ya kuwapo kwa sheria
zinazotoa uhuru na fursa pana kwa wanahabari katika kutafuta, kuchakata na
kusambaza habari bila ya kuwapo vikwazo vinavyotokana na sheria nyingine ambazo
zinapingana na sheria mama ambayo ni Katiba ya nchi.
‘’Waandishi
wana hofu ya kutumia uhuru wao wa kujieleza, hivyo ni vyema
kuwapo na Sheria ambazo ni rafiki kwao na ambazo zinatoa uhuru, ili waweze
kutekeleza majukumu yao bila hofu
yoyote,’’anasema.
Mwandishi
wa habari na Mhariri wa Mtandao wa Pemba Today Haji Nassor Mohamed anasema
waandishi wa habari wamekua na hofu ya kutumia uhuru wao wa kujieleza kwani
katika Sheria zilizopo bado kuna vifungu kadhaa vimekua ni kikwazo, na ni
kandamizi ambavyo vinanyima uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza.
‘’Baadhi
ya sheria zinazosimamia sekta ya habari na nyingine ambazo zinaigusa sekta hiyo
zinazuia mtiririko mzuri wa utafutaji na usambazaji wa habari, ambapo ni
kinyume na kifungu cha 18 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ambacho kinasema mwananchi kutafuta na kupata habari
bila mipaka,’’ anasema.
Anasema
kifungu namba18 (1) na (2) vinaeleza kuwa kila mwananchi amepewa uhuru wa
kutafuta, kupokea na kusambaza habari bila ya vikwazo wala mipaka, ingawa bado
zipo Sheria zinazoweka mipaka, jambo ambalo huwa ni kikwazo katika mchakato wa
upashanaji habari.
Anasema
miongoni mwa vifungu ambavyo vinanyima uhuru wa habari ni kifungu cha 123 cha
sheria ya kufuta Sheria ya Uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984 na kutunga sheria ya
mwaka 2017, ambacho kinanyima fursa ya
waadhishi wa habari kufuatilia harakati za uchaguzi hasa wakati wa kupiga na
kuhesabu kura.
Anaendelea
kusema katika sheria hiyo kuna vifungu ambavyo vimempa mamlaka Afisa Dhamana wa
Uchaguzi kumnyima kitambulisho mwandishi
wa habari, jambo ambalo linaweza kupelekea Afisa huyo kutumia mamlaka yake
vibaya kwa kuwakandamiza wanahabari hivyo kukwaza haki ya wanachi kupata habari
za kweli kuhusu uchaguzi.
‘’Vifungu
hivyo vinatuonesha kwamba hakuna umuhimu
wowote wa kuwepo na waandishi wa habari hapa nchini ,’’
Pia
anasema katika sheria hiyo kuna vifungu ambavyo vimetoa adhabu kubwa ikiwemo ya
kifungo na faini au vyote viwili kwa pamoja kwa
mwandishi atakayekutikana na makosa yaliyoainishwa na sheria hiyo.
‘’Siyo
vizuri kwa ulimwengu wetu huu ambao unahimiza haki, usawa na uwajibikaji,
kuwapo vizingiti (vikwazo) ambavyo katika baadhi ya nchi kama vile Kenya na Nigeria waandishi wa
habari (vyombo vya habari) hutoa matokeo ya uchaguzi baada ya kupata matokeo yaliyotangazwa na mamlaka husika kwenye
majimbo,’’ anasema.
Naye mwandishi wa habari mwandamizi Mchanga Haroub Shehe anasema kutokana na kuwapo kwa vifungu hivyo ambavyo ni kandamizi vinasababisha waandishi wa habari kuwa na mazingira magumu ya kutekeleza majukumu yao.
Anasema
ipo haja kwa waandishi wa habari kuhakikisha wanakua na fursa pamoja na elimu
ya jinsi ya kuripoti masuala ya uchaguzi.
‘’Kama
vifungu hivyo havijaangaliwa na kurekebishwa bado itaendelea kuwaweka katika
wakati mgumu waandishi wa habari hasa katika kipindi cha uchaguzi,’ ’anamalizia
Bi Mchanga.
WANANCHI
Juma
Kombo Hamad mkaazi wa Micheweni anasema endapo waandishi wa habari hawatokua
huru hakutoathiri wao peke yao, bali hata jamii itaathirika kwani itakosa
kupata taarifa za matukio ambayo yanatokezea nchini.
‘’Waandishi
wa habari ni watu muhimu katika nchi, hivyo kama watakua na hofu na hawatokua
na uhuru wa kutekeleza majukumu yao, sio rahisi kupatikana kwa
maendeleo,’’anasema.
Asha
Omar Said mkaazi wa Machomane Chakechake Pemba anasema kutokana na kuwapo kwa
Sheria za Habari ambazo zinawanyima waandishi wa habari uhuru wao wa kujieleza,
ipo haja mamlaka zinazoshughulikia masuala ya kisheria kuhakikisha zinafanyiwa
marekebisho ili kuhakikisha waandishi wa habari wanatekeleza majukumu yao
wakiwa huru na bila ya khofu yoyote.
WANAHARAKATI
Salim
Said Salim mjumbe kutoka Tasisi ya Zameco Zanzibar anasema kuwapo kwa uhuru wa
habari ni jambo muhimu kwani inasaidia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa maendeleo
nchini.
Anasema
endapo kutakuwa na sheria ambazo zinabana uhuru wa habari husababisha kosekana
kwa maendeleo ya wananchi.
‘’Kwanini
waandishi wa habari wasiruhusiwe kupiga picha au kutangaza matokeo ya uchaguzi
ambayo tayari yameshapachikwa kiambazani,’’ anasema.
Mwenyekiti
wa Klabu ya Waandishi wa Habari kisiwani Pemba Bakar Mussa Juma anasema katika kipindi cha Uchaguzi waandishi
wa habari walio wengi hukutana na mazingira magumu, licha ya kutekeleza
majukumu yao kwa misingi ya kisheria.
Anasema
ipo haja ya mamlaka husika kuona umuhimu
wa kuvifanyia marekebisho vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari na kusababisha
waandishi wa habari kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, na kuendelea
kuwaweka katika mazingira magumu kipindi cha chaguzi.
‘’Siyo
jambo zuri mwandishi ashindwe kupata
taarifa za matokeo mpaka
yatangazwe na Tume ya Uchaguzi, hii ni kuidumaza tasnia ya habari,’’ anaeleza.
Zaina
Abdala Mzee Afisa Programu kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania (TAMWA Zanzibar) anasema endapo vifungu vilivyotajwa katika Sheria
hiyo ya Uchaguzi havitofanyiwa
marekebisho, kunaweza kukaja kukapelekea baadhi ya waandishi kuingia
kwenye matatizo na wengine kushindwa kufanya kazi kabisa katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu.
‘’Ni
vyema kukachukuliwa hatua za makusudi kuondoshwa vifungu hivyo ambavyo
vinaonekana vinabana uhuru wa waandishi na kuwanyima wananchi haki yao ya
kupata habari,’’ anashauri.
Zahran
Mohamed Yussuf ni mwanasheria wa kujitegemea kutoka Chakechake Pemba
anasema waandishi wa
habari ndiyo wenye jukumu la
kuuhabarisha umma juu ya mambo yanayotokea katika nchi yao, hivyo kama kutakua
na sheria zinazowabana kunaweza kukatokea athari kubwa kwao na hata kwa jamii.
‘’Ili
kuona waandishi wanatekeleza majukumu yao bila vikwazo na jamii inahabarishwa
juu ya mambo yanatokezea, ni muhimu kuwekwa sheria ambazo ni rafiki na ambazo
hazina mashaka,’’ anafahamisha.
VIONGOZI WA SERIKALI
Akitoa
ufafanuzi juu ya sheria hizo katika kikao cha maafisa habari kutoka Zanzibar
pamoja na Tanzania bara kilichofanyika visiwani Zanzibar Aprili mwaka huu,
Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita anasema
wanatarajia kupeleka muswada wa Sheria mpya ya Habari katika Baraza la
Mapinduzi.
Comments
Post a Comment