Yafahamu mavazi ambayo anatakiwa kuvaaa mwanamke akiwa kwenye michezo
NA FATMA HAMAD, PEMBA
MAUMBILE ya mwanamke kikawaida mwili wote hautakikani kuonekana isipokuwa viganja vya mikono na uso tu.
Na ndio maana wanatakiwa kujisitiri mwili mzima popote watakapokuwepo, ili kulinda zaidi heshima zao.
Kama Qur-an tukufu ilivyoeleza katika suratul Nour aya ya 31… ‘Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika (viganja vya mikono na uso)’.
‘…Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao au kaka zao au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao au wanawake wenzao au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio au watoto ambao hawajajua mambo yaliyohusu uke’
‘…Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubuni nyote kwa Allah (Subhanahu Wataala), enyi waumini, ili mpate kufanikiwa’.
Hivyo, pamoja na mwanamke kujishirikisha kwenye michezo lakini wawe makini katika kuhifadhi miili yao kwa kuvaa mavazi ya sitara.
Mwanamke anaruhusiwa kufanya shughuli mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo michezo ambayo sio ya nguvu ambayo haitopelekea kuumizana.
Mfano wa michezo wanayotakiwa kucheza ni mpira wa mikono, kuogelea, rede (nage) na ngonjera.
Lakini watakapocheza wanatakiwa wavae nguo zao kamili zinazostahiki kuvaa mwanamke wa kiislamu, ili asioneshe maumbile yake kwani ni dhambi.
Masheikh na maimamu wametuelezea kuwa, michezo kwa mwanamke sio haramu bali uharamu unakuja ikiwa watacheza utupu (ikiwa hawatovaa nguo za stara).
Hivyo mwanamke anaruhusiwa kucheza michezo mbali mbali kwa kuzingatia mavazi maalumu akiwa uwanjani ambayo hayamuoneshi maumbile yake.
Hata Sera ya Michezo ya Zanzibar ya mwaka 2018 imeeleza kuwa, itahakikisha mashindano yanayoandaliwa Zanzibar hayasababishi athari mbaya kwa mazingira ya nchi.
Mwandishi wa makala hii amezungumza na viongozi wa dini pamoja na wadau mbali mbali ili kuwafahamisha wanajamii mavazi ambayo anatakiwa avae mwanamke wakati akiwa kwenye michezo.
VIONGOZI WA DINI
Sheikh Said Ahmad Mohamed kutoka Ofisi ya Mufti Pemba anasema, mwanamke wa kiislamu ameruhusiwa kushiriki michezo kadhaa ikiwa atakumbuka kujistiri na kuhifadhi maungo yake.
Anasema, endapo mwanamke atacheza michezo akiwa amevaa nguo ambazo zimemsitiri mwili wake na kwamba hazioneshi maungo yake, basi si haramu kwa wao kushiriki michezo waitakayo.
‘’Uharamu haukuja kwenye michezo, bali umekuja pale ambapo atacheza akiwa hakuvaa nguo ambazo sio za kujisitiri,’’anaeleza.
Anasema mwanamke anatakiwa avae toafauti na mwanamme, anatakiwa avae baibui, Mashungi makubwa au suruali na fulana pana ambazo hazimbani akaonekana maungo yake.
‘’Ni haramu kwa mwanamke kucheza akiwa amevaa suruali vifupi na pia hatakiwi kuweka kichwa wazi (kutokuvaa mashungi ama hijabu),’’anafafanua Sheikh Said.
Anasema, uharamu haukuja kwenye michezo bali umekuja kwenye mavazi, hivyo endapo mwanamke atashiriki michezo akiwa amejisitiri, basi anaruhusiwa na inajuzu kucheza michezo kisheria.
Yohana Ali Mfundo ambae ni Mchungaji kutoka Kanisa la Mkusanyiko wa Mungu Tanzania (TAG) lililopo Ngerengere Chake Chake anasema, michezo ni moja ya sehemu ya mazoezi ambayo huimarisha afya.
Anasema, michezo kwa mwanamke si haramu katika dini yao, isipokua wanatakiwa wavae mavazi ambayo anastahiki kuvaa, kama anavovaa akiwa kwenye harakati zake za kawaida.
‘’Haipendezi kwa mwanamke kucheza michezo akiwa amevaa nguo vifupi, akaonekana maumbile yake,’’anafahamisha Mchungaji huyo.
Anaeleza kuwa, mavazi kwa mwanamke yametajwa katika kitabu cha Kimoteo ya kwanza sura ya pilli aya ya tisa inayoeleza…
‘Wanawake wajikaze kwa mavazi ya kujisitiri pamoja na adabu nzuri na moyo wa kujali’
Juma Othman Nahoda kutoka Jumuia ya walimu wa Madrasa Pemba (JUMWAMPE) anasema, sio vibaya mwanamke kushiriki michezo, isipokuwa anatakiwa kuvaa mavazi ya stara na yenye heshima kwake.
‘’Mavazi ambayo anatakiwa avae mwanamke anaopokua kwenye michezo ni yale ambayo hayatomfanya aonekanae maungo (mwili) yake,’’anasema.
Ni vyema wakavaa mabaibui, sketi ndefu, mashati makubwa na mashungi ili wasionekane miili yao.
Anafafanua kuwa …historia inatuonesha kwamba bibi Aisha (Radhiallahu Anhu) alikuwa akicheza michezo yeye na mume wake Mtume Muhammad (Swallallahu Alaiyhi Wasallim) huku akiwa amejisitiri.
Hivyo, sio vibaya mwanamke kushiriki michezo isipokua ajisitiri, ili isije ikapelekea kuingia kwake kwenye michezo ikaja ikamfanya aingie kwenye maovu.
Kassim Hamad Juma mkaazi wa Wingwi Wilaya ya Micheweni Pemba anasema, ni vyema wanawake wakavaa mavazi yao ya kawaida ikiwemo mashungi, mabaibui na soksi.
‘’Nivyema wanawake wakavaa nguo tofauti na wanaume, sio vizuri kuvaa nguo za kiume,’’anasema.
Kama hadithi kutoka kwa Ibni Abbass (Radhi za Allah ziwe juu yake) ivyoelezwa kuwa… ‘Rasuli wa Allah (Sallallahu alayhi wasallam) amewalaani wanaume wenye kuiga wanawake na wanawake wenye kujifananisha na wanaume’
Ambapo katika riwaya nyengine ‘Rasuli wa Allah amani iwe juu yake amewalaani wanaume wenye kujishabahisha na wanawake, na wanawake wenye kujifananisha na wanaume’ (imepokelewa na Al-bukhaariy)
Hii imeonesha wazi kwamba mwanamke anatakiwa kuvaa nguo zake za kike wakati wowote hata akiwa kwenye michezo.
Khadija Faki Ali mkaazi wa Sizini anasema, wanawake wavae nguo zao ambazo zinaendana na madili yao wakati wanapokua kwenye michezo.
WANAHARAKATI
Amina Ahmed Mohamed kutoka Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA) anasema, ipo haja kutolewa elimu kwa tasisi zinazohusika na masuala ya michezo ili kuona kwamba, wanaweka mavazi maalumu ambayo yanaendana na mila na tamaduni za kizanzibari wakati wakiwa kwenye shughuli zao za michezo.
‘’Ipo haja ya kutolewa elimu ili kuhakikisha wanawake wanavaa mavazi ambayo hayatopelekea kuonekana kama ni kituko katika jamii zetu nah ii itasaidia kuondosha dhana potofu kwamba mwanamke hawezi kushiriki michezo,’’anafahamisha.
WACHEZAJI WANAWAKE
Mchezaji wa timu ya ‘Simba Queens’ Fatuma Issa (Fetty Dansa) anasema, yeye amejizolea umaarufu mkubwa kutokana na uvaaji wake wa hijabu akiwa anatandaza soka dimbani.
Fetty Densa ambaye ni nahodha wa Simba Queens iliyopo Mkoani Iringa anasema, awali alikuwa hachezi na hijabu na kwa mara ya kwanza.
Anaeleza kuwa, alipoamua kuanza kuvaa hijabu alijisikia shida inagawa kwa sasa anajisikia faraja na hatamani kulikosa.
‘’Kwangu haina shida yoyote kucheza nikiwa nimevaa ushungi, ni kawaida na ninaamini kupitia mimi kuna wanawake wengine watajifunza, kwa sababu ni jambo jema na la kupendeza,’’ anafahamisha.
Kul -thum Ali Khamis mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya Wete Star (Women Club) anasema, kwake yeye ni kitu cha lazima kucheza akiwa amevaa shungi pamoja na baibui ama suruali pana ambayo haonekani maumbile yake.
‘’Sisi tunacheza tukiwa tumevaa suruali ndefu, mashati makubwa pamoja na vilemba, ili kutimiza matakwa na misingi ya dini ya Kiislamu,’’anaeleza.
Fatma Mkubwa Mussa mkaazi wa Mtuhaliwa Wilaya ya Mkoani Pemba ambae anacheza mpira wa mikono, anasema wanacheza wakiwa na nguo zao za stara.
‘’Tunacheza wanawake watupu na tumekua tukivaa mashungi, soksi pamoja na mabaibui, ili kukizi vigezo vya Imani ya dini yetu,’’anafafanua.
ZFF
Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar Ofisi ya Pemba (ZFF) Khamis Hamad Juma anasema, watahakikisha wanatoa elimu kwa vilabu vya michezo vya wanawake, ili kuona wanawapatia wachezaji wao mavazi yanayostahiki, ambayo yanaendana na mila silka na maadili yao.
‘’Ili kuhakikisha wanawake pamoja na watoto wa kike wanapata fursa zitokanazo na michezo, tutahakikisha viongozi wa vilabu wanawapatia wachezaji wao, mavazi ambayo hayaondowi utu na heshima zao,’’anasema.
Anasema, yapo mavazi ambayo wanaweza kuvaa wanamichezo na wakaweza kushiriki na wakajipatia fursa zilizomo kwenye michezo.
Anasema, ipo haja kuelimisha wanajamii waachane na itikadi potofu za kuwa michezo ni uhuni kwa wanawake na badala yake wasiwanyime watoto wao wa kike kushiriki michezo, bali wawaruhusu kwani hata dini imeruhusu.
Michezo ni mazoezi na afya hivyo kila mmoja anaruhusika kushiriki michezo mbali mbali kwa kuzingatia mila, tamaduni na imani za dini.



Comments
Post a Comment