Wastaafu anzisheni miradi ili iwasaidie baada ya kustaafu
NA FATMA HAMAD- PEMBA
Afisa Mdhamini Ofisi ya Raisi Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala bora Halima Ali Khamis amewataka wastaafu watarajiwa kuyatumia mafao yao ya kustafu kwa kuanzisha miradi ya maendeleo ambayo itawapatia kipato ili waweze kuendesha maisha yao.
Mdhamini huyo ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya mandalizi ya kustaafu kwa wastaafu watarajiwa huko Tibirinzi Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema kustaafu sio mwisho wa maisha bali ni vyema wakajiwekea akiba pamoja na miradi mbalimbali, ili waweze kuishi maisha yao ya kawaida kama walivyokua wakiwa kazini.
‘’ Niwaombe wazazi wangu,tusishtuke, bali tijiekeze, tusizitumie pesa zetu kwa kuzifanyia mambo ambayo hayatatuletea faida kwetu,’’alisema.
Aidha aliwapongeza watumishi hao kwa kuwa na moyo wa imani na kuutumikia vyema utumishi wao hadi kufikia muda wao wa kustaafu, huku akiwataka waache khofu wakati watakapopaew barua zao za kuustaafu, kwani ni jambo la kawaida kwa kila mtumishi wa umma.
Mapema akiwasilisha mada ya maisha baada ya kustaafu Mwezeshaji wa mafunzo ya wastaafu kutoka Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Williamson Ferdinand alisema ni vyema kwa watumishi wanapostaafu wasikae majumbani bali waendelee kufanya shughuli zao ndogondo pamoja na kufanya mazoezi ili waweze kulinda afya zao.
‘’Niwaombe wazazi wangu mnapofikia kustaafu musikae tu bali tafuteni shughuli zozote mfanye, hatakama ni kufanya mazoezi, ili kuepuka kupata maradhi mapema,’’alisema.
Nao baadhi ya watarajiwa hao ambao walishiriki katika mafunzo hayo wamelishukuru shirika la ZSSF kwa kuwapatia mafunzo hao ambayo yatawafanya waondokane na khofu kabla ya kukabidhiwa barua za kustaafu.
Aidha walisema watahakikisha wanaweka miradi ambayo itawaletea kipato ambacho kitaendesha maisha yao, ili kuepukana na utegemezi ndani ya familia zao.
Comments
Post a Comment