JAMII YAOMBWA KUWASHIRIKISHA WANAWAKE KWENYE MICHEZO
NA FATMA HAMAD, PEMBA
Katika zama za sasa suala la michezo limekuwa ni moja ya njia ambayo hupelekea baadhi ya watu kujipatia fursa mbali mbali za maendeleo, ikiwemo ajira.
Tumekuwa tukishuhudia kuwa vijana wakiajiriwa katika taasisi za Serikali ikiwemo kwenye vikosi vya Polisi, kuajiriwa kwenye timu za ndani na nje ya nchi.
Lakini fursa hizo mara nyingi huzipata vijana wa kiume, kwani jamii bado haijakuwa na mwamko wakutosha kufahamu kwamba, mwanamke na yeye anahitaji kuzipata fursa hizo.
Hadi leo hii bado jamii imekuwa na mawazo kwamba mwanamke akishiriki michezo atakua hana maadili mazuri, hali inayopelekea siku zote kuishia kuwa watazamaji na washangiliaji katika suala la michezo.
Kwa mujibu wa dini, mwanamke ameruhusiwa kushiriki michezo, kwani michezo ni moja ya njia ya kuufanya mwili kuwa imara na kuweza kupambana kwa kila magonjwa kwa sababu ni mazoezi.
Hivyo basi, ili kuona mwanamke na yeye anafaidika na fursa zilizomo kwenye michezo, makala hii imewatafuta wadau mbali mbali pamoja na wanajamii kutaka kujua ni kitu gani cha kifanyika ili kuona na wao wanashiriki michezo kuona wanapiga hatua kimichezo na kujipatia fursa mbali mbali.
JAMII
Rashid Hamad Khamis mkaazi wa Pandani wilaya ya Wete Pemba anasema, ni vyema Wizara inayohusiana na masuala ya Michezo ikaanzisha mabonanza mbali mbali ya wachezaji wanawake mara kwa mara, jambo litakaloishawishi jamii kuwapa fursa wanawake pamoja na watoto wa kike kushiriki michezo.
‘’Ili kuona jamii inashawishika na michezo kwa wanawake, ni vizuri wakaanzisha mabonanza na washindi wakapewa zawadi, hii itatoa hamasa kwa wanawake kushiriki michezo,’’anaeleza.
Khatib Iddi Abdulla mkaazi wa Chake Chake Pemba anasema, ili kuona wanawake wanashiriki michezo, ni vyema itolewe elimu kwa Jamii iweze kuondokana na mawazo mgando na kuhakikisha wanawapa fursa, ili washiriki.
‘’Ipo haja ya kutolewa elimu kwa wanajamii juu ya michezo kwa mwanamke, ili waweze kuwaruhusu kushiriki kwenye michezo, jambo ambalo litawasaidia kujichukulia fursa zitokanazo na michezo,’’anasema.
Mtumwa Ali mkaazi wa micheweni anasema, ili kuona wanawake na wao wanashiriki michezo, ni vyema jamii ikapewa elimu ili iwe na mwamko wa kuwashirikisha wanawake michezoni.
‘’Jamii bado haijaona umuhimu wa mwanamke kushiriki katika michezo, hivyo waelimishwe na kuoneshwa fursa zilizopo, itasaidia wanawake kuzipata fursa hizo,’’ anaeleza mama huyo.
Sheikh Said Ahmed Mohamed anasema ni vyema viongozi wa skuli pamoja wa vilabu vya michezo watakapoanzisha timu za wanawake, ziwe ni zenye kufuata madili na misingi ya kiislamu.
‘’Suala la michezo huwezi kulipinga katika mfumo wetu wa maisha, hivyo tusipoweka michezo yenye misingi ya kiislamu, kutapelekea watoto kujiingiza katika michezo wanayoitaka wao, ambayo haiko kwenye maadili yao,’’anasema.
Aliekuwa Mratib wa Chama cha Wandishi wa habari wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA) kwa upande wa Pemba, Fat-hiya Mussa Said anasema, ili kuona wanawake na watoto wa kike wanashiriki michezo ni vyema ikatolewa elimu kwa jamii waweze kuwaruhusu watoto wa kike kujiunga kwenye michezo, ili wapate fursa zitokanazo na michezo.
‘’Wapo watoto wa kiume wameajiriwa kutokana na masuala ya michezo, hivyo ipo haja kutolewa elimu kwa jamii, ili iweze kufahamu fursa hizo na kuzichangamkia,’’anaeleza.
Anasema, kwa sasa wamekuwa wakiwajengea uwezo waandishi wa habari waweze kuielimisha jamii juu ya michezo kwa mwanamke na kuhakikisha wanaibua vipaji vya michezo vilivyomo katika jamii, ili viweze kujulikana na kupata kuendelezwa.
VIONGOZI WA SERIKALI
Afisa Mdhamini wizara ya Habari Vijana utamaduni na Michezo Mfamau Lali Mfamau anasema, katika kisiwa cha Pemba suala la michezo bado halijapewa kipaumbele, jambo linalosababisha wanawake kukosa fursa zitokanazo na sekta hiyo.
‘’Fursa nyingi za michezo zinatokea ambazo zinahitaji wanawake lakini nafasi hizo zinarudi kwao, kutokana na kuwakosa wanawake hao,’’anasema.
Anasema, wakati umefika kwa jamii kuamka na kuondokana na mawazo potofu juu ya masuala ya michezo, ili wanawake na wao waweze kupata fursa hizo.
Khamis Hamad Juma Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa miguu Zanzibar anasema, ili kuona wanawake wanashiriki ipasavyo katika michezo ikiwemo mpira wa miguu na mpira wa mikono, ipo haja kutolewa elimu kwa jamii kuondokana na mawazo mgando kwamba, mwanamke akishiriki michezo atakua muhuni.
‘’Bado jamii ya wananchi wa Pemba wanaimani potofu juu ya michezo kwa mwanamke, hivyo ipo haja kuelimishwa kufahamu umuhimu wa michezo na kuweza kuwaruhusu watoto wao wa kike,’’anasema.
WANAMICHEZO WA KIKE
Kulthum Ali Khamis mkaazi wa Mgogoni Wilaya ya Micheweni Pemba ambae anacheza timu ya Wete Star anasema, Jamii imekua ikiwachukulia wanawake wanaoshiriki michezo kama ni wahuni na wameshatoka katika misingi ya dini yao.
‘’Tumekua tukiitwa majina mabaya, tukidharauliwa, hivyo ipo haja jamii kuelimishwa ili wanawake tushiriki michezo bila ya kunyanyapaliwa,’’anasema.
Fatma Mkubwa mchezaji wa mpira wa miguu ya wanawake wenye ulemavu iliyopo Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba anasema, bado jamii haijakua na uelewa wa kutosha juu ya michezo kwa mwanamke.
Anasema, ni vyema kukawekwa mikutano maalumu vijijini, ili wazazi wawaruhusu watoto wao ambao wana vipaji vya michezo, kwa ajili ya kuwaendeleza.
Comments
Post a Comment