Wasaidizi wa sheria wapewa mbinu

 

                 NA FATMA HAMAD- PEMBA

Wasaidizi wa Sheria  wametakiwa kuendelea  kutoa elimu kwa jamii juu ya masuala ya udhalilishaji, ili kuona inaondokana na vitendo  hivyo viovu ambavyo  vimekua  vikijitokeza siku  hadi  siku.

Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wasaidizi wa sheria wa wilaya ya Micheweni  Muhasibu wa Jumuia ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya hiyo  Riziki Ali Hamad juu ya masuala ya udhalilishaji, huko Tumbe wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema katika wilaya ya Micheweni  bado kumekua kukijitokeza masuala ya ubakaji na ulawiti  kwa watoto, hivyo ipohaja kwa wasaidizi wa sheria kuisaidia jamii kwa kuwaelimisha madhara yatokanayo na  masuala hayo,  ili kuona yameondoka.

Akitaja  sababu inayopelekea kujitokeza kwa masuala hayo ya ubakaji na ulawiti  katika wilaya hiyo ni utelekezwaji uliokithiri wa wanawake na watoto.

Alisema wapo baadhi ya wazazi wa Micheweni huondoka vijijini mwao  na kwenda kufanya shughuli zao za uvuvi katika maeneo mengine kama vile Tanga, Mombasa, Mafia,  ambapo mwisho wa siku huziacha familia zao na kuzitelekeza.

‘’Mababa wengi wanapondoka na kwenda kufanya shughuli zao za uvuvi maeneo mengine, huzitelekeza familia zao, na  badalayake hutafuta wanawake wengine  na kuanza nao maisha,’ alisema.

Alisema kutokana na hilo ipo haja  kwa wasaidizi wa Sheria kukaza kamba  kuwaelimisha wanajamii, ili kuona kila mzazi analea na kutunza familia  yake, jambo litalopelekea kuwa muarubaini wa masula hayo ambayo imeonekana ni kero kubwa kwa wanawake na watoto, hususani wanaoishi katika maeneo ya bahari.

Alisema kwa sasa wanatekeleza mradi wa sauti ya mwanamke ambao unalengo la kuwasaidia wanawake na wasichana na jamii kwa ujumla juu ya masuala ya udhalilishaji, ili kuona wanaondokana na tatizohilo.

 Mapema mkufunzi wa mafunzo hayo Suleiman Hemed alisema lengo hasa la kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa sheria ni kuhakikisha wanafika kila shehia na kutoa msaada  wa kisheria kwa jamii, ili kuona  wanakua na uwelewa juu ya masuala hayo na kuripoti katika vyombo vinavyo husika wakati vinapotokea vitendo hivyo na kupata haki zao.

Nao wasaidizi hao wa Sheria akiwemo Othman Juma Nahoda na Ziada Ali Hamad walisema watahakikisha wanatekeleza majukumu yao  ipasavyo na kwa mujibu wa Sheria ilivoelekeza, ili kuona jamii imeilimika na kuwa mstari wa mbele kutokomeza udhalilishaji.

Katika Mradi huo wa Sauti ya mwanamke ambao unatekelezwa na Jumuia ya wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Micheweni ni ufadhili wa Shirika  la Msaada wa kisheria LSF na Umoja wa Ulaya (ENABLE)




Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO