WANAHABARI, WADAU ZANZIBAR SASA WATAMANI SHERIA MPYA YA HABARI





                             NA FATMA HAMAD,PEMBA

NI miaka 37 tangu Sheria ya Habari kufanyiwa marekebisho, ingawa bado vipo baadhi ya vifungu katika sheria hiyo vina mapungufu, ambapo  vinaminya uhuru wa habari.

Inavyotakikana kila  baada ya miaka 10 sheria huwa ndio zinahitaji kurekebishwa,  ili kuondosha mapungufu ya vifungu ambavyo vitakua vinaenda kinyume na utekelezaji wa sheria hiyo.

Ambapo wakati mwengine, sio lazima kusubiriwa miaka 10 bali itakapoonekana tu sheria inamapungufu, basi ni vyema ikarekebishwa.

Kwani kufanya hivyo, kutasaidia kuweka sawa vifungu vyenye mapungufu na  kuendana na muda na mazingira ya sasa.

Ila tukiangalia sheria ya Usajili wa Uwakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanywa marekebisho mwaka 1997, imeshakua kongwe, haiendani na ulimwengu wa sasa.

Katika makala hii tutaangalia kifungu cha 30, ambacho kinampa  mamlaka makubwa  Waziri  wa habari kiasi ambacho kinaminya uhuru wa habari.

Kwani  kifungu hicho  kinaeleza kuwa endapo Waziri ataona kuwa ni kwa manufaa Umma au kwa maslahai ya amani na utulivu anaweza kuamuru kufungiwa kwa gazeti.

Na ndio maana wandishi wa habari pamoja na wadau wa habari mbali mbali wamekuwa wakipaza sauti zao , ili kuona sheria hizo zinafanyiwa marekebisho, kwa ajili ya kuondosha mapungufu yaliyomo ili ziendane na wakati wa sasa.

Wandishi wa habari  ndio wadau wa kubwa ambao wanakerwa  na sheria hiyo, wanaeleza  kuwa ni vyema ikaangaliwa  tena upya, ili iweze kufanyiwa marekebisho.

WANDISHI WA HABARI

Khadija Kombo Khamis mwandishi wa habari wa ZBC Pemba anasema wakati umefika kwa wanaohusika na mambo ya kisheria,  kuifanyia marekebisho  Sheria hiyo ili wanahabari waweze kufanya kazi zao bila kuingiliwa.

"Kwa kweli tunapoiona hii Sheria inatupa wakati mgumu wa kutekeleza majukumu yetu, kwa sababu ndani yaku kuna vikwazo kwetu," alisema mwandishi huyo.

Salim Hamad Faki ni Mwandishi wa habari wa Tif TV  anasema  ili kuwepo kwa uhuru wa habari nchini  ni vyema  kifungu hicho kikafanyiwa marekebisho.

"Kwa kweli sheria ya habari ni kongwe kabisa, hivyo tuna tamani ipitiwe na iangaliwe tena upya kwani haiendani tena na muda," alisema.

Khadija Ali Yussuf  ni mwandishi wa Redio Jamii Mkoani  anasema, sheria ya habari inafaa kufanyiwa marekebisho, ili iweze kuendana na mazingira ya kiteknolojia.

"Kifungu hicho kinanyima uhuru wetu, hivyo tunahitaji kifutwe ili tuweze kufanya kazi zetu tukiwaa huru,’’anasema.



                                WADAU WA HABARI

Haura Shamte mwandishi wa habari mkongwe kutoka kisiwa cha Unguja, anasema  ni wakati wandishi wa habari kufanya utetezi wa kina, juu ya  sheria hizo ziweze kufanyiwa marekebisho.

‘’Kwa kweli sheria yetu imeshapitwa na muda tunaomba ifanyiwe marekebisho, ili kuondoa vifungu ambavyo vinakinzana na uhuru wa vyombo vya habari," anasema.


Mustafa Mohamed  kutoka Tasisi ya Moyo Media anasema,  uwezo aliopewa Waziri, kifungu cha 30  cha Sheria ya Usajili wa Uwakala wa habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 ni mkubwa.

Anaona wakati ndio kwa serikali pamoja na watu wahabari kukaa pamoja ili waweze kuiangalia tena sheria hiyo.

Anasema, ni vyema kwa nafasi ya uwaziri kupewa mtu ambae ana amesomea masuala ya habari (fani)  ya habari, ili iwe ni rahisi kuiendesha wizara hiyo kwa ufanisi.

 TAASISI ZINAZOSHUGHULIKIA MASUALA YA HABARI

Mwenyekiti wa Klabu ya Wandishi wa Habari Pemba (PPC) Bakar Mussa Juma anasema, ipo haja kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya habari kwani ilishakua ya zamani, haiendani tena na mazingira ya sasa.

Anasema, Sheria hiyo inathiri uhuru wa habari kwani imempa mamlaka makubwa Waziri, ambayo yanapelekea kukosekana kwa uhuru wa habari.

Afisa  programu  kutoka Chama cha wandishi wa habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA) Zaina Abdalla Mzee, anasema wameweka  mikakati  mbali mbali kuzisemea sheria hizo,  ili kuona wahusika wanaoshughulika wanachukua hatua kuhusu kilio chao hicho.

"Tunafanya makongamano na wadau mbali mbali pamoja na kuwapa kazi waandishi wa habari nawao waweze kuzisemea katika vyombo vyao, ili kuona zinafanyiwa kazi," alisema.

Anasema, endapo sheria hizo zitaendelea kuwa kandamizi hazitowathiri wanahabari tu, bali kutaathiri jamii nzima kwa sababu kutakosekana kupatikana kwa habari.

MWANASHERIA

Khalfan Amour Mohamed mwanasheria wa kujitegemea kisiwani Pemba anasema ipo haja ya kuondoshwa kabisa kifungu hicho cha 30.

Kwani anasema Waziri  ni binadamu kama binadamu wengine ana mapungufu yake, hivyo  akipewa mamlaka  makubwa kama hayo, lazima atakuwa na udhaifu wake na ikitokea kukerwa na mwandishi , atakifungia  chombo cha habri kwa maslahi yake binafsi na sio kwa taifa. 

"Hii ni kasoro kubwa na haitoi uhuru kwa mwandishi anapoamua kufanya kazi zake, alisema.

ATHARI YAKE

Kukosekana kwa Sheria ya habari ambayo inakandamiza uhuru wa wandishi wa habari, kunaweza kukapelekea kutokuripotiwa baadhi ya matukio yanayotokea Nchini (Asha Ali ) ambae sio jina lake halisi  mkaazi wa Tumbe Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba anasema.

NINI KIFANYIKA

Ili kuona wandishi wa habari wanatekeleza majukumu yao wakiwa huru bila ya woga wowote, ni budi vifungu vyote ambavyo vinaminya uhuru wa habari vikafanyiwa marekebisho, ama vikafutwa kabisa wadau wa habari wanasema.

        

       

Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO