Mchango wa wanaume juu ya michezo kwa mtoto wa kike



 


NA FATMA HAMAD, Pemba

Watoto wa kike nao wana haki ya kupata fursa mbali mbali zitokanazo  na sekta ya michezo, kama wanavyopata watoto wa kiume.

Katika ulimwengu wa sasa michezo imekua na fursa nyingi, kama vile ajira, kupata kutembea nchi tofauti tofauti na pia kupata afya bora.

Hata Katiba ya Zanzibar ya 1984 katika kifungu cha 6 (2) kinaeleza kuwa, kila mzanzibari kwa misingi ya Katiba hii, ataweza kufaidi haki na fursa zote anazostahiki mzanzibari.

Hivyo, ipo haja kwa wanaume kuamka na kutoa fursa kwa watoto wa kike washiriki michezo, ili waweze kujichukulia fursa zitokanazo na michezo.

Na hii ilionekana tangu miaka ya zamani ambapo mtoto wa kike alikua akiachwa nyuma katika suala zima la michezo.

Katika makala yetu hii, tutaangalia mchango wa wazazi wa kiume katika kuwahamasisha  watoto wa kike kushiriki michezo.

JAMII

Ali Khamis Kombo mwenye miaka 60 mkaazi wa Sizini Wilya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazi Pemba, anasema tangu alipotia fahamu hakuwahi kuona hata siku moja katika vijiji vyao wanamke kushiriki michezo.

‘’Tangu enzi za zamani wanawake waliachwa nyuma, katika suala zima la michezo,’’anasema.

Mkaazu wa Gombani Chake Chake Khatib Iddi Mwalim anasema, wanaume wawaruhusu watoto wao wa kike kujiunga kwenye michezo kwani, michezo ni moja njia inayoweza kuwapatia ajira.

‘’Tumekua tukishuhudia vijana wengi wakipata ajira kama vile vikosi, hivyo wazazi wa kiume msiwazuie watoto wa kike kujiunga na michezo na wao wanayo haki ya kupata hizo ajira,’’ anaeleza.

Bimkubwa Mohamed mkaazi wa Tumbe Mashariki wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba anasema, michezo huimarisha afya, hivyo ni vyema  wanaume   kutoa fursa kwa watoto wa kike kujiunga na michezo, ili kuwakinga na maradhi.

‘’Wazazi wa kiume wapeni nafasi watoto wa kike wajiunga kwenye michezo, kwani kufanya hivyo, kutawasaidia kuwa na afya njema,’’ anaeleza.

Juma Kombo Hija mkaazi wa Micheweni Pemba anasema, ni vyema wanaume kuwa na imani juu ya watoto wao wa kike kushiriki kwenye michezo, ili na wao wajione kama ni sehemu ya jamii ambayo inahitaji kupata fursa za maendeleo, ambazo zipo nchini.

WANAMICHEZO WA KIKE

Kul-thum Ali Khamis ambae ni mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya Wete Star (Women Club) anasema, wanaume wana nafasi kubwa ya kuhakikisha wanatoa fursa kwa watoto wao wa kike kushiriki kwenye michezo.

Anasema, wazazi wa kiume waliowengi bado hawajawa na imani ya kutosha juu ya kuwaruhusu watoto wao wa kike kushiriki michezo, kwani wanahisi ni uhuni.

‘’Akinababa wengi bado hawajawa na imani juu ya mtoto wa kike kushiriki kwenye michezo kumbe anaweza kujipatia kipato kupitia michezo,’’ anaeleza.

Anasema, ipo haja kwa wazazi wa kiume kuondosha mawazo finyu na badala yake wawape fursa watoto wao wa kike kushiriki kwenye michezo, ili nawao waweze kujipatia fursa za kimaendeleo ambazo zinatokana na sekta hiyo.

Kul-thum anatamani siku moja awe miongoni mwa wachezaji wakubwa wa mpira wa miguu duniani, ili aipatie sifa nzuri familia yake ambayo imemunga mkono na hata Taifa lake.

Aisha Ali mwenye umri wa miaka 17 mkaazi wa Sizini anasema, anapenda mchezo wa riadha pamoja na mpira wa miguu, ingawa aliishia kucheza akiwa skuli tu, kwa sababu familia yake haimruhusu tena kutokana na kile kilichoonekana kuwa akiendelea atakuwa muhuni.

‘’Nilitamani siku moja nije niwe mwanamichezo maarufu duniani, lakini kipaji changu kimedumaa kwa sababu sikupata kuendelezwa,’’ anasema.

Mtoto Fatma Mkubwa mwenye umri wa miaka 15 mkaazi wa Mkoani anawashauri wazazi wawaruhusu washiriki michezo, kwani wanatamani kufika mbali.

‘’Nasisi tuna uwezo wa kucheza na tukafanya vizuri, hivyo wazazi musituzuie, michezo itasaidia kukuza vipaji vyetu,’’anasema.

Anasema, anacheza mpira wa mikono katika timu ya watoto wenye ulemavu huku ndoto yake siku moja ni kuona amefika nchi za Ulaya kwa ajili ya mchezo huo.


                            VIONGOZI WA SERIKALI

Afisa Mdhamini wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mfamau Lali Mfamau anasema, bado wananchi hususani Pemba, hawajawa na mwamko juu ya la michezo kwa mtoto wa kike, kwani wanahisi ni kitendo kinachokwenda kinyume na madili yao.

‘’Tukiangalia vipaji vya michezo kwa watoto wa kike tunavyo mitaani, lakini wazazi hawawaruhusu,’’ anaeleza.

Anasema, Idara ya Michezo imekuwa ikitoa fursa mbali mbali kupitia michezo, hivyo ni wakati kwa wazazi wa kiume  na wa kike kuamka na kuwahamasisha watoto wao wa kike kujiunga kwenye michezo, ili wafaidike na fursa zilizopo.


Khamis Hamad Juma ambae ni Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) Ofisi ya Pemba, anasema ipo haja kwa Serikali, pamoja na wadau wa michezo kuwaelimisha wazazi hasa wa kiume juu ya  umuhimu wa michezo.

Anasema, ni vyema wakawaruhusu watoto wao wa kike kwenye michezo, kwani siku moja inaweza kuwa mkombozi wa maisha yao.

WANAHARAKATI

Amina Ahmed Mohamed kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande Pemba anasema, wazazi wa kiume wanahitaji kupewa elimu, ili waweze kufahamu umuhimu wa michezo kwa mtoto wa kike na wawaunge mkono.

Anasema, kutokana na itikadi potofu zinazojengeka katika jamii kwamba michezo kwa mwanamke  ni uhuni, wazazi wa kiume wanashindwa kuwapa nafasi watoto wao wenye vipaji vya michezo.

‘’Utakuta watoto wa kike wengi wanaishia kucheza michezo wakiwa skuli tu, wakimaliza vipaji hivyo vinakufa, kwa sababu imejengeka katika jamii kuwa michezo ni kwa wanaume tu,’’ anaeleza.


                    

                    

 

 

 

 

 

 



Comments

Popular posts from this blog

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

‘’KATIBU MKUU ELIMU ‘’TOENI ELIMU YA MALEZI BORA’’

UROHO WA MALI KWA WANAUME UNAVYONYIMA WANAWAKE ARDHI