Wagombea wanawake wanavyosahau fursa ya mitandao ya Kijamii- Pemba.
Na Fatma Hamad
Pemba:
Mitandao ya Kijamii si sehemu ya anasa kama ambavyo wengine hudhani bali pia ni sehemu inayoweza kusaidia kuwaleta watu pamoja wenye mitazamo ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kimichezo.
Hadi kufikia Januari 2018 duniani kulikua na watumiaji wa huduma za Interneti takriban Bilioni 4.02 sawa na 53% ya idadi ya watu wote.Kati ya hao watumiaji wa Mitandao ya kijamii wanafikia Bilioni 3.2 sawa na 42% ya watu wote Duniani.
Kwa mujibu wa Jarida la Forbes hapa Tanzania mpaka kufikia Mei 2021 kumeripotiwa kuwa na watumiaji wa huduma za Intaneti zaidi ya Milioni 29, huku watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya kielekroniki wafikia Milioni 32.
Wapo baadhi ya watu wamekua wakiijingizia kipato kupitia mitandao na kupata umarufu kwa kuuza bidhaa zao.
Shikha Seif Suleiman, (40) mkaazi wa Chake chake ambae anafanya biashara ya nguo kupitia mitandao ya kijamii zaidi ya miaka minne anasema amejizolea wateja wengi baada ya kujitangaza kwenye mitandao.
”Unapotumia mitandao unaweza kuwafikia wateja wengi, na pia soko linakua la uhakika kwani watu wengi wako kwenye mitandao kwa sasa” Amesema Shikha huku akieendelea kusema kuwa ni wakati kwa wanawake wagombea kuitumia mitandao ya kijamii kunadi sera zao kwa kipindi chote cha uchaguzi na hata wanapoanza harakati za siasa. “Fursa hio ipo na ni vyema wanawake wanasiasa na viongozi kutumia” Amemaliza.
Ingawa licha ya mitandao kuwa ni fursa lakini bado wagombea wanawake kisiwani Pemba wamekuwa wakikosa fursa hiyo kwa kutokumia kikamilifu mitandao ya kijamii katika harakati zao za kisiasa kutokana na uwelewa mdogo wa matumizi ya mitandao hio.
Hadia Omar Dadi mwanachama wa Chama cha Mapinduzi - CCM amegombea uwakilishi Jimbo la Wingwi ,Wilaya ya Mkoani na Mkoa zaidi ya mara tatu anasema hajawahi kutumia mitandao ya kijamii kurusha tarifa zake kwa kipindi chote cha kampeni.
‘’Sikuwahi hata siku moja kutumia mitandao ya kijamii kwani sikuwa na elimu hiyo ya kutumia mitandao na hata sasa nikipata nafsi tena sijui kama nitaweza maana sijajua kutumia’’
Hadia ni mama ambaye alianza siasa mwaka 2000, amesema kuwa mwaka jana alipata elimu juu ya umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii kutoka Chama cha wandishi wa habarai Wanawake Tanzania –TAMWA-Z, na ameanza kuitumia mitandao ikiwemo kurasa za facebook na Twitter ama X.
Hadi mwaka 2023, takriban watu milioni 10.5 nchini Tanzania wanatumia mitandao ya kijamii, kama Facebook, Whatsapp, Instagram, na TikTok, na wengi hutumia zaidi kwa mawasialiano, burudani, na biashara,huku wanawake takriban 40.45% ambapo ni zaidi ya milioni 5 wanaotumia intaneti nchini Tanzania.
Huko Chake Chake ,Mkoa wa Kusini Pemba Mwanachama wa Chama cha Tanzania Labour Party – TLP Ziada Khalfan Saleh,48 mkaazi wa Machomane, ambae aligombea Ubunge Jimbo la Ziwani zaidi ya mara tatu kupitia amekiri hajawahi kutumia mitandao ya kijamii kwenye shughuli zake za kisiasa.
‘’Sikuwa na uwezo wa kuwaita wandishi wa habari wakanirushia kwenye mitandao, na mimi mwenyewe sikuwa na hata hiyo simu kubwa nikaweza kujitangaza hivyo hizo changamoto zilizonikabili’’Amesimulia Ziada huku akiomba wadau kuwasaidia wanawake waliopo kwenye siasa kutumia mitandao ya kijamii.
Wataalamu wa masuala ya kiteknolojia ni wadau muhimu kwenye kuweza upatikanaji wa maarifa na ujuzi wa matumizi ya mitandao ya kijamii,Mustapha Mohamed Moyo ambae ni mtalamu wa masuala ya matumizi ya mitandao kisiwani Pemba,amesema mitandao ya kijamii inaweza kumsaidia mtu kupiga hatua moja na kwenda nyengine na kutambulika .
‘’Mitandao ya kijamii ni moja ya njia inayomsaidia mtu kupiga hatua kimaendeleo,’’amesema.
Mustafa ameongeza kuwa ni wakati kwa wanawake wanaogombea kuitumia mitandao ya kijamii kujitangaza, kwani kunaweza kukawafanya kupata nafasi kwa vile tu kujitangazaAmemaliza Mustafa.
Afisa Msajili wa vyama vya siasa Zanzibar Abdul-Razak Said Ali amesema uwepo wa sheria inayosimamia makosa ya mitandao Tanzania, ya mwaka 2015 itasimamia ulinzi wa wanawake na unyanyasaji mitandaoni hivyo kuna uhuru wa wanawake wanasiasa kutumia na kukuweza kujipatia wafuasi na kupata maarifa
“Masuala yote kuhusiana na makosa ya kimtandao yanadhibitiwa juu ya sheria hiyo lengo ni kuwasadia wanawake wanapata haki zao pindi wakikumbana na ukatili kwenye mitandao” Amesema Abdul –Razak huku akiwataka wanawake kutumia nafasi hio “Wanawake wasirudi nyuma bali waitumie haki yao hiyo ya mitandao ya kijamii na kuweza kunadi sera zao na kuweza kutambulika kwenye nyaja za kisiasa” Amemaliza kuzungumza Abdul Razak.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania - TCRA Dkt. Jabiri Bakari amesema mamlaka hio inaendeleza kutoa elimu ya masuala ya kidijiti na usalama mtandaoni kwa kuhakikisha mazingira salama na imara ya matumizi bora ya mitandao kwa watu wote.
”Ingawaje mipango ya kuongeza uelewa wa umma ni ajenda ya kudumu ya TCRA, kampeni hii inatokana na umuhimu wa kipekee kuwapatia watanzania mbinu za kujilinda dhidi ya mashambulio ya mitandao ya intaneti na simu niwaombe hii pia ni kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni” Amesema Jabir.
Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA –ZANZIBAR, ni Taasisi isiyo ya kiserikali inajikita katika utetezi wa masuala ya wanawake,watoto na watu wenye ulemavu,wakiwa katika utekelezaji wa mradi wa Wanawake wa uongozimradi unawawezesha wanawake kupitia vyombo vya habari wanaona kuwa kuna haja ya wao kusaidia wanawake kwenye kujua na kufahamu matumizi sahihi ya mitandao.
Afisa mkuu wa Mahusiano kutoka chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA) Sophia Ngalapi anasema juhudi zao ni kuwaelimisha wagombea wanawake, waweze kutumia mitandao ya kijamii waweze kurusha habari zao, ili waweze kujulikana na kungwa mkono katika jamii.
Comments
Post a Comment