Mkakati wa Polisi kwa wagombea wanawake katika Uchaguzi wa 2025
NA FATMA HAMAD-PEMBA
Ni wakati sasa wa dunia kutambua umuhimu wa wanawake katika uongozi, kwani wanapokua katika ngazi za maamuzi ni chachu ya kuondosha ubaguzi wa kijinsia, na kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Hata hivyo idadi ya ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi bado ni mdogo, hivyo ipo haja kuwekwa mikakati madhubuti, ikiwemo kutekeleza sheria ambazo zinazingatia mazingira salama naya uwazi kwa wanawake kuweza kushiriki katika uongozi.
Na ndio maana Serikali ya mapinduzi Zanziba ikafanya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa Zanzibar ya mwaka 2024, ili kuondosha baadhi ya vifungu ambavyo vimekua ni kandamizi kwa wagombea wanawake.
Kutokana na hayo wenzetu wa Jeshi la Polisi Zanzibar likaja na mkakati makhsusi kwa ajili ya kuwalinda wagombea wanawake dhidi ya vitendo vya udhalilishaji, ili kuona wanakua salama katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025.
JESHI LA POLISI
Kamishna Msaidizi wa Polisi Cyprian Mushi akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Abdallah Moh’d, anasema, watahakikisha wanaimarisha ulinzi kwa wagombea wanawake dhidi ya vitendo vya udhalilishaji, ikiwemo kupigwa, kutukanwa na kunyanyaswa katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Anasema wapo baadhi ya wanawake ambao wana nia ya kuingia majimboni kugombea uongozi ingawa, wamekua na hofu ya kufanyiwa kwa vitendo vya udhalilishaji.
Anasema, suala la kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya kila raia kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, hivyo ni wakati wa akinamama kuhakikisha wanaingia kwa wingi kwenye chaguzi, ili wawe wengi kwenye vyombo vya maamuzi.
‘’Suala la uongozi si kwa mwanamme pekee bali hata mwanamke, hivyo msiogope kuingia majimboni, kwa sababu ni haki yenu kikatiba, msiwaachie wanaume pekee,’’ameeleza.
Anaeleza kuwa, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 watahakikisha wanaimarisha ulinzi mkali hasa kwa wagombea wanawake, ili kuona wanamaliza uchaguzi katika hali ya amani na usalama bila ya kupatwa na madhara yoyote.
Sambamba na hayo, anawasisitiza wanawake ambao wataingia kwenye mchakato wa uchaguzi, kuhakikisha waimarisha suala la amani na utulivu wakati wote wa kampeni, wakati wa uchaguzi na hata utakapomalizika.
WAGOMBEA WANAWAKE
Tumu Mwalimu Khamis aliegombea ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Wingwi anasema, wanawake wengi ambao wanania ya kuingia katika chaguzi hasa wa vijijini, wamekua wakirudi nyuma, kutokana na kuwa na hofu ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Anasema, ni ukweli uliowazi kwamba baadhi ya wagombea wanawake wamekuwa wakidhalilishwa kwa kutukanwa, kuitwa majina mabaya, kupigwa n ahata udhlilishaji wa kingono, jambo ambalo limesababisha wengi kukata tamaa.
Batuli Mussa Sharif kutoka Chama cha ACT Wazalendo mkaazi wa Sizini Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba anasema Jeshi la Polisi litafanya jambo la msingi kwani kutapunguza vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wagombea wanawake.
Anasema tunatamani sana mkakati huo ukafanyiwa kazi ipasavyo, kwani wanawake waliowengi wanarudi nyuma kujingiza majimboni kugombea, kwani wanaogopa vishindo ambavyo hujitokiza katika kipindi cha Uchaguzi mkuu.
‘’Kama kweli Jeshi la Polisi litatekeleza vyema mkakati wao hu wa kuweka ulinzi kwa wagombea wanawake, itakua ni chachu ya ukuwaji wa harakati za kisiasa katika Nchi yetu,’’anasema.
Maryam Saleh Juma aliegombea Ubunge jimbo la Ole mwaka 2020, kupitia chama cha Ukombozi wa Uma (CHAUMA ) anasema, endapo wagombea wanawake watawekewa ulinzi madhubuti, kutasaidia kuwatoa hofu na kua na imani ya maisha yao wakati wote wa Uchaguzi.
JAMII
Juma Kombo Hamad mkaazi wa wingwi Wilaya ya Micheweni Pemba anasema wakati wa Uchaguzi kumekua kukijitokeza vurugunyingi na kupelekea wanawake wengi kuogopa kugombea kwa kuhofia juu ya usalama wao.
‘’Ni jambo jema Jeshi la Polisi kuhakikisha linaimarisha ulinzi ili kuhakikisha wagombea wanawake wanaepukana na matatizo kwa wakati wote wa uchaguzi,’anasema
Faudhia Muhammed mkaazi wa Micheweni anasema kama Jeshi la Polisi litasimamia ipasavyo harakati za uchaguzi kutaepusha kutokea kwa vitendo hivyo vya udhalilishaji, kwa wagombea wanawake na hata jamii kiujumla.
‘’Tumekua tukishuhudia wakati wa Uchaguzi baadhi ya wagombea hususani wanawake wamekua wakikumbana na vitendo vya kikatili, jambo linalorejeshanyuma juhudi za wanawake katika kufikia ndoto zao,’’anaeleza.
VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA
Habib Ali Khamis katibu wa Chama cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA) kanda ya Pemba anasema kama Jeshi la Polisi litasimama kuwalinda wagombea wanawake katika kipindi chote cha Uchaguzi, itakua ni chachu ya wanawake kugombea kwa wingi majimboni katika uchaguzi wa mwaka huu.
‘’Kama watawalinda wagombea wanawake wa vyama vyote, kama walivyoeka ulinzi kwa wagombea wa Uraisi, kwa kipindi chote cha uchaguzi kutawafanya wanawake wasiogope kugombea, kwani itakua wana ulinzi wa kutosha’’anaeleza.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Micheweni kichama Rashid Khalid Salim , analipongeza Jeshi la Polisi kwa kuandaa mkakati huo wa kuwahakikishia wagombea wanawake usalama wao kwani kutatoa fursa zaidi kwa wanawake wengi kuingia majimboni kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.
WANAHARAKATI
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar Mzuri Ali Issa anasema, hofu ya usalama ni jambo linalozuia wanawake wengi kushiriki siasa.
“Wanawake hukumbwa na vitisho vya moja kwa moja vinavyohatarisha maisha yao na ya familia zao, hili huwatisha hata wale walio tayari kugombea,” anasema.
Anaeleza, kutokana na wanawake na makundi maalumu kuwa na wasi wasi na vurugu za uchaguzi, anapendekeza kifungu kipya kinachozungumzia ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi ambacho kinaitaka Tume ya Uchaguzi kuwa na Polisi mahususi kwa ajili ya uchaguzi na kuwapangia majukumu kwa namna ambavyo itafaa.
Mshauri Elekezi na Mchambuzi Masuala ya Utawala Bora na Mtetezi wa Demokrasia, Almas Suleiman anasema, ili nchi iwe na demokrasia lazima isimamie yale ambayo wananchi wake wanayataka kwa mustakbali mzuri.
‘’Siasa safi kwa kila mmoja ni wajibu kusimama na kuwajibika kwa nafasi yake ikiwezekana demokrasia ya kweli, itachukua nafasi yake na sio kuilazimisha kwa nguvu”anamalizia.
MWANASHERIA
Mwanasheria wa kujitegemea kutoka wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba Khalfan Amour Mohamed anasema Jeshi la Polisi likisimamia sheria zao ipasavyo na wakaweza kuweka ulinzi wa hali ya juu kwa wagombea wanawake katika uchaguzi wa mwaka huu, kutawafanya waondokane na woga na kupelekea kuingia majimboni kwa wingi.
‘’Endapo Jeshi la Polisi litasimamia ipasavyo wanawake watakua huru, na watagombea, na kuingia kwa wingi katika ngazi za maamuzi,’’anaeleza
Moja ya jukumu la Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2024, ni kuandaa na kusimamia Kanuni za Maadili ya Uchaguzi.
Comments
Post a Comment