Jamii yatahadharishwa kuachwa nyuma wanawake wenye ulemavu mradi mabadiliko tabia nchi

 







                                 Na Fatma Hamad- Pemba

…...hana mguu, hana mkono, haoni, atawezaje kutunza mazingira…….

HAYO NI MANENO ya ALi  Juma Mbarouk  kiongozi wa kamati ya uhifadhi mazingira Chwale anasema wanawake wenye ulemavu ni vigumu kuingizwa kwenye kamati za utunzaji mazingira.

Anasema kamati yake, ina wajumbe 15, kati ya hao hamna hata mjumbe mmoja mwanamke mwenye ulemavu.

Anasema hajamshirikisha  mwanamke yeyote mwenye ulemavu, kwani anadhani hawezi kufanya shughuli hizo za uhifadhi kutokana na hali zao.

‘’Mtu aliekua hana mguu, hana mkono, wala haoni atawezaje kupambana na mabadiliko ya tabianchi hasa kwa kuwemo ndani ya kamati,’’anasema.

VIONGOZI/WAJUMBE WA KAMATI

Fatma Shaaban Mohamed ni kiongozi wa kamati ya kilimo mseto Shehia ya Mjini kiuyu, anasema katika kamati yake anao wajumbe 25 mtu mwenye ulemavu hana hata mmoja.

Anasema hajawahi kumpa elimu ya mabadiliko ya tabianchi, mwanawake yeyote  wenyeulemavu.

‘’Kwakweli sijawatafuta wenye ulemavu nawao nikawaingiza katika harakati hizi za utunzaji wa mazingira,’’anathibitisha.

Bakar Hamad kutoka kamati ya upandaji wa mikoko ya Kambini kichokochwe ambaye, kamati yake inao wajumbe  55, kati ya hao hakuna mjumbe mwanamke hata mmoja mwenyeulemavu.

Anasema alitoa elimu kwa wananchi wote, ingawa wanawake wenye ulemavu hawakuitikia ipasavyo wito huo, juu ya  kujiunga na kamati hizo za mabadiliko ya tabianchi.

‘’Mabadiliko ya tabianchi yanaathi watu wote, ila nashangaa sijui kwa nini wenzetu hawa wenye ulemavu hawajajitokeza,’’anajiuliza.

Kamati, inayojishughulisha na kilimo mseto ya Mchanga mdogo ambayo inaongozwa na Anu Omar Juma,  ndio kamati pekee na  ya kupigiwa mfano ambayo, imewashirikisha wanawake wenye ulemavu.

Anasema kamati hiyo inawajumbe sita (6) wote ni wanawake, wawili wakiwa ni wenye ulemavu.

Aliamua kuwaelimisha wanawake wenye ulemavu wajiunge katika kamati hizo, ili kuona nawao wanajiinua kiuchumi, kupitia shughuli hizo za uhifadhi.

‘’Watu wenye ulemavu nawao wanauwezo wa kutunza mazingira, ndio maana nikawashirikisha ili waweze kupiga hatua juu ya mabadiliko ya tabianchi,’’anasimulia.

Asya Abeid Said  mjumbe wa kamati ya kilimo msitu shehia ya Mjini kiuyu, anasema  wanawake wenye ulemavu, hawajashirikishwa kwenye harakati za mabadiliko ya tabianchi.

‘’Kwa kweli wenzetu wenyeulemavu hatujawatendea haki, ni lazima tujitafakari, kwani kunapotokea kiangazi, wao ndo waathirika wakubwa,’’anafahamisha.

Chumu Mbarouk Omar  mjumbe wa kamati ya uhifadhi  mazingira shehia ya Kambini kichokochwe, anasema bado jitihada za kuwashajiisha wanawake wenye ulemavu,  kujiunga na kamati hizo ni ndogo.

WANAWAKE WENYEWE WENYE ULEMAVU

Mwajuma  Kombo ambae ni  mwenye ulemavu wa uoni,  mkaazi wa shehia ya Mjini kiuyu, anasema bado hajashajiishwa kujiunga kwenye kamati za uhifadhi wa mazingira.

Anasema athari za mabadiliko ya tabianchi zinawaathiri watu wote, sasa iweje kama kweli wameshirikishwa wakatae kutunza mazingira.

‘’Inapotokezea mvua, jua, sisi wanawake wenye ulemavu tunaathirika kwa kiasi kikubwa, tunahitaji tupewe elimu ya mabadiliko ya tabianchi, ili tuweze kukabiliana nayo,’’anafafanua.

Anaona hakuna mtu yeyote, anaekataa jambo lenye kuleta tija, ingawa kwa eneo hili la kukabiliana na mabadiliko tabia nchi wamesahauliwa.

Maryam Khamis Bakari mwenye ulemavu wa uziwi mjumbe kutoka shehia ya Mchanga mdogo, anasema ameshirikishwa katika kamati ya kilimo msitu, ili aweze kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Anasema licha ya ulemavu wake, amekuwa akifanya vizuri kama wengine wasio na ulemavu, juu ya utunzaji wa mazingira.

‘’Tayari nimeshatayarisha shamba langu vya kutosha, na sasa changamoto  yangu ni mbegu tu, ili niwe mtu wa mbele wa kukabiliana na hali ya hewa,’’anasema.

Anasema alifuatwa nyumbani kwake na kupatiwa elimu ya mabadiliko ya tabianchi, na anasema amekua mstari wa mbele kuifanyia kazi elimu hiyo.








JAMII

Asha Ali Khamis mkaazi wa Mchangamdogo anasema wenye ulemavu wanauwezo wa kufanya kazi na wanauwezo wa kujitegemea wenyewe kiuchumi,hivyo ipo haja nawao washirikishwe.

Hamad Ali Omar mkaazi wa Mjini kiuyu, anasema athari za mabadiliko ya tabianchi zinawakumba watu wote, kwanini na wao wasishirikishwe wakaweza kuepukana nayo.

KAULI  ZA  VIONGOZI WA SERIKALI  JUU YA WATU WENYE ULEMAVU

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Bi Salma Saadat Haji, anasema Watu wenye Ulemavu wana haki ya kushirikishwa katika nyanja zote kama raia wengine.

Hidaya Mjaka Ali katibu wa Jumuia ya wanawakewenye ulemavu kisiwani Pemba anasema mikakati yao, ni kuwashajiisha wanajamii kuwapa fursa, ili na wao washiriki katika harakati zote.

WANAHARAKATI

Chama cha Wandishi wa habari wanawake (TAMWA) Zanzibar kimekua ni mdau mkubwa wa kuielimisha jamii kuacha ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu, hasa katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, Nairat Abdullah Ali anaeleza.

Saada Juma Segeja ni Afisa kilimo mseto kutoka taasisi ya Uhifadhi Misitu Pemba (CFP)  anasema lengo la mradi huo, ni kuona watu wote, wanaelewa wa athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

‘’Tunataka jamii yote inufaike na fursa hiyo ya utunzaji wa mazingira, kwani tatizo la mabadiliko ya tabianchi ni kikwazo kwa watu wote,’’anaeleza Saada.

ATHARI

Aisha Abdala Juma Afisa utawala kutoka Shirikisho la jumuia za watuwenyeulemavu Zanziba (SHUJUWAZA)  Ofisi ya Pemba, anasema endapo watu wenyeulemavu hawatopatiwa  elimu ya mabadiliko ya tabianchi, wanaweza kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.

NINI KIFANYIKE

Nivyema watuwenyeulemavu kushirikishwa katika fursa zinazokujanchini, ili nawao wapate kunufaika nazo wasiachwenyuma, Hidaya Mjaka kutoka Umoja wa wanawake wenye ulemavu Zanziba upande wa Pemaba anafahamisha.

Kutokana na mabadiliko ya tabaianchi ambayo yameonekana kuiathiri kwa kiasi kikubwa jamii, Tasisi  ya upandaji misitu Pemba (CFP) wakishirikiana na wenzao wa kimataifa CFI kwa ushirikiano wa karibu na Tamwa Zanzibar, wakaja na mradi wa  miezi 30 wa uhiadhi mazingira.

Mradi ambao unafadhiliwa na Ubalozi wa Canada  ikishirikiana na serikali ya Mapinduzi Zanzibar, unatekelezwa katika shehia za Mkijini Kiuyu, Mchanga mdogo, Kambini kichokochwe na Chwale katika Wilaya ya Wete Pemba.

Kwa upande wa wajumbe wa kamati hizo nne za uhifadhi wa mazingira  wapo 101, kati yao watu wenye ulemavu ni wawili (2) tu,  ambapo ni sawa na asilimia 2 ya wajumbe wote.

Kamati hizo  ambazo zina viongozi tisa (9) hakuna hata mwanammke mmoja, mwenye ulemavu

NYARAKA

Licha ya kuachwa nyuma kwenye kamati hizo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka muongozo maalum, ili maendeleo ya nchi yasiwaache nyuma Watu wenye Ulemavu, kwa kuimarisha muundo wa taasisi ya Watu wenye Ulemavu.

Eneo jengine ni uwepo wa sheria nambari 8 ya mwaka 2022 ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar, nayo kifungu cha 28 (e) kinaeleza kundi hilo, linahaki ya kuishi kwa kujitegemea na kujumuishwa katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Kimataifa, nako haki ya kushiriki katika harakati za kimaendeleo, imeelezwa kwenye ibara ya 9 ya mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu ulioridhiwa na Tanzania mwaka 2009.

Hata Katiba ya Zanzibar ya 1984  Kifungu cha 21 (3) kinaeleza, wazi kuwa, ‘kila mzanzibari anayo haki ya kufanya kazi na anastahili fursa na haki sawa, kwa masharti ya usawa ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyoko chini ya mamlaka ya Zanzibar’.

CHANZO MITANDAO

Ripoti mpya ya Hali ya Hewa na Maendeleo (CCDR) kwa Tanzania iliyozinduliwa na Benki ya Dunia (WB) imetaja hatua tano zinazoweza kuchukuliwa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Moja wapo ni kuwajengea uwezo na uelewa wa kukabiliana na hatari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi wanawake na makundi mingine. 



Comments