Wanawake watakiwa kugombea nafasi za uongozi

 

NA FATMA HAMAD, PEMBA

WANAJAMII Wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba wamesema, kutokugombea nafasi za uongozi kwa wanawake, ni jambo moja linalorejesha nyuma maendeleo yao.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti walisema, ili kuondokana na  changamoto mbali mbali zinazowakabili ndani ya jamii zao, ni kuhakikisha wanawake wanagombea nafasi za uongozi.

Mwananchi Biache Othman Ramadhan mkaazi wa Sizini alisema, iwapo akina mama  wataweza kujitoa wenyewe katika kugombea nafasi mbali mbali za uongozi, mambo yanayowakwaza yatatatuka kwa urahisi, kwani wataweza kuyasemea wenyewe kwenye vyombo vya kutoa maamuzi badala ya kusubiri wanaume kuwasemea.

"Katika kugombea nafasi za uongozi kwa wanawake hakuna kizuwizi, isipokua sisi wenyewe tuwe tayari ili kuibua changamoto zinazosababisha tusiweze kugombea na kuhakikisha zinatatuliwa" alisema.

Nae Salma khamis Tumu mkaazi wa Tumbe  alisema, imezoeleka siku zote mwanamke kuwekwa katika kundi la mwisho na kusababisha kunyimwa haki zao zinazowahusu.

Fatma Rashid Ali wa Micheweni alisema, tatizo kubwa linalopelekea wanawake kutogombea nafasi za uongozi ni dhana potofu kwa jamii ya kuwa, wanawake hawawezi kuongoza na ndio maana nafasi nyingi huchukuliwa na wanaume.

"Nivyema kila mmoja kutimiza wajibu wake ikiwemo kupewa moyo kwa watoto wa kike, ikiwa ni pamoja na kuwasomesha hadi elimu ya juu ili waweze kua na ujasiri wa kusimama imara katika kugombea nafasi hizo" alisema.

Akizungumzia sababu ya kupewa nafasi za uongozi wanaume huku wanawake wakiwekwa nyuma, mwananchi Juma Kombo Hija  alisema ni kutokana na mfumo dume uliokuwepo zamani, ingawa kwa sasa umeanza kuondoka hivyo ni wakati kwa wanawake kujitoa katika kugombea nafasi hizo kwa maslahi ya taifa.

Ali Sharif Mkaazi wa Mjini wingwi alisema, kikwazo kikubwa kwa wanawake hadi sasa ni kushindwa kusimama kwenye majukumu na kuweza kuzungumza, jambo ambalo linachangia kuonekana bado hawajaweza kushika nafasi.

Alisisitiza kwamba ni vyema jamii ianze kumuandaa mwanamke kwa namna mbali mbali ili kujakua kiongozi bora, kuanzia ndani ya familia ili kuhakikisha wanawake wanakua imara na wenye uwezo mkubwa katika kuongoza.

Nae Kaimu Mkugurugenzi wa Jumuia ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Micheweni Saleh Hamad Juma alisisitiza kua, watu wote wana haki sawa, na katiba zote hazijambagua mwanamke, hivyo ni vyema kuendelea kupata fursa na haki kama ilivyo kwa wanaume.


Tatu Abdala Mselem ni Mratibu wa Jumuiya inayoshughulika na makundi maalumu wakiwemo wanawake, watoto wenye ulemavu, watoto yatima, vijana na wazee wasiojiweza (TUJIPE) alisema, wanawake wamehamasika kujitokeza kugombea, lakini wanashindwa kuchukua nafasi.

‘’Bado suala la kifedha ni gumu kwa wanawake, kwani wengi wao wanaogombea wanatoka kwenye mazingira ya kimaskini,” anafafanua Tatu.

Afisa Mkuu wa Mahusiano kutoka chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Zanzibar Sophia Ngalapi alisema, wamekua kiguu na njia kwa ajili ya kuwaelimisha wanawake waweze kuingia majimboni kugombea.

‘’Ndoto zetu ni kuona wanawake wanaingia kwa wingi kwenye vyombo vya maamuzi, lakini gharama za uchaguzi bado zimekua zikiwakosesha kufikia malengo yao,’’alisema. 

Comments

Popular posts from this blog

KERO YA MAJI, TATIZO KWA WANAKIJIJI CHA GOMBEUME

HIVI NDIVYO UTELEKEZWAJI WA WATOTO UNAVYOATHIRI MALEZI, MAKUZI YAO

DNA YA THIBITISHA, MTUHUMIWA NDIE BABA MZAZA WA MTOTO