Wananchi wahimizwa kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura
NA FATMA HAMAD PEMBA.
Wananchi ambao wameshafikia sifa za
kuwa wapiga kura wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika uboreshaji wa Daftari la kudumu la
mpiga kura linalotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Wito huo umetolewa na Makamo mwenyekiti wa Tume huru ya
Taifa ya Uchaguzi Jaji mstafu wa Mahkama ya Rufaa Mbarouk Salim Mbarouk katika mkutano wa wadau
wa Uchaguzi kuhusu uboreshwaji wa Daftari la kudumu la mpiga kura, huko Makonyo
Chake chake Pemba.
Amesema ili
kufanikisha ipasavyo zoezi hilo ni vyema wananchi kushirikiana na tume huru ya
uchaguzi,na kuhakikisha wenye sifa za kuwa wapiga kura wanajitokeza
kujiorodhesha kwenye daftari hilo.
‘’Ndugu
wananchi tufahamu Tume huru ya uchaguzi imeanza na zoezi la uboreshaji wa
Daftari la kudumu la mpiga kura,hivyo tuhakikishe kila mwenye sifa anapata haki
yake hiyo,’’alisema.
Alisema kwa
mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria namba Moja ya mwaka 2024, Sheria ya
Uchaguzi wa Rais, Madiwani na wabunge itahakikisha inamuandikisha katika Daftari la kudumu la mpiga kura
mwananchi yoyote wa Tanzania aliekosa sifa ya kujiandikisha kwenye Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar.
Alieleza
kuwa kwa upande wa Pemba Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 8,162
ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 ya wapiga kura wapya45,643waliopo kwenye
Daftari la kudumu la wapiga Kura.
Aidha
aliendelea kusema kuwa jumla ya vituo 40,126 vya kuandikisha wapiga kura
vitatumika katika uboreshaji wa Daftari mwaka huu wa 2024.
Alieleza
kuwa kwa upande wa Tanzania bara kuna jumla ya vituo 39,709, ikiwa Zanzibar ni
417, ambapo kuna ongezeko la vituo 2,312ikilinganishwa na vituo 37,814
vilivyotumika mwaka 2019/2020.
Aidha
aliwasihi viongozi wa vyama vya siasa kuepuka kuingia katika vituo vya kuandikisha ili kuepusha vurugu
wakati wa zoezi hilo.
‘’Niwaombe
ndugu viongozi kama kutatokezea tatizo basi ni vyema mkafuata njia sahihi kwa
ajili ya kwenda kupeleka malalamiko yenu, na sio kuingia kwenye vituo ya
uandikishaji,’’alieleza kwa msisitizo.
Mapema akiwasilisha mada ya uboreshaji wa Daftari la mpiga Kura Kaimu mkurugenzi wa Uchaguzi Giveness Nswile alisema kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani sheria namba moja ya mwaka 2024 miongoni mwa wananchi ambao hawana sifa za kuandikishwa katika Daftari hilo ni mtu asie na akili timamu, pamoja na asiekua raia wa Tanzania.
Kwa upande
wake Balozi Omar Ramadhan Mapuri aliwasisitiza wadau walioshiriki mkutano huo
kuwa mabalozi wa kuwaelimisha jamii kuhakikisha wanajitokeza kwenye Daftari hilo ili waweze kuja kupata fursa yao ya
kuwachaguwa Viongozi wanaowataka hapo mwakani.
Nao
washiriki wa mkutano huo wameihakikishia Tume huru ya Taifa kutoa elimu kwa
jamii na kuhakikisha kila mwenye sifa anapata haki yake hiyo.
Kauli mbiyu
ya zoezi hilo la uboreshaji wa Daftari kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa Uchaguzi bora.

Comments
Post a Comment