Gharama za Uchaguzi zinavyokatisha ndoto za wanawake wanaogombea.
Wasema hali isiporekebishwa majimbo yataendelea kuwa magumu kwao
Na Fatma Hama, Pemba
‘’NATAMANI kugombea tena
uongozi katika uchaguzi ujao wa mwaka 2025, lakini kila nikifikiria gharama…nakata
tamaa,’’
Hayo
si maneno ya mtu mwengine bali ni ya mwanamama Tumu Mwalim Massoud mwenye miaka
40 mkaazi wa Wingwi Limani wilaya ya Micheweni Pemba, ambae aligombea uwakilishi
Jimbo la Wingwi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka
2020.
Mwanamama
huyo kiu yake ni kuwa mwakilishi ili aweze kutetea haki za wananchi, ingawa
anakumbuka gharama zilizomtoka katika uchaguzi wa mwaka 2020 na hatimae
kushindwa katika kura.
Anasema,
kwa hali hiyo ndoto nyingi za wanawake wenye nia ya kugombea zitakatika na
majimbo yataendelea kuongozwa na wanaume watupu, ambao kuna baadhi ya mambo
yanaowahusu hawawezi kuyatetea.
Ni
mwaka wa 23 tangu Tumu aingie kwenye harakati za kisiasa, lakini anaanza
kupoteza matumaini kutokana na gharama kubwa asizoweza kuzimudu kwenye mambo ya
uchaguzi.
Tumu
anasilimulia kuwa, hakua na mtu wa kumsaidia gharama isipokua ni yeye mwenyewe
pamoja na familia yake ambayo iliyoikimchangia pesa kwa ajili ya kufanyia
kampeni.
‘’Unataka
ufanye mikutano kwenye jimbo lako, unahitaji upate usafiri, vipaza sauti,
wasanii, wandishi wa habari na vyote hivyo vinahitaji gharama ila sasa utazitoa
wapi,” anauliza Tumu.
Chama
chake kilimsaidia pesa kidogo mwishoni mwa kampeni, jambo lilimfanya akope
fedha kwa ajili ya kuendesha kampeni zake,” anasema.
Baada
ya kumalizika kwa uchaguzi na kushindwa, alianza kuuza mali zake na za familia
yake ili apate fedha ya kulipa madeni.
‘’Kwa
sasa najifikiria kugombea tena kwa sababu nakumbuka maumivu ya kulipa madeni,
ingawa natamani niingie tena kwa sababu ndoto yangu ya kuwa kiongozi
haijakamilika,’’ anasema.
Anasema,
wanawake wengi wamekuwa na ndoto ya kuwa viongozi ingawa mwisho hukata tamaa na
kushindwa kufanikisha malengo yao kutokana na kukosa pesa za kuendeshea
shughuli za uchaguzi.
Tumu
ana elimu ya ngazi ya diploma ya masuala ya Kompyuta (IT) na ana watoto Saba
(7) ambao wanamtegemea.
Sio
Tumu pekee mwenye kilio hicho bali kuna wanawake wengi ambao wanakwama kutokana
na kukosa fedha za kujigharamia kwenye kugombea…
Ambapo
mwanamama Ziada Khalfan Saleh mwenye miaka 48 mkaazi wa Machomane Wilaya ya
Chake Chake nae ni miongoni mwa wahanga.
Yeye
aligombea ubunge Jimbo la Ziwani zaidi ya mara tatu kupitia Chama Cha Tanzania
Labour Party (TLP) huku akishindwa kufanya mikutano kutokana na ukosefu wa fedha.
‘’Ninachokifanya
mimi ni kupiga hodi nyumba baada ya nyumba na kuomba kura, kweli kwa hali hii nitalipataje
Jimbo wakati nyumba siwezi kuzimaliza na sina uwezo wa kufanya mikutano ya
kampeni,’’ anaeleza.
Anasema,
ni wakati sasa Serikali kutoa ruzuku kwa vyama vyote na sio tu kwa vyama
vikubwa, ili ziwawezeshe wanawake kwenye kampeni ambapo itakuwa ni sababu ya
wao kufanikiwa kuwa viongozi.
Hata
mwanamama Asha Ali Mohamed miaka 45 aliewahi kugombea Jimbo la Wawi Wilaya
Chake Chake kwa zaidi ya mara tatu kupitia Chama cha United Democratic Paty
(UDP) nae alikumbwa na kadhia hiyo ambapo anasema gharama za uchaguzi ni
kikwazo kikubwa kinachowanyima usingizi wanawake kisiwani Pemba.
‘’Kama
ningekuwa ninapesa za kufanyia kampeni katika maeneo yote ya jimbo langu
naamini ningeshinda, kwani kila nikigombea idadi ya kura huwa
zinaongezeka,’’anasema mama huyo.
Kila
siku zinapoendelea, wanawake wanaojitokeza kugombea wanakata tamaa, hivyo Serikali
pamoja na Tume ya Uchaguzi ikiwa hawatoviangalia kwa jicho la pili vyama vya
siasa hususani vidogo vidogo kutapelekea kutokuonekana majimboni.
Riziki
Mgeni Juma mwenye umri wa miaka 42 mkaazi wa Mtambwe wilaya ya Wete Pemba ambae
aligombea udiwani wadi ya Mtambwe kupitia Chama cha Demockrasia na Maendeleo (CHADEMA)
alifanya kampeni ya nyumba kwa nyumba na maskani, ili awafikie wananchi 16,237
wa wadi yake.
‘’Sikuwa
na uwezo wa kufanya mikutano na ndio maana nikaamua kupiga hodi nyumba baada ya
nyumba kuomba kura, lakini sikuwafikia wote,’’ anaeleza.
WANACHAMA
WA VYAMA VYA SIASA
Arafa Ahmad Juma mkaazi wa Tundaua Chake Chake
ni mwanachama wa Chama cha Civic United Front (CUF) anasema, wanawake wengi wanaogombea
hususan wa vijijini wanakua ni maskini hawamudu Gharama za chaguzi
Juma
Kombo Hamad mwanachama wa Chama cha Alliance for Change and Transpareny (ACT WAZALENDO)
mkaazi wa Wingwi Micheweni, anasema suala la uchaguzi linahitaji gharama, kwani
wanawake wengi wanaogombea hawana ajira rasmi.
‘’Kama
Serikali hawajalikalia kitako, hio 50 kwa 50 ya usawa wa kijinsia kwenye ngazi
ya mamuzi haitofikiwa,’’anasema.
Katiba
ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 21 (3) kinaeleza kwamba, kila mzanzibari
anayohaki ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyoko chini ya
Mamlaka ya Zanzibar.
Sensa
ya watu na makazi ya mwaka 2022 Zanzibar ina wanawake wengi ambao ni 974,281
sawa na asilimia 51.6 kuliko wanaume, ikiwa wao ni 915,492 sawa na 48.4 ambapo
licha ya uwingi huo bado idadi kwenye ngazi za maamuzi ni kidogo.
Kati
ya hao, ni asilimia 21.14 tu kwa wanawake 71 waliojitokeza kugombea udiwani.
Kwa
nafasi ya uwakilishi wanawake waliogombea ni 251, wakiwemo wanaume 190 na
wanawake 61, ambapo walishinda wanaume 42 na wanawake nane (8) sawa na asilimia
16, wabunge walioshinda
wanawake ni wanne sawa na asilimia 8,
VIONGOZI
WA VYAMA VYA SIASA
Abass
Mohamed Khatib Mratibu wa Chama cha Demokrasia Makini (DP) kisiwani Pemba anasema,
mara nyingi chama chao kimekua kikiwasaidia wagombea wanawake gharama za uchukuaji
wa fomu tu na sio kwenye kampeni.
‘’Hatuna
ruzuku yoyote tunayoipata kutoka Serikalini, hivyo hatuna msaada wowote wa
kuwasaidia ili waweze kujigharamia kwenye kampeni wakati wa uchaguzi,” amekiri
Abass.
Mohamed
Haji Kombo ambae ni Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Chake Chake
anasema, umasikini ni kilio kikubwa kinachowakosesha nafasi wanawake waliopo kwenye
siasa kupata nafasi za uongozi.
‘’Tume ya Uchaguzi Zanzibar ni chombo
kinachoendeshwa na Serikali, kwanini kishindwe kuwasaidia wanawake na kuonekana
wameingia kwa wingi kwenye nafasi za Uongozi?’ amehoji Mohamed.
Katibu
wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Micheweni Khamis Juma Omar anasema, chama
chao kimekua kikiwawezesha wanawake kwa kuwapatia mitaji ambayo itawainua
kwenye shughuli zao hizo za uchaguzi.
‘’Anaposimama mgombea, hasimami kama Asha wala Halima pekee, bali chama ndicho kinachomsimamia na kumuwezesha hata kwa pesa kidogo ili aweze kufanikiwa,’’ anasema KhamiS
WANAHARAKATI
Tatu
Abdala Mselem ni Mratibu wa Jumuiya inayoshughulika na makundi maalumu wakiwemo
wanawake, watoto wenye ulemavu, watoto yatima, vijana na wazee wasiojiweza (TUJIPE)
anasema, wanawake wamehamasika kujitokeza kugombea, lakini wanashindwa kuchukua
nafasi.
‘’Bado
suala la kifedha ni gumu kwa wanawake, kwani wengi wao wanaogombea wanatoka
kwenye mazingira ya kimaskini,” anafafanua Tatu.
Afisa Mkuu wa Mahusiano kutoka chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Zanzibar Sophia Ngalapi anasema, wamekua kiguu na njia kwa ajili ya kuwaelimisha wanawake waweze kuingia majimboni kugombea.
‘’Ndoto
zetu ni kuona wanawake wanaingia kwa wingi kwenye vyombo vya maamuzi, lakini
gharama za uchaguzi bado zimekua zikiwakosesha kufikia malengo yao,’’anasema.
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA.
Abdul-Razak
Said Ali ambae ni Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Zanzibar amekiri kuwepo kwa gharama katika chaguzi na kusema, kwasasa baadhi ya
kanuni zinazoonekana kuwa na ukakasi ingawa tayari zipo katika mchakato wa
kufanyiwa marekebisho.
‘’Sasa
hivi kanuni zipo katika hatua za mwisho za kufanyiwa marekebisho, hivyo
tusubirie mabadiliko vipi Sheria itatoa kipaombele katika suala la gharama kwa
wanawake,’’anafafanua Abdulrazak.
GHARAMA
ZA KUFANIKISHA KUWA MWAKILISHI.
Kwa
mujibu wa utaratibu ulivyo, anaetaka kugombea uwakilishi anatakiwa alipie chamani
shilingi laki 100,000 kwa kuchukua fomu.
Pia
anatakiwa kulipa Tume ya uchaguzi shilingi laki 200,000, wakati huo huo ukitakiwa
kuchukua fomu ya pingamizi ambayo ni shilingi 300,000.
Licha
ya gharama hizo za kununua fomu ya uwakilishi ili uweze kugombea na kutambulika
kuna mambo ya lazima mgombea anatakiwa ayafanye ambayo yanawakwaza.
Kwa
mujibu wa utaratibu uliowekwa na chama lazima uprinti picha kwa ajili ya
kupachika kwenye kuta katika jimbo lako, kuwalipa viongozi siku ambayo wanakwenda
kupiga kampeni ya nyumba kwa nyumba.
Vile
vile wanahitajika kununua nguo (Sare) yoyote itakayotolewa na chama, pamoja na
kuwalipa mawakala ambao watasimamia siku ya uchaguzi.
NINI
KIFANYIKE
Hadia
Omar Ali mkaazi wa Micheweni anasema, ikiwa Serikali haitokipatia ufumbuzi
kilio hicho siku zote wanawake wataendelea kushikia mkia tu kwenye mamuzi.
Mkaazi
wa Finya wilaya ya Wete Khamis Mohamed Kombo anasema, ipo haja kwa Tume ya
Uchaguzi (ZEC) kuweka ruzuku malumu ambayo itawasaidia wagombea hususan wanawake.
SERA
Sera
na Sheria mbali mbali za Zanzibar zimeelekeza kutambua haki ya mwanamke
kushiriki katika demokrasia na uongozi.
Kifungu cha 21 (2) cha Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 64 kimeeleza kwamba, kila mzanzibari anayo haki na uhuru wa
kushiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu mwanamke
na taifa lake.
ILANI
YA UCHAGUZI YA WANAWAKE.
Ilani
ya Uchaguzi ya wanawake, Uchaguzi wa Serikali za mitaa ya mwaka 2019 na
Uchaguzi mkuu wa 2020, Madai ya mtandao wa
wanawake wameitaka serikali kusimamia matumizi ya rasilimali fedha, hususani
ruzuku zitokanazo na kodi ya Watanzania, ili kuhakikisha zinatumika kwa kuziba
mapengo ya jinsia wakati wa uchaguzi.
ILANI
YA CHAMA CHA MAPINDUZI.
Moja
ya mkakati wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2024 imesema, ni
kuwawezesha wanawake kushiriki katika ngazi mbali mbali za mamuzi.
Comments
Post a Comment