TIGO ZANTEL wautunisha mfuko wa fidia kwa wanaoanguka mkarafuu
NA FATMA HAMAD,PEMBA
Mtandao wa simu wa Tigo Zantel
umechangia shilingi milioni 350 kwenye mfuko wa fidia kwa ajili ya watu
wanaopata ajali ya kuanguka mkarafuu wakati wakiwa katika harakati za uchumaji
wa zao hilo.
Akizungumza mara
baada ya kukabidhi mfano wa hundi ya milioni 350, huko Makonyo Chake ghake Pemba, Mkurugenzi wa mtandao wa Simu wa Tigo
Zantel Azizi Said Ali alisema wameamua kuchangia fedha hizo, ili
kuuboresha
mfuko huo ambao utawanufaisha wahanga.
‘’Kwa vile
na sisi Tigo ni sehemu ya familia tumeamua kutoa mchango wetu ili kuona
wanaopata ajali nawao wanaingizwa katika bima maalum,’’alisema.
Akifungua
hafla hiyo ya ugawaji wa zawadi kwa washindi wa vuna na Tigo pesa, Waziri wa
biashara na Viwanda Zanzibar Omar Said Shaban amewataka wakulima wa zao hilo
kuendelea kutumia mfumo wa malipo wa Tigo pesa katika kuuza karafuu zao.
‘’Niwaombe
wananchi wenzangu endelea kuunga mkono mfumo huo,msisikilize maneno ya
wasiopenda maendeleo,’’alieleza.
Aidha aliutaka
uongozi wa Tigo pesa katika msimu wa vuna na tigo pesa ujao, kuhakikisha
wanatoa zawadi ya gari kwa wakulima watakaouza karafuu zao na kupokea malipo
kupitia Tehama, ili kuwatia hamasa wananchi kuutumia mfumo huo.
Akiwasilisha
mfumo huo wa Tehama Mkurugenzi mkuu wa Tehama kutoka shirika la Biashara la
ZSTC Najma Nuhu alisema kuna hatua tano ambazo mkulima atazipitia kabla ya
kupokea malipo yake.
Alisema
miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na Usajili, Kutoa daraja, Kuchunga ili kupata
karafuu safi, Kupima na mwisho ni malipo.
Alifahamisha
kwa kupitia mfumo huo mkulima atapokea ujumbe wake wa malipo kwenye simu yake
kabla ya kuondoka kituo cha kuuzia karafuu.
‘’Mfumo wetu
ni wa papo kwa papo mkulima atapokea malipo yake akiwa yupo pale pale kituoni,’’alisema.
Nao wakulima ambao wamepokea zawadi walisema utaratibu huo ambao wameufanya Tigo zantel wa kutoa zawadi, utawahamasisha wananchi kuuza karafuu zao kwa kutumia mfumo huo wa kisasa
Katika hafla hiyo jumla ya washindi 25 wa Vuna na Tigo pesa walizawadiwa zawadi, ambapo 20 wamezawadiwa simu janja, Watatu walipokea Baskeli na wawili walipatiwa Piki piki.
Comments
Post a Comment