MTAZAMO WA UISLAMU NA MICHEZO KWA MWANAMKE
NA FATMA HAMAD, PEMBA
WATU wengi
wamekua na mawazo kwamba, uislamu unakataza mwanamke asishiriki michezo, kwani
wanahisi atavaa nguo zisizo sahihi (za uchi).
Jambo linalowatia hofu wanajamii ya kiislamu na kupelekea ushiriki mdogo wa wanawake, pengine kwa dhana za kuwa michezo ni uhuni kwao.
Na hili linaweza kuchangiwa na ushiriki mdogo kati yao na wanaume kwa michezo kadhaa ambayo mwanamke wa kiislamu alipaswa ashiriki kwa kuonesha kipaji chake.
Ingawa historia ya uislamu, inaonesha michezo ilianza tokea kipindi cha MTUME MUHAMMAD (S,A,W), kwani Mtume alikua akicheza michezo kama vile ngware, Ngumi yeye na maswahaba zake, huku akiwa amefunga pazia na mke wake Bibi Aisha (A,S) akiwa anangalia na kushangilia.
Ukhti Amina Abdala Omar Katibu wa Tasisi ya
Akinama ya Akhlasi L islamia (JAI) anasema mwanamke wa kiislamu
ameruhusiwa kucheza michezo kama atavaa nguo zake za stara.
Kuna hadithi moja Omar Bin khatwab ( R,A)
alimkuta Mtume (S,A,W) kakaa na wanawake wakiwa wanazungumza na wanacheza,
akaghadhibika kwanini wanacheza na Mtume wakiwa hawakuvaa hijabu,
Mtume
akamuambia usiwe na munkari Omari, kwani yeye shetani wake kazuiwa kuangalia maaswi,
kipindi hicho ilikua hakuja halalishwa vazi la hijabu.
Mwanamke anaruhusiwa kucheza michezo ambayo
si ya nguvu, haitopelekea kuumizana mfano mchezo wa mpira wa mikono, kuogelea,
Ngonjera.
Ingawa
kama watacheza michezo ambayo inashabihiana na wanaume kamavile mpira wa miguu,
Kupanda Minazi basi wavae nguo zao kamaili anazostahiki kuvaa mwanamke wa
kiislamu.
Hivyo ni dhahir kwamba, uislamu umerusuhu
michezo kwa mwanamke kama atafuata masharti yaliowekwa.
WACHEZAJI WANAWAKE
Mchezaji wa Simba Queens Fatuma Issa 'Fetty
Dansa', anasema yeye amejizolea umaarufu
mkubwa si tu uwanjani, bali pia kutokana na uvaaji wake wa hijabu akiwa anatandaza soka dimbani.
‘Fetty Densa’ ambaye ni nahodha wa Simba Queens iliyopo mkoani Iringa, anasema awali alikuwa hachezi na hijabu na kwa mara ya kwanza, alipoamua kuanza kuvaa ilikuwa shida, lakini kwa sasa haoni tatizo
lolote.
"Kwangu haina shida yoyote kucheza nikiwa nimevaa ushungi, ni kawaida na ninaamini kupitia mimi kuna watu wengine watajifunza kupitia hichi ninachokifanya kwa kuona ni kitu kizuri,"anasema.
Kul -thum Ali Khamis mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya Wete Star (Women Club) anasema uislamu unakataza michezo pale ambapo mtakuwa hamvai nguo za kujistiri, wakati mnapokuwepo uwanjani.
‘’Sisi tunacheza tukiwa tumevaa suruali refu, Mashati makubwa pamoja na vilemba ili kutimiza matakwa na misingi ya dini ya kiislamu,’’anaeleza.
Fatma Mkubwa Mussa mkaazi wa Mtuhaliwa Mkoani, anaecheza mpira wa mikono, anasema wanacheza wanawake watupu hawachanganyiki na wanaume huku wakiwa na nguo zao za stara.
‘’Tunacheza wanawake watupu, na tumekua tukivaa Mashungi, soksi pamoja na mabaibui, ili kukizi vigezo vya Imani yetu,’’anafafanua.
JAMII
Khadija
Abdala Nuhu kutoka Wete, anasema uislamu haujakataza mwanamke asishiriki
michezo, hiyo ni mitazamo tu ya watu kuitafsiri wapendavyo.
‘’Hivyo ni vikwazo tu vya binadamu kutuzuia wanawake tusishiriki michezo, kwani tunacheza tukiwa na nguo zetu za stara,’’anasema’.
Anaeleza kuwa, ni vyema Wizara ya Michezo kutoa taaluma kwa viongozi wa dini pamoja na walimu Madrasa, ili kuona kwamba wanawapa fursa watoto wa kike, kushiriki michezo
Abdalla Ali Abdalla wa Kiuyu Minungwini, anasema dini ya kiislamu haijambagua mwanamke kwamba asishiriki michezo, kwani na yeye ni binadamu anastahili kupata fursa zilizomo.
‘’Uislamu haujamkataza mwanamke asishiriki michezo, isipokua tu wamewekewa masharti malum ikiwa ni pamoja kuvaa nguo za stara,’’anasema.
WANAHARAKATI
Fat-hya Mussa Said, ambae ni Mratibu wa Chama
cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba, anasema
uislamu haujamkataza mwanamke asishiriki michezo, kwani historia inaonesha kwamba hata mke wa Mtume Muhammad
(S,A,W) Bi Khadija (A,S) alikua akicheza michezo na mumewe.
‘Watu wanaimani kwamba wanawake wanapocheza
watavaa nguo ambazo ni kinyume na dini, ingawa sio hivyo tunaweza kuvaanguo
zetu za kiislamu na tukaweza kufanya vizuri,’’anaeleza.
Amina Omar, Msellem anaeleza kuwa, wanawake
wanaweza kucheza na huku wakiwa wamevaa mavazi yao ambayo yanaendana na dini
yao bila ya tatizo lolote.
‘Sio lazima kwamba wanawake wavaenguo za
michezo kama za wanaume, bali wao wana weza wakava hata mashungi mbaibui ama mashati
makubwa na masuruali mapana ambayo haziwavunjii heshima,’’anaeleza.
OFISI YA MUFTI
Sheikh Said Ahmed Mohamed, kutoka Ofisi ya Mufti
Pemba, anasema mwanamke wa kiislamu ameruhusiwa kushiriki michezo kadhaa ikiwa
atakumbuka kujistiri na kuhifadhi maungo yake.
‘’Ni haramu kwa mwanamke kucheza michezo
akiwa amechanganyika na mwanamme, wacheze wanawake watupu nao wakiwa wamejihifadhi,’’anafafanua.’
Anasema endapo mwanamke atacheza michezo
akiwa amevaa nguo ambazo zimemsitiri hazioneshi maungo yake, basi si kharamu
kwa wao kushiriki michezo waitakayo.
‘’Uharamu haukuja kwenye michezo, bali
umekuja pale ambapo atacheza akiwa hakuvaa nguo ambazo sio za kujisitiri,’’anaeleza.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 12 (1) kinafafanua kuwa, watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa.
Katika utekelezaji wa Sera ya michezo ya
Zanzibar ya mwaka 2018, moja ya mkakati wa serikali, ni kuhakikisha mashindano
yanayoandaliwa Zanzibar hayasababishi athari mbaya kwa mazingira ya nchi.


Comments
Post a Comment