WANDISHI WA HABARI WAPEWA MBINU
NA FATMA HAMAD,PEMBA
Wandishi wa habari wametakiwa kujikita zaidi Vijijini, kuibua na kuziandika kero zinazowakwaza
Wananchi ili ziweze kufahamika na kupatiwa ufumbuzi.
Wito huo umetolewa na Katibu wa Mwavuli wa Asasi za Kiraia kisiwani Pemba (PACSO) Sifuni Ali Haji katika mkutano uliowakutanisha wandishi wa Habari pamoja Asasi za kiraia huko ukumbi wa Maktaba kuu Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema wananchi hususan wa Vijijini wamekuwa wakikumbana na matatizo kadhaa ikiwemo Maji, Bara bara na Udhalilishaji, hivyo endapo mtazisemea zinaweza zikatatuliwa kupitia malaka husika.
‘’Wandishi wa habari nyinyi ndio mdomo wa wanyonge, wasemeeni ili muweze kuwaokoa na
matatizo,’’alisema.
Mapema mwenyekiti wa Pacso Muhammed Ali Khamis alizitaka Asasi za kiraia kushirikiana na wandishi wa habari wakati wanapofanya kazi zao ili ziweze kusikika.
‘’Tunafahamu nyinyi asasi mmekua mkifanya kazi kubwa ya kuisaidia jamii, lakini hazisikiki ipasavyo
kwani hamuvitumii vyombo vya habari mkaweza kuzitangaza,’’alieleza.

Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo Gaspary Charles kutoka Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA) Ofisi ya Pemba alisema ushirikiano kati ya Wandishi wa habari pamoja na Asasi za kiraia kutasaidia jamii kupata haki zao wakati zitakapovunjwa.
Mkurugenzi wa Mwavuli wa Asasi za Kiraia (Pacso) Muhammed Najim alisema lengo la mkutano huo katiya Wandishi wa Habari na Asasi za kiraia ni kuzitaka asasi za kiraia kuvitumia vyombo vya habari wakatiwanapofanya kazi zao ili waweze kujitangaza na kufahamika katika jamii.
Nao washiriki wa mkutano huo walisema mkutano huo umewaonesha njia, hivyo wameahidi kuyafanyiakazi waliofundishwa ili kuona wamekua ni msaada mkubwa kwa jamii.


Comments
Post a Comment